Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

Hon. David Ernest Silinde

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tunduma

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, kunipatia fursa hii kuchangia hotuba ya bajeti ya mapato na matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, tumeona tutolee ufafanuzi baadhi ya hoja ambazo Waheshimiwa Wabunge wakati wanachangia hotuba ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia wamejaribu kuzitoa hapa ambazo sisi Ofisi ya Rais, TAMISEMI tunazigusia.

Mheshimiwa Naibu Spika, hoja namba moja ambayo Wabunge wengi walichangia walikuwa wanaiomba Serikali ama kuitaka Serikali kukamilisha maboma ambayo ni nguvu ya wananchi, ambayo yalitokana na nguvu za wananchi huko katika maeneo husika. Na sisi kama ambavyo bajeti yetu ilivyopita, tumetenga fedha kwa ajili ya kukamilisha hayo maboma nchi nzima lakini kwa awamu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano katika mwaka wa fedha 2021/2022, kwenye maboma ya maabara peke yake kwa shule za sekondari tumetenga bilioni 26.07 kwa ajili ya maboma 1,043. Lakini vilevile kwa ajili ya kukarabati na kukamilisha majengo ya shule za msingi tumetenga bilioni 23.154 kwa ajili ya ukamilishaji wa maboma ya shule za msingi 1,852. Na kwa ajili ya sekondari tumetenga bilioni 23 kwa ajili ya maboma 1,840. Kwa hiyo, hiyo ni hatua ya awali kuhakikisha kwamba tunaunga mkono nguvu za wananchi ambazo wamekuwa wakijitolea katika maeneo husika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili, Waheshimiwa Wabunge walijenga hoja hapa wakitaka mkakati wa Serikali wa kukabiliana na ongezeko la wanafunzi wa sekondari wanaotokana na elimu bila ada au elimu bila malipo ambao sasa tunaamini katika mwaka wa keshokutwa, kwa sababu sasa hiivi ukiangalia watoto wa darasa la sita tulionao ambao wanatokana na Sera ya elimu bila ada wako milioni moja na laki nane. Kwa hiyo, watakavyofika mwaka 2022 tutakuwa na watoto ambao wanatakiwa kwenda kidato cha kwanza mwaka 2023, ukifuatilia ili pass rate ya kila mwaka ya zaidi ya asilimia 80, zaidi ya watoto milioni moja na laki mbili wanatakiwa wajiunge na kidato cha kwanza.

Mheshimiwa Naibu Spika, na ndiyo maana kwenye bajeti yetu tumetenga fedha, kwa mwaka huu tutaanza na ujenzi wa shule mpya 300, lakini ndani ya miaka mitatu tutajenga shule 1,000 ambazo zitakuwa na uwezo wa kuchukua wanafunzi 400,000 kwa hiyo, maana yake ukichanganya na idadi ya sasa tutakuwa walau tumeshapunguza hiyo kero ya wanafunzi hao.

Mheshimiwa Naibu Spika, tumezielekeza halmashauri zote nchini kulingana na mapato yao ya ndani kutenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa madarasa. Na tumeweka categories, kwa mfano halmashauri zenye kipato chini ya bilioni 1.5 kujenga madarasa 20 kila mwaka kwa kutumia fedha za ndani, kwenye halmashauri ambazo mapato yake ni kati ya bilioni 1.5 na bilioni 5 watajenga madarasa 40 kwa kutumia mapato ya ndani, na katika halmashauri zenye mapato zaidi ya bilioni 5 watajenga madarasa 80. Kwa hiyo, yote hii ni mikakati ya kuhakikisha kwamba tunaondoa hiyo kero ya madarasa katika maeneo yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu suala la taulo za kike tuliona Waheshimiwa Wabunge wengi wamechangia, na sisi TAMISEMI tukaona ni vizuri tuka-respond. Tumeziagiza shule zote na tumeandika mwongozo kuhakikisha kwamba kwenye ile fedha ya capitation grant, asilimia kumi itatumika kwa ajili ya kununulia taulo za kike shuleni. Kwa hiyo, hilo nimeona tuliseme kwasababu ndiyo dhamira ya Serikali, na litakwenda kutekelezeka na sisi kama wasimamizi tutahakikisha hilo linafanya kazi yake. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna miradi mbalimbali ambayo ipo sasa hivi; tunakamilisha majengo, tunakarabati, tunaboresha, zikiwemo shule kongwe na zingine ambazo tumeziainisha kupitia Miradi kama ya EQUIP, SEQUIP, Boost na Shule Bora; tuna Miradi vilevile ya EP4R pamoja na LINES II. Kwa hiyo hii yote ni sisi Wizara ya Ofisi ya Rais, TAMISEMI tukishirikiana na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, tunataka kuhakikisha mtoto wa Kitanzania anapata elimu bora na anakuwa na mazingira bora na sahihi.

MHE. CONCHESTA L. RWAMLAZA: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Rwamlaza.

T A A R I F A

MHE. CONCHESTA L. RWAMLAZA: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kumpa taarifa Naibu Waziri, Mheshimiwa Silinde, kwamba hiyo capitation inayopelekwa shuleni, shilingi 4,000 inabaki Wizarani, inabaki shilingi 6,000 kwenye shule. Nina mashaka kama shilingi 6,000 hiyo ambayo haitoshelezi hata kununua chaki katika shule kama inaweza kusaidia watoto katika kupata taulo za kike.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Silinde, unaipokea taarifa hiyo?

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, nafikiri Mheshimiwa Mbunge anafikiri labda ni shilingi 6,000 peke yake ndiyo inayokwenda shuleni kwa mwanafunzi mmoja; fedha tulizotenga kwenye bajeti kwa ajili ya capitation ya kwenda kule ni zaidi ya bilioni 298. Kwa hiyo fedha hiyo wewe calculate asilimia 10 ya hiyo fedha kwa ajili ya kwenda kununulia hizo taulo za kike kwa ajili ya kusaidia wananchi, kwa hiyo hilo ndilo lengo la Serikali na tumejipanga kulitekeleza kwa vitendo.

Mheshimiwa Naibu Spika, Waheshimiwa Wabunge, niwaombe mtakapokuwa mnapita kwenye ziara zenu katika shule waombeni taarifa, kila mkuu wa shule na mwalimu mkuu wamenunua taulo za kike kiasi gani kwa kutumia fedha ya capitation. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwasababu katika shule siyo kwamba inakwenda 6,000 peke yake, hiyo 6,000 ni kwa mwanafunzi mmoja. Kwa hiyo, kama shule ina wanafunzi zaidi ya 1,000 na kuendelea maana yake unachukua ile 6,000 unazidisha mara 1,000. Kwa hiyo, kuna shule zinapata zaidi ya milioni 30, kuna shule zinapata milioni 12, kwa hiyo inategemeana.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini sasa hivi kwenye hiyo formula ya capitation grant tunakuja na formula mpya kuhakikisha kunakuwepo na minimum amount. Kwasababu shule nyingine zina idadi ndogo ya wanafunzi lakini mahitaji ya kishule yanalingana. Kwa hiyo, tumeliangalia vizuri na tuko makini katika kulikamilisha hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nimeona niyatolee hayo ufafanuzi, na niunge mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)