Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

Hon Omary Juma Kipanga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mafia

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kunipa fursa ya kuchangia hoja hii. Wachangiaji wengi wakati wakisimama hapa walikuwa wana-declare interest na wengi wao walikuwa ni walimu, na nimepata bahati ya kufanya kazi sasa na walimu, naomba ni-declare interest ya professionalism yangu, by profession ni Quantity Surveyor, kwa maana ya kwamba ni QS.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya maelezo hayo sasa naomba nichangie hoja kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote napenda kutumia fursa hii adhimu na adimu kwanza kumshukuru sana Mwenyezi Mungu aliyenijalia afya njema na leo nimepata fursa ya kusimama mbele ya Bunge lako Tukufu.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia namshukuru Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kuendelea kuniamini na kuniteua katika nafasi hii. Ninampongeza kwa kazi kubwa anayoifanya katika kuwaletea maendeleo Watanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile, sina budi kumshukuru Mheshimiwa Dkt. Philip Isdor Mpango, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa ushauri na maelekezo yao muhimu katika utekelezaji wangu wa majukumu ya kila siku.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kukushukuru wewe na Mheshimiwa Spika kwa kuliongoza Bunge hili kwa hekima, busara na weledi mkubwa. Naishukuru pia Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kwa ushirikiano mkubwa wanaotupatia; hii ni moja ya Kamati bora sana ambayo Wajumbe wake wana uelewa mpana katika sekta ya elimu na hivyo kuendelea kutoa ushauri muhimu katika kuboresha Sekta ya Elimu.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda pia kumshukuru Mheshimiwa Prof. Joyce Lazaro Ndalichako, Mbunge, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, kwa uongozi wake thabiti ndani ya Wizara. Pia namshukuru Katibu Mkuu, Dkt. Akwilapo; Naibu Makatibu Wakuu na watendaji wote wa Wizara kila mmoja kwa nafasi yake, kwa ushirikiano wanaonipa.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho lakini siyo kwa umuhimu, naishukuru familia yangu kwa upendo na ushirikiano mkubwa wanaonipatia katika utekelezaji wa majukumu yangu. Pia nawashukuru sana wapigakura wangu wa Jimbo la Mafia kwa imani yao kubwa kwangu na ushirikiano ambao umesaidia jimbo letu kupiga hatua kubwa katika kipindi cha Awamu ya Tano na ya Sita ya Serikali yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya shukrani hizo sasa naomba kutoa ufafanuzi kwa baadhi ya hoja ambazo zimechangiwa na Waheshimiwa Wabunge, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, hoja kuhusu umuhimu wa sayansi teknolojia na ubunifu; Waheshimiwa Wabunge wengi walionesha umuhimu wa kuendeleza sayansi, teknolojia na ubunifu kwa ajili ya maendeleo ya nchi. Serikali inatambua umuhimu wa mchango wa ubunifu na teknolojia katika kurahisisha na kuongeza ufanisi wa utekelezaji wa shughuli mbalimbali za kiuchumi na kijamii na ni nyenzo ya kichocheo cha maendeleo ya haraka katika sekta ya huduma za jamii na uzalishaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeanzisha Mashindano ya Kitaifa ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu (MAKISATU) kwa lengo la kuibua, kutambua na kuendeleza ubunifu na ugunduzi wa teknolojia mbalimbali unaofanywa na Watanzania, hususan wale wa ngazi za chini. Mashindano haya yanawapa nafasi wabunifu na wagunduzi wa teknolojia kujitangaza na hivyo kujulikana na wadau wa ubunifu unaozalishwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, tangu kuanza kwa mashindano haya mwaka 2019, Serikali imefanikiwa kuibua na kutambua wabunifu wachanga 1,780 kati ya hao, wabunifu mahiri 1,030 wameendelezwa na Serikali ili ubunifu na teknolojia walizoanzisha zifikie hatua ya kubiasharishwa na hivyo kuongeza fursa za ajira kwa vijana na kuchangia kwenye Pato la Taifa. Aidha, Serikali kupitia COSTECH imeanzisha vituo atamizi 17 kwa ajili ya kukuza na kuendeleza ubunifu nchini.

Mheshimiwa Naibu Spika, hoja kuhusu Serikali kuongeza vyuo vya VETA kwa kila mkoa na wilaya; Serikali ina mpango wa kuhakikisha kunakuwepo na Chuo cha Ufundi Stadi katika kila mkoa na wilaya nchini. Kwa sasa vyuo 42 vinaendelea na mafunzo, pamoja na hivyo, Serikali inaendelea na ujenzi wa vyuo 29 vya wilaya na vyuo vine vya ufundi stadi vya mikoa ambavyo vipo katika hatua mbalimbali za ujenzi. Hata hivyo, Serikali itaendelea na utekelezaji wa ujenzi wa vyuo vya VETA vya wilaya kwa kadri fedha zitakavyopatikana.

Mheshimiwa Naibu Spika, hoja kuhusu Wizara kuboresha vyuo vya ufundi ili viweze kuendana na maendeleo ya sayansi, teknolojia na ubunifu. Serikali inaendelea na kuboresha na kuimarisha vyuo vya ufundi kwa kuboresha miundombinu ya kufundishia na kujifunzia pamoja na kununua vifaa na mitambo ya kisasa. Kwa sasa Serikali kupitia mradi wa A STRIP inaendelea na ujenzi wa vituo mahiri (Centers of Excellence) katika Chuo cha Ufundi Arusha, Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam katika Kampasi za Dar es Salaam na Mwanza na Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) katika Nyanja za nishati, usindikaji wa ngozi, usafiri wa anga na TEHAMA.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kukamilika, vyuo hivi vitakuwa na hadhi ya kimataifa vinavyoweza kutoa ujuzi unaoendana na soko la ajira na hivyo kuvutia wanafunzi wa ndani na nje ya nchi. Serikali itaendelea kutenga fedha kwa ajili ya kuboresha vyuo vingine vya ufundi nchini katika bajeti yake ya maendeleo ili kuhakikisha vyuo hivyo vinatoa elimu stahiki inayoendana na mahitaji ya soko la ajira.

Mheshimiwa Naibu Spika, hoja kuhusu Serikali kuwa na utaratibu w akufanya ufuatiliaji wa wahitimu baada ya kumaliza masomo (tracer study); Serikali impokea maoni na itaendelea kuhakikisha kuwa ufuatiliaji wa wahitimu unafanyika na unakuwa endelevu ili utumike katika kuboresha mitaala ya mafunzo na hivyo kukidhi mahitaji ya soko.

Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, vyuo vikuu mbalimbali, Baraza la Elimu ya Ufundi (NACTE), Mamlaka ya Ufundi (VETA) na Taasisi ya Sekta Binafsi (Tanzania Private Sector Foundation) na mamlaka nyingine nchini hufanya tracer studies mara kwa mara kwa baadhi ya fani ili kupata taarifa za wahitimu hao, waajiriwa na waliojiajiri.

Mheshimiwa Naibu Spika, hoja kuhusu Serikali kuwa na utaratibu wa kufanya utafiti wa soko la ajira ili kubaini mahitaji…

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Naibu Waziri, kengele imeshagonga.

NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimalizie kipengele cha mwisho cha udhibiti ubora; Serikali kupitia miradi yake ya kuendeleza elimu Lens na imekuwa ikituwezesha idara ya udhibiti ubora wa shule kutekeleza majukumu yake kwa kufanya yafuatayo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, tumeongeza bajeti ya wadhibiti ubora kutoka bilioni 5.2 mpaka bilioni 5.7.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo naunga mkono hoja, nawashukuru sana kwa kunisikiliza, ahsante sana. (Makofi)