Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. KABULA E. SHITOBELA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi hii niweze kuchangia katika Wizara ya Elimu. Kwanza kabisa napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa afya njema hata uhai pia. Napenda kumpongeza Rais wetu mpendwa Mama yetu Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri anazoendelea kuzifanya. Niende moja kwa moja kuchangia hoja hii ya Wizara ya Elimu. Tatizo la ajira katika nchi yetu limekuwa tatizo kubwa sana, kusababisha matatizo mengi kwenye familia hasa kwa kina mama. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mfano, wakinamama wengi wanalea watoto kupitia biashara ndogo ndogo kama mama lishe na kutembeza hata vitu vidogo vidogo, kwa ajili ya kujipatia pesa kwa ajili ya kutunza watoto wao na vile vile kuwapeleka shule. Mama huyu wakati anampeleka mtoto shule anakuwa na imani kwamba, baada ya kuhitimu masomo mtoto yule ataweza kuwa mkombozi wake. Lakini, badala yake mtoto yule anapohitimu masomo anajikuta anaongeza mzigo tena kwa mama yule, anaanza tena kutembea kila siku na vyeti kwenda kutafuta kazi akitumia nauli ya mama yake, anaomba kila siku kwa mama nauli. Kwa hiyo, inazidi kumuongezea shida mama huyu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, na ukizingatia mama huyu anakuwa amekopa mikopo kwenye SACCOS na sehemu mbalimbali kama VICOBA, ili aongezee ule mtaji wake na kuweza kupata school fees ya mtoto wake.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nilikuwa naiomba Wizara ya Elimu ijaribu kuangalia mitaala yake lakini pia, iwajengee watoto confidence kuanzia utotoni kwamba, haendi kusoma kwa ajili ya kufanya kazi au kuajiriwa. Wawajenge kisaikolojia kwamba, anaenda shule kutoa ujinga au kuongeza elimu ya vitu mbalimbali. Lakini nia yake ni kupata biashara, akifanya biashara anauwezo wa kutengeneza maisha yake au kutengeneza faida kubwa kuliko hata huo mshahara ambao angeenda kulipwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, niiombe sana Wizara ya Elimu ijaribu kuliangalia hilo, ili kuwajengea uwezo watoto wetu wa kujitegemea kuliko kutegemea ajira. Mfano, tukiangalia matajiri wengi duniani ni wale ambao hawakusoma sana je, tumejaribu kujiuliza ni kwa nini wale ambao hawakusoma sana wameweza kufanikiwa sana katika biashara au katika kujitegemea? Jibu ni kwamba, waliona hawana option nyingine hawakusoma hawana vyeti vizuri vya kuweza kuajiriwa katika nyadhifa nzuri. Kwa hiyo, ndio maana wakasimamia zile biashara zao au kazi yao, kama walikuwa wakilima walilima vizuri na kuhakikisha mazao yale yametoka kwa wingi na kuweza kuuza kupata pesa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nizidi kuiomba Wizara ya Elimu isimame vizuri kuangalia hiyo mitaala hata kama ni mtoto anakwenda kusoma kama anasomea kilimo, akitoka pale akaweze kulima na kuangalia ni nini kitakachoweza kumpatia manufaa?
Mheshimiwa Naibu Spika, huo ndio mchango wangu, naomba kuwasilisha. (Makofi)