Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

Hon. Abeid Ighondo Ramadhani

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Singida Kaskazini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

MHE. ABEID R. IGHONDO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipatia nafasi angalau na mimi niseme machache kwenye mjadala wa Wizara yetu ya Elimu ambayo ni Wizara muhimu kwelikweli kwa mustakabali wa Taifa letu.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nianze kwa kuipongeza na kuishukuru Serikali; nampongeza sana Rais wetu Samia Suluhu Hassan kwa hatua yake muhimu sana ya kuondoa ile asilimia sita kwenye mikopo ya elimu ya juu. Kitendo hiki ni cha kiungwana na kwa kweli nampongeza sana. Vilevile nimpongeze Waziri wa Elimu kwa kuondoa ile asilimia kumi iliyokuwa inatokana na penati kwa maana ya wanufaika kuchelewesha mkopo ule kwa hiyo naishukuru sana Serikali kwa hatua hii hapa imeonyesha ni kwa kiwango gani inamjali Mtanzania wa chini, yule maskini, kwa sababu mikopo hii lengo lake ni kuwakomboa watoto wa kimaskini wa Kitanzania ambao hawawezi kukopeshwa na mtu yeyote yule isipokuwa Serikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa niombe mikopo hii sasa tupanue wigo tuipeleke kwenye ngazi za chini, kwenye ile elimu ya kati, vyuo vya kati, VETA vyuo vingine vya ufundi tumesha-train graduates sasa naona kwa kiwango fulani, mpaka tumeshindwa kuwaajiri na wenyewe wako mataani kila mahali. Naomba sasa tuelekee na huku kwenye hii elimu ya kati ambao ndio wanaofanya kazi moja kwa moja, tena hawa ukiwapa mkopo leo hii, ndani ya miezi mitatu anakwenda kufanya kazi moja kwa moja, kama ni fundi atapaua, atajenga ukuta, atapata fedha atakuja kurudisha huu mkopo.

Kwa hiyo, naomba sana Serikali iangalie sasa kwenye elimu ya kati nao wanufaike na hii mikopo na ikumbukwe hivi sasa tuna shule hizi za sekondari karibu kila kata. Kwa hiyo sio wote wanaoweza kwenda vyuo vikuu, turudi huku chini huku nao wanufaike na mikopo hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, hapohapo niombe sasa huu mpango wa Vyuo vya VETA, nilishaongea sana na Waziri wa Elimu mara kadhaa, aipe kipaumbele Halmashauri ya Wilaya ya Singida, Jimbo la Singida Kaskazini katika kupata Chuo Cha VETA. Namwomba sana Mheshimiwa Waziri, vijana wana wito mkubwa sana wa kwenda kusoma mafunzo ya ufundi, lakini hakuna chou, vilivyopo ni mbali, havifikiki, kwa hiyo Mheshimiwa Waziri akija hapa niombe commitment yake, aniambie ujenzi wa Chuo cha VETA Singida Kaskazini ni lini utaanza.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna jambo moja hapa naomba nichukue nafasi hii kulisema, kwa sababu tukiendelea kunyamaza tutakuwa hatuitendei haki nchi yetu. Nchi yetu imeweka rasilimali nyingi sana kwenye elimu, vyuo vikuu vya kutosha, vyuo vya kati na shule za sekondari na hata za msingi. Nataka nitoe masikitiko yangu makubwa sana, sisi hapa Bungeni mara kadhaa tumekuwa sasa vinara wa kubeza juhudi hizi na kuonyesha elimu haina umuhimu. Hili jambo kwa kweli, naomba tulichukulie umakini na twende kwa tahadhari.

Mheshimiwa Naibu Spika, statement tunazozitoa sisi Wabunge humu Bungeni hata wakati mwingine utanisamehe, hata kiti, kwamba elimu ya darasa la saba ni ya muhimu kweli kuliko wasomi maprofesa. Hii statement sio nzuri, sio kwamba napuuza darasa la saba, hapana, naheshimu sana mchango wao na naheshimu sana umuhimu wao kwenye nchi yetu, lakini naomba twende kwa tahadhari, tusije tukafika mahali tukapuuza elimu, tukapuuza taaluma, tukapuuza wataalam, tutalidhalilisha Taifa hili. Tutafika mahali tutaangamiza Taifa.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuanzia leo baada ya hotuba hii, tuache kabisa kejeli kwenye taaluma, kwenye elimu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine naomba pia nizungumzie upungufu wa Walimu kwenye shule zetu za misingi na sekondari…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. ABEID R. IGHONDO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nikushukuru kwa nafasi. (Makofi)