Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Busokelo
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa fursa ili niweze kuchangia kwenye Wizara hii ya Elimu.
Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote, nimshukuru sana Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehma ambaye ametufanya tuwepo katika Bunge lako hili Tukufu. Pili, nimpongeze sana Waziri wa Elimu, Mheshimiwa Prof. Joyce Ndalichako kwa kuiongoza vizuri Wizara hii ya Elimu pamoja na Naibu wake na watendaji wote. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kipekee kabisa, nimshukuru Mheshimiwa Waziri na Serikali yote ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa namna ambavyo wameweza kulitendea haki Jimbo la Busokelo. Busokelo mengi yamefanyika kupitia Wizara ya Mheshimiwa Prof. Ndalichako hususan ujenzi wa shule mbalimbali.
Mheshimiwa Naibu Spika, hivi ninavyozungumza katika Mkoa wa Mbeya mojawapo ya halmashauri zinazofanya vizuri sana kwenye mitihani ya kidato cha nne Busokelo tumekuwa tukiongoza kwa miaka miwili mfululizo. Hii ni kutokana na msaada mliotupatia kama wa ujenzi wa shule za wasichana na za watoto wa kiume. Kwa mfano, Busokelo Girls imejengwa na inafanya vizuri na ndiyo inayoongoza, Busokelo Boys imejengwa inafanya vizuri na inaongoza. Kuna shule nyingine zimekarabatiwa kama Ntaba Sekondari, Mwakaleli Sekondari, Ruangwa, Lufilyo, kwa kweli mnastahiki pongezi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, zaidi ya yote mmejenga na Chuo cha VETA ambapo leo hii VETA Busokelo inachukua wanafunzi kutoka mikoa mbalimbali. Niipongeze sana Wizara hii kwa sababu hivi karibuni walitoa agizo kwamba vyuo vyote vya VETA vichukue wanafunzi na ambao siyo wanafunzi waende kusoma katika vyuo vyote nchini. Busokelo tumelitekeleza hilo na hadi sasa wameshajiandikisha zaidi ya wanafunzi 300. Kwa hiyo, nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kama tunavyofahamu na kwenye Vitabu vya Imani mfano Biblia imesema: “Mkamate sana elimu, usimwache aende zake; Mshike, maana yeye ni uzima wako”. Maneno haya ni kutoka Mithali 4:13 ndiyo maana tunang’ang’ana na suala zima la elimu. Mataifa mengi yaliyoendelea yamewekeza sana kwenye sekta ya elimu. Ni- compliment michango ya Waheshimiwa Wabunge kwamba Taifa kama China waliwekeza sana katika ufundi ama vyuo vya kati ndiyo maana leo hii ipo vile ambavyo tunaiona. Hawakuwekeza sana katika vyuo vikuu kwa sababu waliona wafanyakazi wazuri ni wale ambao wamepata elimu ya kati ama vyuo vya kati. Kwa hiyo, naamini pia tunaweza tukajifunza kupitia kwao. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nchi inayoongoza kwa kutoa elimu bora dunia nzima ni Finland. Pia tunaweza tukapeleka wataalam wetu huko wakajifunza kwa nini Finland inaongoza kwa kutoa elimu bora. Ukisoma ripoti mbalimbali za World Economic Forum pamoja na ripoti zingine utaona hiki nachozungumza.
Mheshimiwa Naibu Spika, nishauri yafuatayo katika sekta ya elimu. Tumezungumza suala la mitaala, ni kweli ni changamoto na Mheshimiwa Waziri ametoa commitment hapa kwamba wanakwenda kuibadilisha ama kuihusisha mitaala hii ya elimu. Ikimpendeza Mheshimiwa Waziri anaweza kutuma wataalam wake ama wao wakaja huku wenzetu wa South Africa, wana mfumo ambao nimewahiusema huku Bungeni ambao unawasadia sana vijana wengi ambao wanamaliza vyuo na wengine wakiwa vyuoni kupata kazi baada ya kumaliza masomo yao.
Mheshimiwa Naibu Spika, wao wanatumia mfumo unaitwa Youth Education System (YES). Tafsiri yake hawataishia tu kwamba wakisoma imetoka lakini Serikali inafanya utaratibu mara baada ya kumaliza masomo yao ya vyuo kuwaunganisha na taasisi, mashirika na makampuni mbalimbali yaliyopo katika nchi yao. Sisi pia tukifanya hivyo maana yake wanapotoka kule wanakuwa na ujuzi kamili kwa sababu kwa miaka hii mitatu mwanafunzi akiwa chuoni siyo rahisi sana kupata uzoefu wa kusema anaweza kufanya kazi bali akiunganishwa na taasisi na mashirika ambayo yanafanya kazi tayari itakuwa rahisi sana huyo mwanafunzi kupata ujuzi lakini baadaye kuajiriwa na taasisi hizo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili nataka nizungumzie suala la Bodi ya Mikopo. Nimezungumza hapa mara nyingi na tarehe 31 Machi, 2021 niliuliza swali, je, ni sifa zipi za mwanafunzi ambaye anastahili kupata mikopo? Mheshimiwa Naibu Waziri alieleza lakini ukweli Bodi ya Mikopo kuna haja ya msingi ya kufanya either transformation ama kubadilisha kanuni zinginezo ili wanafunzi wote wenye sifa wapate mikopo siyo kama ilivyo sasa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi ni miongoni mwa Wabunge ambao nimewapeleka wanafunzi wangu zaidi ya 20, zaidi ya mara mbili au mara tatu kwenda Dar es Salaam kuwatafutia mikopo maana wana sifa lakini hawapewi mikopo. Ukikutana na Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Mikopo atakwambia vizuri kabisa lakini utekelezaji wake unakuwa haupo. Nashauri Mheshimiwa Waziri aiangalie vyema hii Bodi ya Mikopo kwamba kuna haja ya msingi ya kubadilisha mifumo inayotumika pale ama kuiboresha zaidi ili wanafunzi wote wenye sifa wapate mikopo hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niungane na Mheshimiwa Mbunge aliyechangia jana mikopo hii isiwe tu kwa vyuo vikuu. Tumezungumza hapa kwamba nguvu kazi kubwa ipo katika vyuo vya kati, kama tutaweza kutoa mikopo hata kwa vyuo vya kati ndiyo tutapata nguvu kazi ya kuzalisha lakini uchumi utaboreka zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo napenda kuzungumzia ni suala zima la upungufu wa walimu katika shule na halmshauri zetu. Busokelo peke yake walimu wa sekondari kuna upungufu wa zaidi ya walimu 93, walimu wa shule za msingi 439 pamoja na matundu ya vyoo zaidi ya 500. Kwa hiyo, tunawaomba Mheshimiwa Waziri utakapokuja ku-wind up hapa aone namna gani anaweza kutusaidia katika jimbo hili la Busokelo.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia tunajenga shule nyingine kwa kushirikiana na wananchi wa Busokelo, kuna shule inaitwa Kifunda Sekondari, Ntaba Sekondari na Ndembo Sekondari. Pia nitumie fursa hii kuwapongeza sana Diaspora wa Busokelo ambao wameendelea kuiwezesha na kuichangia shule yetu ya sekondari inayoitwa Busokelo Girls. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mbali na hayo nataka nimalizie kwa kusema, tukiboresha vyuo vya VETA kwa maana ya vyuo vya ufundi, nina hakika elimu yetu ya Tanzania na ajira hakutakuwa na changamoto kwa kuwa watakuwa wamepata ujuzi hakika na sahihi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, naunga mkongo hoja. (Makofi)