Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Kondoa
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. DKT. ASHATU K. KIJAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nishukuru kwa kunipatia fursa hii niweze kuchangia katika sekta hii muhimu kwa wananchi wa Tanzania. Naomba nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri mdogo wangu Aweso, kwa kazi kubwa anayoifanya kwenye Wizara hii na nimuambie, kwa utu wake kwa wema wake Mwenyezi Mungu atakusimamia na utatenda maajabu kwenye Wizara hii. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nianze kwa kunukuu maneno ya Mheshimiwa Rais mama Samia Suluhu Hassan, aliyoyasema tarehe 22 April, 2021 wakati akihutubia Bunge lako Tukufu, alisema maneno yafuatayo nanukuu: “Licha ya mafanikio yaliyopatikana katika miaka mitano iliyopita, tatizo la maji bado ni kubwa kwenye maeneo mengi nchini. Hali hii inachangiwa na usimamizi usioridhisha wa miradi na vile vile, matumizi mabaya ya fedha zinazotengwa, kwa ajili ya upatikanaji wa maji safi na salama.” (Makofi)
Mheshima Naibu Spika, naomba pia nimnukuu na nikupongeze sana Mheshimiwa Aweso kwa kutambua mchango wa watangulizi wako, Mheshimiwa Eng. Kamwele, Mheshimiwa Prof. Mbarawa. Mheshimiwa Prof. Mbarawa Waziri wa Maji wa Serikali ya Awamu ya Tano mwaka 2020 wakati akihitimisha hotuba ya Wizara yake alisema maneno yafuatayo nanukuu pia: “Tatizo ndani ya Wizara ya Maji sio upatikanaji wa fedha bali ni usimamizi wa fedha zinazopelekwa sekta ya maji.” (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimetanguliza maneno haya ili kumwambia Mheshimiwa Waziri kwamba, anatakiwa atengeneze kitengo chake imara cha usimamizi na ufuatiliaji wa miradi yote ya maendeleo ndani ya sekta yake husika. Hapo ndipo Taifa letu linapoteza fedha nyingi kwasababu, nimemsikia mtanguliza wangu Mheshimiwa Subira Mgalu akisema ukawazingue waliotajwa kwenye vitabu vya CAG. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunakwenda kuwazingua watu ambao wameshawaumiza watanzania faida yake ni nini! Jambo la kwanza, tunatakiwa kwanza tuimarishe usimamizi, sifa ya mradi ina mwanzo na mwisho wa utekelezaji wa mradi husika. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, na katika Serikali ndani ya Afrika zilizowekeza kwenye mifumo mingi ya kiteknolojia ni Taifa letu la Tanzania. Zipo software ambayo unaweza uka- install ndani ya ofisi yako popote ulipo, kwenye simu yako, ukafanya monitoring and evaluation ya miradi yako yote iliyopo kwenye sekta yako husika. Na hii itatuondoa kwenda kwenye post valuation, watanzania wanaumia wameshapelekewa fedha za kutosha hawapati matokeo chanya, hapana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, twendeni kimkakati miradi yote inayopelekewa fedha siku ya kwanza ujue inaanza tarehe 1 mwezi Julai inamaliza tarehe 1 mwezi wa Septemba, nenda nayo kila siku na utaokoa fedha za kutosha za watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sasa nijielekeze jimboni kwangu Kondoa, sisi wana Kondoa tunabahati kubwa tuna chanzo cha maji cha Mto Moko. Chanzo cha maji cha Mto Moko umekieleza ukurasa wa 27 kwenye kitabu chako. Ulipoeleza chanzo hiki Mheshimiwa Waziri kule ambako chanzo cha maji kipo, ni vijiji viwili tu vinavyopata maji kutoka kwenye chanzo hiki cha maji. Vijiji vyote vinavyopata maji kutoka kwenye chanzo hiki cha maji vinakwenda Wilaya ya Chemba. Kwa nini mradi huu usihujumiwe na kule ambako mabomba yanapita? Wananchi wanaona maji yanakwenda Chemba lakini wao hawana maji. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri nilishafika ofisini kwako nikakuambia, nimeona wananchi wametoboa bomba linalopeleka maji Chemba nikawauliza kwa nini wanafanya hivi? Wanasema maji yanatoka kwetu sisi hatuna maji, tunahangaika na maji tunaangalia maji yanakwenda sehemu nyingine hapana. Basi naomba Mheshimiwa Waziri nipendekeze, mnapotekeleza miradi ya maendeleo tekelezeni sera ya maji ya mwaka 2002, inayoelekeza kila Kijiji ambako miundombinu ya maji inapita, basi wao wapate maji kwanza kabla ya kule mnakowapelekea. Hii itawezesha miradi yetu na miundo mbinu yetu ya maji iweze kuwa ya kudumu kwa sababu, walinzi wa kwanza wa kudumu watakuwa ni wanavijiji ambayo mabomba yale yanapita kwenye vijiji vyao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye ukurasa wa 27 wa kitabu cha Mheshimiwa Waziri anapendekeza pia vijiji 11 vya Wilaya ya Chemba vinakwenda kupata maji kwenye bwawa la kimkakati la Kisangaji ambalo linajengwa Wilaya ya Kondoa. Kwa hiyo, vijiji 11 vipo Chemba, bwawa lipo Kondoa, hakuna Kijiji hata kimoja cha Kondoa kinachokwenda kupata maji. Wanakondoa wamekukosea nini Mheshimiwa Waziri? Naomba sana mtekeleza Sera ya Maji wapatieni maji pale Bwala la Kisangaji lilipo vijiji vyote vilivyozunguka bwala hilo viweze kupata maji. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimalizie kwa kumwambia Mheshimiwa Waziri kwamba akiimarisha Kitengo cha Tathmini na Ufuatiliaji miradi yote, mfano mradi uliopo katika Kijiji cha Sauna Kisese ingekuwa ya kuendelea mpaka leo sasa miundombinu imechoka kwa sababu hatufuatilii, fedha nyingi zimewekezwa, wananchi wanakosa maji. Vijiji vya Busi, Sambwa na Pahi wana miundombinu ya maji inahitajika fedha kidogo sana lakini Wizara haifuatilii na haijui nini kinaendelea tutakuja kuwekeza fedha nyingine nyingi ambazo hazitakuwa na msaada tena maana miundombinu ile itakuwa imeshachoka na imeoza. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema maneno haya nimalizie kumtakia kila la kheri Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ameanza vizuri na amesema tatizo la maji ni la kwake analibeba kwa kuwa ni mama. Nina uhakika kwa uchapakazi wa Mheshimiwa Waziri atamtendea haki mama yetu, atawatendea haki Watanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa fursa hii. (Makofi)