Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

Hon. Dr. Paulina Daniel Nahato

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

MHE. DKT. PAULINA D. NAHATO: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia katika Wizara hii ya Elimu.

Mheshimiwa Spika, awali ya yote, napenda sana kumpongeza Profesa Ndalichako, mwalimu wangu ambaye najivunia sana kumuona akiwa kwenye kiti hicho, anatosheleza. Ni mwalimu mahiri na yupo vizuri sana. Kwa hiyo, hapo alipo pamoja na Naibu Waziri wametosheleza kwa jinsi ninavyomfahamu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia nampongeza sana kwa kuwakilisha taarifa yake nzuri sana. Nami ni mwalimu kwa hiyo mambo yote ambayo kwa kweli kama mwalimu nilikuwa nategemea yasemwe, nimeyasikia. Kwa hilo nimeburudika sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia napenda kukushukuru sana wewe na kwa sababu muda ni mdogo naomba niende moja kwa moja kwenye uchangiaji. Kwa kuwa na shule ya wasichana ya Bunge, Kamati tumefika kuiona, ile shule ni nzuri sana na ni ya sayansi tunategemea kupata madaktari na engineers. Tuliwaona wamekuja hapa Bungeni, wanang’aa kwa hiyo tuna uhakika baada ya muda fulani tutakuwa na kada ya watalaamu wanawake wa kutosha. Hiyo ni sifa kubwa sana kwa wanawake, kwa hiyo, hongera sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wanawake tuliosoma miaka ya nyuma masomo ya sayansi yalikuwa si ya wanawake. Mwanamke akisoma masomo ya sayansi alikuwa anaonekana kama yupo tofauti na hii ilikuwa ni mtizimano fulani ambao ulikuwa umejengeka hata wanawake wenyewe tulikuwa tunaona hivyo. Juzi Rais wetu alipokuwa anahutubia alisema moja kwa moja kwamba akili ya mwanamke na mwanaume zipo sawa tofauti yetu ni masuala ya biolojia tu kwamba mwanamke anabeba mimba na anazaa mtoto na mwanaume ana mbegu ya kuweka mimba kwa mwanamke, hiyo ndiyo tofauti. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, masuala mengine yote tupo sawa kabisa kuanzia kwenye akili, kwenye matendo, hamna kazi ambayo mwanaume anafanya mwanamke hawezi kufanya, hakuna. Ni utamaduni uliojengeka tu, is a socially constructed idea. Kwa hiyo, tunapoona wanawake wanasoma sayansi hao ndiyo tunaotegemea wawe ma-engineer, watengeneze caterpillars, viwanda watakuwa wanawake wakipanda juu na kutengeneza mashine. Nataka kusema nini hapa? Nataka shule za wasichana ziongezwe hasa katika michepuo ya sayansi ili kuwe na ile notion ya zamani ambayo wengine tuliikosa katika masomo ya sayansi sasa tunapoenda kwenye fifty fifty wanaume kwa wanawake pia kwenye masuala ya sayansi tuwepo.

Mheshimiwa Spika, nini sasa tufanye ili tuweze kufikia pale? Kwa tafiti ambazo zimefanyika zinaonyesha kwamba wasichana wanapokuwa wenyewe katika shule zao, wanaposhindana wenyewe wanafanya vizuri sana. Mtakubaliana na mimi tunapoangalia zile shule ambazo zimefanya vizuri, japokuwa zipo pia na za wanaume wenyewe kwa wenyewe lakini za wanawake zinaoongoza ni zile ambazo wanawake wako wenyewe.

Mheshimiwa Spika, sijajua sababu ni kitu gani lakini mojawapo ni kwamba wanawake wanapokuwa wenyewe wanakuwa na ile hali ya kujiamini zaidi kwa sababu yale mambo ya kuona aibu na maneno maneno ambayo yalikuwa siku za nyuma yanakuwa hakuna. Kwa hiyo, wanaposhindana wenyewe kwa wenyewe kunakuwa na kujiamini.

Mheshimiwa Spika, mimi nafikiria siku zijazo angalau tufike hata kila wilaya kuwa na shule za bweni za wasichana ambazo zitakidhi mahitaji ya wasichana. Hata masuala aliyoongea Mheshimiwa mambo ya taulo za kike, ile sisi tumejisikia vibaya lakini ndiyo ukweli ila kwa vile ameongea mwanaume tukajisikia vibaya, tuondoke tu ni mwanaume kasema ni sawa.

Mheshimiwa Spika, kwa kusema hivyo Mheshimiwa Waziri nafikiri baadaye tutawaza kuona kwamba kila wilaya inakuwa na shule ya wasichana na itiliwe mkazo masomo ya sayansi. Ili chuo kikuu basi zile faculty zote za sayansi tuone wanaume na wanawake ili baadaye wanapoingia katika soko la viwanda wanawake wawepo wengi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, naomba sasa nizungumzie suala moja la mfumo wa mikopo. Suala hili tunaishukuru Serikali kwamba sasa hivi angalau imeongeza pesa. Takwimu inaonyesha kwamba itakapofika 2525 wanafunzi watakaokuwa wanaingia shuleni ni mara mbili. Hii ina maana kwamba form four, form six na chuo kikuu wataongezeka mara mbili, tumejiandaaje? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mfumo wa mikopo uliopo sasa hivi una changamoto, haupo sawa. Kuna wanafunzi ambao wanakosa mikopo, hawa wanaotoa mikopo kuna masharti ambayo wanasema ni lazima huyu kijana anayepata mkopo awe yatima, wazazi wake waonyeshe hawana uwezo na vitu kama hivyo. Sasa utawezaje kupima kwamba huyu kijana ni maskini hiyo ni kazi kubwa sana. Matokeo yake nini? Wanafunzi wanaingia chuo kikuu wanakosa mikopo na mbaya zaidi hawa wanaokosa mikopo ni wale ambao kabisa kwa ukweli ni maskini na hivyo wanashindwa kumaliza masomo yao. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Ahsante Mheshimiwa Paulina Nahato.

MHE. DKT. PAULINA D. NAHATO: Mheshimiwa Spika, ahsante na naunga mkono hoja. (Makofi)