Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hotuba ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa Kufungua Bunge la Kumi na Moja

Hon. Prof. Jumanne Abdallah Maghembe

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mwanga

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hotuba ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa Kufungua Bunge la Kumi na Moja

WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii na ninapenda kwanza nimpongeze Mheshimiwa Rais wetu Dkt. John Pombe Magufuli kwa hotuba nzuri iliyotoa malengo thabiti ambayo yamenukuliwa duniani kote kama hotuba ya mfano. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru Mheshimiwa Rais kwa kuniamini na kunipa dhamana ya kuiongoza Sekta ya Maliasili na Utalii. Wasemaji wengi wameeleza changamoto zilizopo katika sekta hii, lakini kwanza nilikuwa nataka niwahakikishie ndugu zangu kwamba Sekta ya Maliasili ukiondoa misitu inachangia uchumi wetu kwa asilimia 17, lakini ukiongeza misitu mchango wake unafika asilimia 23 ya uchumi wetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mchango huo, sekta hii ndiyo ya kwanza kutupatia fedha za kigeni kwa kuchangia asilimia 25 ya fedha zote za kigeni.
Pamoja na mchango huu, sekta hii ndiyo inahakikisha tunapata maji, inahakikisha mvua zinakuwa za kuaminika, inahakikisha tunapata watalii wengi sana kutoka maeneo yote duniani. Sekta hii pamoja na changamoto zilizopo, ina ubora katika nchi yetu kuliko nchi zote za Kiafrika, na ni ya pili duniani kote ukiacha Brazil kwa ubora dunia nzima. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu hiyo ni muhimu tupambane sana na changamoto ambazo zinaikabili; ya kwanza ikiwa ujangili. Hili tunapambana nalo kwa kuwafanyia utafiti majangili. Hivi sasa wamebadilisha sana njia zao za kuwaua wanyama ambao wanawahitaji katika mapori yetu. Tembo wanauawa kwa kupewa sumu na wanyama wengine wanapewa sumu tena kwa aina ambayo kwa kweli ni ya kusikitisha sana. Na sisi tunabadilisha mwendo wetu wa kushughulika nao.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hivi tunafanya majaribio ya ndege ambazo hazina marubani, kwanza kuhakikisha kwamba zinaondoa migogoro kati ya wananchi wenye mashamba na mapori ya akiba na mapori tengefu, lakini pia kuhakikisha kwamba tunaona shughuli za binadamu pamoja na majangili katika maeneo ambayo yana maliasili.
Mheshimiwa Naibu Spika, tumechukua hatua pia ya kuongeza wafanyakazi ambao wanashughulikia ulinzi wa wanyamapori kutoka askari 1,506 mwaka 2014 na sasa wamefikia askari 2,064. Aidha, tumeongeza vitendea kazi kwa sehemu kubwa sana na tumelitengeneza Shirika la Tower ambalo kazi yake itakuwa kulinda maliasili zetu kwa karibu zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo ni kubwa sana na Waheshimiwa Wabunge mmelisema kwa uchungu mkubwa ni uharibifu unaofanywa na wanyamapori katika mashamba na katika maeneo tunakoishi. Tutashirikiana na Wizara ya Ardhi, Wizara ya Mazingira na Wizara ya Kilimo na Mifugo ili kuhakikisha kwamba migogoro hii inaondoka mapema iwezekanavyo. (Makofi)
Aidha, tunachukua hatua mbalimbali za kuhakikisha kwamba mapato yetu kutoka kwenye maliasili zetu yanaongezeka. Kuacha sasa, wizi ule mdogo mdogo unaotendeka ndani, malengo yetu ni kuongeza watalii kutoka 1,100,000 hivi sasa na kufika 3,000,000 mwisho wa mwaka 2018 tukilenga kwamba utalii sasa utupatie asilimia 40 ya mapato yote ya Taifa letu. Ndugu zangu naomba tulinde maliasili zetu. Ahsanteni sana. (Makofi)