Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

Hon. Hussein Nassor Amar

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nyang'hwale

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi hii niweze kuchangia. Kwanza, nianze kumshukuru Mwenyezi Mungu ambaye ameniwezesha mimi pamoja na sisi sote humu ndani kuwa na afya njema. Pia, nimpongeze Waziri na Naibu Waziri pamoja na Watendaji wa Wizara kwa hotuba yao nzuri sana.

Pia, niipongeze Serikali ya Awamu ya Tano kwa kutoa elimu bure kwa wanafunzi wa shule za msingi pamoja na sekondari kwa nchi nzima, ikiwemo Wilaya ya Nyang’hwale ambayo imeweza kupokea fedha hizo zaidi ya bilioni tatu. Naipongeza sana Serikali. Pia, kuna changamoto mbalimbali nyingi, lakini nitazungumza chache.

SPIKA: Mheshimiwa Amar.

MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Spika, naam.

SPIKA: Wenyewe wanaiita Elimu Bila Malipo kama sikosei, lakini siyo Elimu Bure. Watanisahihisha baadaye. Wanasema kuna tofauti kati ya vitu hivyo viwili.

MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Spika, ahsante. Nirekebishe kauli, Elimu Bila Malipo.

Mheshimiwa Spika, pia Serikali imeweza kutuletea fedha zaidi ya shilingi bilioni tatu kwa ajili ya Elimu Bila Malipo upande wa shule za msingi pamoja na sekondari. Kuna changamoto nyingi kwenye upande wa elimu lakini nitazungumza chache, hususan kwenye upande wa Wilaya yetu ya Nyang’hwale.

Mheshimiwa Spika, naamini kabisa kwamba upungufu wa vyumba vya madarasa kwa nchi nzima upo, lakini nitazungumzia kwa upande wa Wilaya yetu ya Nyang’hwale. Tuna upungufu sana katika shule za msingi, mahitaji ya madarasa ni kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, tunahitaji madarasa 1,138, lakini yaliyopo ni 616, upungufu ni madarasa 522. Kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Waziri hili alichukue, lakini nitakuwa na ushauri huko mbele. Pia, tuna upungufu wa madarasa kwenye shule zetu za sekondari zaidi ya vyumba 30, lakini pia tuna upungufu wa Walimu. Upande wa shule za msingi tuna upungufu wa Walimu 342 na upande wa sekondari tuna upungufu wa Walimu 180.

Mheshimiwa Spika, naomba kutoa ushauri kwa Mheshimiwa Waziri kwamba tumekuwa tukiandaa vijana wetu na wanapomaliza masomo ama kutokuendelea na masomo wanarudi mtaani. Mfano, vijana wetu wanaoshindwa kuendelea na elimu ya juu, wanarudi mitaani wanakuwa hawana kazi. Naomba kushauri kwamba Wilaya ya Nyanghwale tuweke utaratibu mzuri hapo mwakani Wizara iingize ndani ya bajeti iweze kutujengea Chuo cha Ufundi Stadi ili wale wanafunzi wanaoshindwa kuendelea na elimu ya juu, basi waweze kujifunza ufundi ili waweze kujiajiri wenyewe.

Mheshimiwa Spika, nataka nifikishe pia kilio cha Walimu wetu wastaafu. Kuna Walimu wastaafu wapatao 20, leo wana zaidi ya miaka sita wanadai mafao yao na wameshakuja hapa Dodoma nimewapeleka kwenye ofisi husika zaidi ya mara nne, wamehakikiwa.

SPIKA: Mheshimiwa rudia hiyo point yako, Waziri wa Nchi alikuwa hakusikilizi.

MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Spika, kuna Walimu wastaafu zaidi ya 20, wakidai mafao yao zaidi ya miaka sita. Wamekuja hapa Dodoma nimewafikisha sehemu husika zaidi ya mara tatu, wanaambiwa tumeshahakiki subirini malipo yenu. Mpaka leo hii wamenipigia simu wanasema Mheshimiwa hatujalipwa mafao yetu na wengine ni wagonjwa, hali zao si nzuri. Naomba nilifikishe hilo kwa Mheshimiwa Waziri.

Mheshimiwa Spika, mwisho, naomba kutoa ushauri kama walivyoshauri wenzangu kuhusu wanafunzi wetu wanaotoka majumbani saa 12, wanarudi jioni wakiwa hawajanywa chai, hawajala chakula, naomba uwekwe utaratibu ulio mzuri ili wanafunzi wetu waweze kupata chakula. Kipindi cha nyuma kulikuwa na utaratibu huo wa kutoa chakula kwenye shule zetu, lakini pakawa na upotevu wa chakula ambacho kilikuwa kikilimwa na wale wanafunzi. Tujaribu kuweka utaratibu mzuri, Bodi ya Shule iwashirikishe wazazi pindi watakapokuwa wanalima wanafunzi chakula chao, wazazi na wenyewe washughulike kuhakikisha kile chakula kinatumia ipasavyo; ili wale wanafunzi wapate chakula. Nitatoa mfano, kuna vijana wa sekondari wanatoka eneo moja kwenda eneo lingine maili saba kwenda kusoma kuanzia saa 12 mpaka jioni, wanarudi wakiwa hawajala chakula. Nadhani hawatakuwa na mafanikio mazuri kuhusu elimu yao, ndio maana tunatengeneza vijana wengi ambao wanashindwa kuendelea na masomo yao.

Mheshimiwa Spika, sina mambo mengi ni hayo tu machache ya ushauri, lakini naomba suala la Walimu wangu wastaafu lichukuliwe kwa umakini, walipwe haraka fedha zao kwa sababu leo ni miaka sita wanafuatilia mafao yao.

Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi hii. (Makofi)