Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

Hon. Nusrat Shaaban Hanje

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

MHE. NUSRAT S. HANJE: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi nami nichangie katika Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia na nitaomba niseme yafuatayo kwanza. Wanafunzi wanaweza kuwa 20% tu ya population yetu. Yaani students may be 20% of our population, but they are 100% of our future. Kwa sasa tunaweza tukaona wanafunzi kama sehemu tu, kwa sababu ni sehemu ndogo ya jamii yetu, lakini kwa maisha yetu yajayo, wanafunzi ndio watakuwa sisi, yaani watakuwa 100% ya population yetu. Maana yake kuna umuhimu mkubwa sana wa kuwekeza nguvu zetu na uwezo wetu wote kwenye mfumo wetu wa elimu Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Sera ya Elimu ya mwaka 2014 dhima yake ni kuwa na Mtanzania mwenye maarifa, ustadi, umahiri, uwezo, na mtazamo chanya katika kuchangia maendeleo ya Taifa. Sasa katika mambo haya ambayo tunasema ndiyo dhima ya elimu katika Sera ya Elimu ya mwaka 2014, hatuwezi kuyazungumza haya bila kutaja ubora na kuboresha mfumo wetu wa elimu.

Mheshimiwa Spika, nitazungumza kidogo kuhusu udhibiti ubora. Ripoti ya CAG inaonyesha kwamba kumekuwa na upungufu mkubwa sana wa udhibiti ubora kwa 8%, baadhi walishazungumza. Tumepeleka wadhibiti ubora 98 kati ya 1,306 ambayo ilikuwa ndiyo kusudio. Sasa kwa kutekeleza hili, maana yake hawa ndio wanaoenda kuangalia ubora wa elimu yetu. Sasa tumetekeleza kwa 6% tu, ni jambo ambalo linavunja moyo kiasi kubwa. Kwa hiyo, hata kama kuna mambo makubwa tunayapanga, lakini katika ufuatiliaji, tunawategemea watu ambao ni wadhibiti ubora kwa ajili ya kwenda kuangalia utekelezaji.

Mheshimiwa Spika, hili siyo jambo la kihisani, ni suala ambalo liko kisheria. Katika Sheria ya Vyuo Vikuu ya Mwaka 2005 kifungu cha 27 inaeleza hayo, lakini pia katika Sheria ya Baraza la Elimu ya Ufundi ya Taifa (NACTE) ya Mwaka 1997 Kifungu (5) na (1) kinavitaka Vyuo Vikuu na Vyuo vya Ufundi kuwa na utaratibu na kujiwekea miongozo ya kudhibiti ubora ili kuhakikisha kwamba elimu yetu inayotolewa Tanzania kweli iaakisi 100% ya population yetu ya Taifa in the future, ambayo future hatuzungumzi miaka 3,000 ijayo.

Mheshimiwa Spika, hawa hawa wanafunzi baadaye watakuja kuwa Mawaziri na watakuja kuwa watendaji. Sasa ubora wa elimu yetu tunategemea hawa watu wakadhibiti, lakini tumeweza kwa 8% tu jinsi ambavyo hatuweki nguvu katika udhibiti ubora. Ni jambo ambalo linasikitisha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nataka nizungumze kidogo kuhusiana na mtaala. Kwanza ni-declare interest, mimi ni mwalimu professionally. Nimeona wivu kidogo, kuna wenzangu wameanza kuchangia wameitwa Walimu; kwa hiyo, kwenye record yako naomba iingie kwamba nami pia ni Mwalimu. (Makofi)

SPIKA: Mwalimu Nusrat Hanje. Nashukuru tumefahamu sasa. (Kicheko/Makofi)

MHE. NUSRAT S. HANJE: Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwanza elimu yetu ina tatizo kubwa sana. Kimsingi ninakusudia kuleta maelezo binafsi kwenye Bunge hili kushauri kama miongoni mwa watunga sheria kwenye Bunge hili Tukufu namna ambavyo elimu yetu inaweza kusaidia vijana wetu na hasa ambao tunategemea watakua 100% of our future. Elimu yetu inakosa mambo matatu ya msingi. Inakosa kitu kinaitwa Person Development. Juzi Ijumaa niliuliza swali kwenye Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia kuhusiana na kufanya topic ya life skills kuwa somo kuanzia Darasa la Tano mpaka Form Four na tutaangalia Form Five na Six tuone namna bora ya kujenga uwezo wa kibinadamu, uwezo na utashi wa kimtu, kwa sababu ndiyo dhima ya Sera ya Elimu ya Mwaka 2014, ambayo inataka kujenga Mtanzania mwenye maarifa, ustadi, umahiri na uwezo na mtazamo chanya katika kuchangia maendeleo ya Taifa. Sasa tunakosa kitu kinaitwa personal development. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ushawahi kutoa tafakuri tunduizi hapo hapo kwenye kiti chako kwamba unashangaa kwamba Watanzania hatuna uaminifu? Kwa nini mtu anaaminiwa afanye kitu na anashindwa ku-perform kama ambavyo aliyemwamini amempa wajibu huo? Hilo siyo katika biashara tu, kuna vitu vingi ambavyo Watanzania; vijana wanaotoka vyuoni wanashindwa ku-perform.

Mheshimiwa Spika, leo watu kama Marehemu Ruge, kwa kweli tunatambua mchango wake mkubwa kwenye Taifa hili, anaonekana ni genius. Everybody is genius, but if you judge a fish by its ability to climb a tree it will live its whole life believing it is stupid. Yaani kila mtu ana akili, lakini kama tutamhukumu samaki kwe uwezo wake wa kupanda mti, hataweza kushindana na nyani. Nyani ana uwezo wa kupanda mti kuliko Samaki. Samaki anaweza kuogelea. Kwa hiyo, samaki ana uwezo wa kuogelea, kwa hiyo, anatakiwa apelekwe baharini na nyani apelekwe kwenye miti kwa sababu ndiyo ana uwezo huko. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa mfumo wetu wa elimu unawafanya watu baadhi wenye mawazo mbadala kwa sababu ya kujipa maarifa kwingine waonekane wana uwezo mkubwa. Tumeshasema, ili ulime kilimo cha biashara, ni lazima uanzie sokoni, ukajue soko linahitaji nini ndiyo ukalime. Huwezi kulima ndiyo ukatafute soko. Sasa mtu akizungumza hivi, anaonekana ni genius, lakini ni suala ambalo tunatakiwa tu-train vijana wetu kwenye Taifa, kwenye personal development; uwezo wa kuthubutu. Tuna tatizo la kubwa la uthubutu. Watu hawawezi kuthubutu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo la pili, nitaleta maelezo binafsi kuelezea kwa nini tunasema vitu vitatu vinakosekana katika elimu yetu? Jambo la pili ambalo linakosekana ni kitu kinaitwa financial literacy. Sisi walimu tunafundisha shuleni financial knowledge, ndiyo tunafundisha accounts, yaani mtu anafundishwa kufugua makabati; anatakiwa akajibu mtihani ili aonekane ana akili, afaulu aende darasa la mbele. Leo ninyi hapa Bungeni tulivyoapishwa tu, tuliletewa wataalamu wa fedha waje kutushauri how much do we spend? How much do we invest? How much do we save? How should we donate? Spirit ya donation watoto wanatakiwa wafundishwe kwenye nchi hii. Tunatakiwa tuanze ku-train vijana wetu wakiwa mashuleni financial literacy, siyo financial knowledge. Financial Knowledge inamfanya akajibu mitihani afaulu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala la tatu, ambayo elimu yetu haitupatii, ni kitu kinaitwa Career Development, amezungumza Mheshimiwa Mpina, ambayo inamfanya kijana aliyepo shuleni ajue, akutane na watu ambao wanafanya kitu ambacho anatamani kukifanya. Siyo mimi nina kipaji cha kucheza mpira, lakini kwa sababu sijawa trained vizuri, mimi role model wangu anakuwa mwanasiasa, come on! Yaani tunatakiwa tuwa-connect vijana wetu na watu ambao wana- inspire kwenye maisha, tangu wakiwa shuleni. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, vitu tatu vya msingi, kama kuna mwalimu humu katika walimu uliowataja au wataalamu ma-professor ataniambia hivi vitu vinapatikana kwenye mfumo wetu wa elimu, basi nitakuwa nimekosea, lakini kwa sababu ninajua hivi vitu tunavisoma tukitoka; kuna watu wanaitwa motivational speakers mnawajua, ndiyo vitu wanavyovizungumza, ni hivi hivi kwa sababu wanajua mfumo wetu wa elimu hauwapi hivi vitu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mfumo wetu wa elimu upo Paper Oriented. Duniani model ya elimu bora kabisa duniani, the best education system in the world ni ya Finland. Kuna watu wanazungumza kuhusu China; kwenye uchumi, sawa ni China kwa sababu tunaona performance outcome yake, lakini the best education system in the world ni ya Finland. Wameweza kufanikiwa kwa sababu watoto hawafanyi mitihani. Standardized testing; kuna watu wamefeli Form Four, lakini leo ndiyo billionaires. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna waliofaulu sana tunawajua sana ma-professor wapo hapa, tunakutana nao huko na nini, tunashukuru, tunawapongeza kwamba mmesoma na nini, lakini tunawajengea watoto wetu uelewa mbaya kuhusiana na nikifeli, maana yake sina uwezo. Yaani mfumo wa elimu unanilazimisha mimi hata kwa cram, hata kwa kuibia, ndiyo maana tuna watoto wanamaliza Darasa la Saba hajui kusoma na kuandika na utashangaa amefanya mtihani kafaulu. Vipi? Kumbe kuna watu wana vipaji vya kupiga chabo. Mnajuwa chabo!

Mheshimiwa Spika, Chuo Kikuu tulikuwa tunasema kudesa. Kuna watu wana uwezo wa kudesa, anafaulu, lakini hana uwezo. Yaani the output, material ambayo inatoka chuoni haiwezi kuwa challenged kwa sababu iko very low. Yaani ile output ya kutoka vyuoni bado kuna shida kwa sababu tupo Paper Oriented.

Mheshimiwa Spika, bado kuna tatizo kubwa sana la…

MHE. SAASHISHA E. MAFUWE: Mheshimiwa Spika, taarifa.

SPIKA: Mwenye taarifa endelea, Mheshimiwa Saashisha.

T A A R I F A

MHE. SAASHISHA E. MAFUWE: Mheshimiwa Spika, kwanza nataka nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge anavyochangia madini ya kutosha hapo, lakini nilitaka nimpe taarifa tu kwenye eneo aliosema la career development kwamba kwenye hoja yake sasa ni vizuri career development ikaingizwa kwenye kozi za ile tunasema ni seven, four, two, three plus. Ile mwaka wa mwisho, career development ifundishwe hapo.

Mheshimiwa Spika, kwa sababu msemaji anayeendelea kuzungumza, kama hayatafundishwa, wanafunzi wanafika chuoni ndiyo wanaanza kujadiliana, anayemaliza Form Six, wewe unataka kwenda kusoma nini? Mwanasheria; au mwingine baba yake kwa sababu alifanya vizuri kwenye Hesabu, anamwambia kasome Hesabu, lakini kuna kitu kinaitwa core curriculum. Kama haya mambo yote yakiunganishwa na hii career development, hata watoto wanapomaliza kwenye ile seven ya mwisho, wafundishwe kwamba wewe kwa namna ulivyo, tunavyokuona, tunadhani uende hivi na utashi ulionao kwa kuzingatia mawazo ya watoto.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nilitaka nimwongeze tu kwamba career development ni sehemu muhimu sana ya kubadilisha na ku-transform mindset za wasomi wa nchi hii. Ahsante. (Makofi)

SPIKA: Mheshimiwa Nusrat, unapokea ushauri huo?

MHE. NUSRAT S. HANJE: Mheshimiwa Spika, napokea. Kimsingi nampongeza pia aliyezungumza. Pia, nampongeza Mheshimiwa Waziri kwa sababu wakati nauliza swali alisimama mwenyewe akasema kwamba atafungua mjadala kwa ajili ya wadau kutoa maoni yao. Nafikiri hayo pia ni sehemu ya maoni ambayo tutayatoa. Kwa hiyo, naipokea. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba nimalizie katika eneo moja. Wakati tunarekebisha mitaala yetu tukumbuke kwamba kuna wale vijana ambao wanamaliza shule ya msingi wanashindwa kuendelea na Sekondari na kuna wale wanaomaliza form four wanashindwa kuendelea na elimu ya juu zaidi; wale kwenye mtaala wetu tuwawekee utaratibu ambao katika stadi za kazi wanazosoma shule wakafundishwe vitu kutokana na uchumi wa maeneo yao husika.

Mheshimiwa Spika, mathalani, maeneo ambayo kuna migodi… (Makofi)

(Hapa sauti ya Mhe.Nusrat S. Hanje ilikauka)

SPIKA: Pole sana Mwalimu. Hakuna maji karibu hapo! (Kicheko)

MBUNGE FULANI: Amefunga.

SPIKA: Amefunga loh! Pole sana. (Kicheko)

MHE. NUSRAT S. HANJE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba nimalizie taratibu taratibu. Maeneo ambayo labda kuna migodi, maziwa na mito ambapo tunategemea watu wa pale wengi ni wavuvi...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Naambiwa ya pili tayari. Basi sentensi moja tu.

MHE. NUSRAT S. HANJE: Mheshimiwa Spika, basi tunategemea pia wale wananchi na wanafunzi wanaopewa elimu katika maeneo husika, basi wakafundishwe kwa sababu wengi wakimaliza wanashindwa kuendelea na vyuo, wanarudi mtaani, halafu wanaanza kujifunza upya kuhusu kilimo, kuhusu uvuvi, kuhusu uchumi unaopatikana kwenye hilo eneo. Kwa hiyo, stadi za kazi zikafundishwe kutokana na uchumi wa eneo husika ili wale vijana wanaoshindwa kuendelea na vyuo waende kufanya shughuli za uzalishaji mali katika maeneo husika. Ahsante sana. (Makofi)