Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

Hon. Judith Salvio Kapinga

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

MHE. JUDITH S. KAPINGA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi. Aliyekuwa Rais wa South Afrika Hayati Nelson Mandela, Mwenyezi Mungu amlaze mahali pema peponi, aliwahi kusema na nitamnukuu: “From the poorest of countries to the richest of nations, education is the key to moving forward in any society”. Kwa lugha yetu ya Taifa anasema kuanzia kwenye nchi masikini kabisa hadi mataifa tajiri kabisa elimu ndiyo ufunguo pekee wa maendeleo katika jamii yoyote. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, maneno haya kwa namna moja ama nyingine yalielezwa na Rais wetu mpendwa na anayewapenda Watanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan tarehe 6 Aprili, wakati wa hafla ya kuwaapisha Makatibu Wakuu na Manaibu Makatibu Wakuu na alisema napenda nimnukuu: “Lazima kufanya tathmini ya elimu itakayomsaidia Mtanzania. Tuangalie mitaala yetu tuone mtaala utakaotupeleka mbele na kukuza Taifa letu”. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, maneno haya ya Rais wetu mpendwa kwa namna moja ama nyingine yanatuonyesha umuhimu wa mfumo wa elimu katika kuongeza kasi ya maendeleo kwa taifa letu. Mfumo wa elimu kwa namna moja ama nyingine ndiyo unaoamua nguvu kazi ya taifa letu itasukuma vipi gurudumu la uchumi katika nchi yetu. Mfumo wa elimu ndiyo unaoamua ajira za wananchi wa Tanzania zitapatikana vipi na kwa kiasi gani. Mfumo wa elimu ndiyo unaoamua umaskini katika taifa letu utaondolewa ama utapungua kwa kiasi gani na kwa wakati gani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nasema haya kwa sababu mengi yameongelewa kuhusiana na kubadilisha mfumo wa elimu lakini mimi napenda kujikita katika namna ya kulinda mfumo wa elimu. Hata kama tutafanya mabadiliko ya mfumo wa elimu tusipolinda mfumo wa elimu ni sawasawa na kutwanga maji kwenye kinu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kabla sijaenda kwenye kueleza namna gani tunapaswa kulinda mfumo wa elimu, hapa ningependa nimpongeze mama yangu Mheshimiwa Prof. Joyce Ndalichako; kwa kipindi hiki ambacho amekua Waziri tumeona mabadiliko yasiyo na tija na ya haraka katika mfumo wa elimu, kidogo yameweza kuwa contained. Huko nyuma mabadiliko katika mfumo wa elimu yalikuwa yanaweza yakafanyika abruptly, muda wowote na ku-disturb walaji ambao kwa kiasi kikubwa ni vijana wa Taifa hili. Kwa hiyo, Mheshimiwa Prof. Ndalichako kwa kipindi hiki ambacho amekuwa Waziri, amejitahidi sana kuwalinda walaji ambao ni vijana wa Tanzania. Hongera sana mama yangu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, napenda nijielekeze ni kwanini tunapaswa kulinda mfumo wa elimu, kwa sababu mabadiliko yoyote katika Mfumo wa Elimu yanaweza kuathiri vijana wa Taifa hili kwa kiasi kikubwa sana. Tunashukuru Mungu leo tuna Mheshimiwa Prof. Ndalichako, kesho hatutakuwa naye. Kwa mantiki hiyo, inatupasa kulinda mfumo wa elimu kwa kuweka taratibu ambazo zitalinda misingi ya mfumo wa elimu. (Makofi)

Mhehimiwa Spika, hapa napenda kutoa mifano michache ili muweze kunielewa. Mwaka 1997 aliamka mtu akafuta UMITASHUMTA, lakini tunashukuru Serikali ilirudisha UMITASHUMTA mashuleni na sasa hivi inafanyika katika utaratibu mzuri tu. Hii ilikuwa hatari sana kwa sababu wote tunajua michezo namna ilivyo multibillion industry duniani.

Mheshimiwa Spika, nitatoa mfano wa pili. Kuna kipindi pia kuna mtu aliamka akaamua akataka kuunganisha Chemistry na Physical; yaani kipindi kile somo hili lilitakiwa liitwe Physics with Chemistry. Tunashukuru mambo haya hayakuweza kufanyika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nitatoa mfano wa tatu, mwaka 2014, Kidato cha Nne waliwekewa alama zao za ufaulu kwa kutumia wastani wa point ama kwa lugha nyingine GPA. Vijana waliomaliza 2014 na 2015 waliwekewa kwa mfumo huu na sababu zilizotolewa kipindi kile, ni ili tuwe na system inayofanana. Mwaka 2016 tukarudisha mfumo ambao tumeuzoea wa division. Kwa hiyo, tuna wanafunzi katika nchi hii ambao kuna kipindi waliwekewa marks zao kwa mfumo wa GPA, baadaye ikabadilishwa ikarudisha division. Nasema haya ili mnielewe ni kwa nini inatupasa kulinda mfumo wetu wa elimu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mfano mwingine, Serikali iliwahi kugharamika kupeleka walimu nje waweze kujifunza programme za re-entry, kuwasaidia watoto wa kike wanaopata ujauzito waweze kuwa accommodated tena katika mfumo wa elimu. Zoezi hili lilikuwa frustrated kwa sababu lilikuwa halilindwi. Baadaye ikaonekana halina mantiki, likawekwa kwenye kapu, lakini tayari tuligharimika kuwasomesha walimu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mfano mwingine, ilitokea programme ya voda fasta ya walimu kusomeshwa miezi mitatu. Walimu walisomeshwa na wakapelekwa kufundisha watoto wetu na kuambiwa kwamba wana-qualify. Miezi hii, mitatu! Naeleza haya ili kuonesha ni kwa nini tulinde mfumo wetu wa elimu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, leo hii mtoto wa miaka mitatu yuko boarding school. Mtoto wa miaka mitatu mama yake au baba yake amempeleka boarding school. Naeleza haya ili tuweze kuona hatari hizi na kuona umuhimu wa kulinda mfumo wetu wa elimu.

Mheshimiwa Spika, la mwisho ambalo ningependa sasa nilieleze hapa, leo hii kuna vijana katika nchi hii walisoma miaka mitatu chuo, walivyomaliza wakaambiwa vyeti vyao havitambuliki. Inawezekana sisi tukawa tumesahau, lakini wale vijana hawajasahau, wamelibeba hili kwenye mabega yao na kwa machozi zaidi ya miaka saba sasa wanatembea nalo bila kupata msaada. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kama mnakumbuka, Chuo kilikuwa kinaitwa Chuo cha Kilimo Mbeya (Mbeya Polytechnic College) kati ya mwaka 2013 mpaka 2016. Chuo hiki kilipewa usajili na NACTE, vijana walisajiliwa na kudahiliwa na walisoma pale miaka mitatu. Baada ya kusoma miaka mitatu, vijana hawa wakaambiwa vyeti vyao havitambuliki. NACTE wakasema Chuo chenu kilikuwa hakilipi ada za usajili. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Mheshimiwa Jidith, muda hauko upande wako.

MHE. JUDITH S. KAPINGA: Mheshimiwa Spika, ahsante, naunga mkono hoja. (Makofi)