Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maji

Hon. Dennis Lazaro Londo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mikumi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maji

MHE. DENNIS L. LONDO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia bajeti ya maji. Kwanza nianze tu kwa kusema kwamba naipongeza Wizara, nampongeza Waziri ndugu yetu Mheshimiwa Aweso; Naibu Waziri, Mheshimiwa Maryprisca Mahundi na timu yake. Kwa kweli, wanafanya kazi kubwa nasi tunaiona. Nashukuru kwa jinsi ambayo ameweza ku-transform Wizara yake katika kipindi hiki kifupi. Kwa kweli, ni mwakilishi mzuri wa vijana nasi tunashukuru kwa uwakilishi huo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na kuzunguka sana katika miradi mbalimbali ya maji, sisi bado hatujakuona Jimbo la Mikumi kwa sababu hakuna mradi wa kuja kuutembelea. Hatuna mradi wa kichefuchefu wala mradi wa maji ambao unaendelea. Shida ya maji kwenye Jimbo la Mikumi ni kubwa na ninaomba niweke kwenye rekodi zako kwamba Jimbo lile linaongozwa na Mbunge ambaye anawakilisha wananchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, jukumu la kuwaangalia wanyama tumewaachia TANAPA, kwa hiyo, sasa hivi tunaangalia shida za wananchi wetu. Wananchi wetu kule shida kubwa ambayo wanayo ni maji. Kuna miji mikubwa kama Mikumi ambayo huwa unapita ukielekea Jimboni kwako kutokea Dodoma ama kupitia Dar es Salaam. Shida kubwa ya Mji ule ni maji. Usanifu umefanyika, lakini hakuna mradi wa maji na watu wana shida sana ya maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia, kwenye mji wa Ruaha ambao una watu wengi sana ambao wanafanya kazi katika Kiwanda cha Sukari Kilombero, watumishi na vibarua wale kazi kubwa ambayo wanaifanya muda wao mwingi ni kutafuta maji. Mheshimiwa Waziri, huwezi kuamini kwamba muda ambao watumishi wa kiwanda kile wanatafuta maji katika Mji ule ni mwingi kuliko muda ambao wanautumia mashambani na viwandani. Hapo hatuzungumzii wakulima.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mji mkubwa wenye uzalishaji mkubwa kama huo unapokuwa na shida ya maji unashindwa kuelewa shida ikoje katika maeneo ya pembezoni kama Ruhembe, Tindiga, Mabwelebwele, Ulaya, Malolo na hata Zombo. Kwa kweli, Jimbo la Mikumi limesahaulika kama yalivyo Majimbo mengi Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Waziri, aliangalie Jimbo hili kwa namna ya kipekee sana kwa sababu kuna vyanzo vingi vya maji ambavyo havitumiki kwa ajili ya kuwasaidia wananchi wetu kuondokana na adha ya maji ambayo inawakumba.

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ambalo ningependa kuchangia ni mahusiano ya Taasisi zetu ama wakala wetu wa maji kwa mfano MOROWASA na RUWASA. Kwa kweli mahusiano yao yanatuchanganya na hatujui nani ni nani na nani anafanya lipi? Kwa mfano, katika Mji mdogo wa Mikumi wamechukua MOROWASA na katika maeneo yote mengine wako RUWASA. Yote haya tunazungumzia ni maeneo ya pembezoni ambayo RUWASA walikuwa wanapaswa kuwa wasimamizi wa miradi hii ya maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, hatuelewi ni vigezo gani ambavyo Mikumi Jumuiya ya Maji imechukuliwa kwa MOROWASA na hasa ukizingatia kwamba ilikuwa inafanya vizuri na ilikuwa Jumuiya ya mfano katika Jumuiya zote za maji hapa Tanzania na imekuwa ikichukua cheti cha ubora kwa miaka mitatu mfululizo. Tangu wamechukua ile jumuiya wamepeleka MOROWASA, Mheshimiwa Waziri anaweza akatuthibitishia hapa performance ya maji na shida ya maji imeongezeka maradufu. Hata hayo madogo ambayo yalikuwa yanapatikana sasahivi yanapatikana kwa mgao ambao haumithiliki. Kwa hiyo, tunaomba wakati wanaanzisha maeneo mapya ya kuyagawa kati ya Mamkala ya Maji ya Mijini na Vijijini waangalie vilevile katika kuboresha hali ya upatikanaji wa maji katika maeneo hasa haya ya pembezoni. Pia hata hizi mamlaka mahusiano yake na halmashauri za miji, zinaripoti kwa nani?

Mheshimiwa Naibu Spika, tulikuwa na changamoto tulikuwa tunazungumzia kuhusiana na mahusiano ya TARURA na halmashauri zetu, lakini changamoto hiyo bado ipo hata kwa RUWASA. Hatujui ni nani ambaye anapanga vipaumbele? Nani anashiriki katika usimamizi wa utekelezaji wa miradi? Wananchi wanawakilishwa na nani katika Serikali za Mitaa kwenye miradi ambayo inahusiana na maji? Kwa hiyo, naomba hilo Mheshimiwa Waziri aliangaliwe kwa namna yake.

Mheshimiwa Naibu Spika, Chuo chetu cha Maji cha Rwegarulila kilikuwa ni chuo maarufu sana katika miaka ya 80 na 90, lakini chuo hiki kinahitaji maboresho makubwa. Naomba kupitia Bunge lako kwamba, Mheshimiwa Waziri aangalie ni jinsi gani mitaala ya chuo hiki inaendana na changamoto zilizopo. Vile vile aangalie ni jinsi gani anaweza akashirikisha vyuo vingine vya ufundi kushirikiana na Rwegarulila katika kuzalisha wataalam wabobezi katika kusimamia, ku-design na ku-implement miradi ya maji katika maeneo mbalimbali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunazungumza kwamba, maji ni uhai, lakini ni kwa kiasi gani kauli hii ina-reflect ama inaakisi uhalisia katika maeneo ya pembezoni? Kodi katika vifaa ambavyo vinahusiana na miradi ya maji bado ni kubwa.

Kwa sababu tunaamini kwamba, maji ni uhai sioni busara ya kuweka kodi kubwa katika vifaa, hasa pump za maji kwa sababu, pump za maji zinaenda kuhudumia watu. Pump za maji ni huduma, pump za maji zinaenda kupunguza ukali wa maisha kwa wananchi wetu hasa katika maeneo ya vijijini. Kwenda kutoza kodi ama kufanya pump za maji kuwa chanzo kikubwa cha kodi ni kumuumiza mwananchi ambaye tunataka twende kumtua ndoo kichwani, hasa mwanamke wa vijijini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba Wizara yetu na Taasisi za Serikali zizungumze. Zione ni jinsi gani zinaenda kutekeleza ilani ya chama chetu ambayo inasema kwamba, tunaenda kumtua mama ndoo kichwani. Hatuwezi kwenda kumtua mama ndoo kichwani kama vifaa ambavyo ni muhimu katika uzalishaji na usambazaji wa maji tunaenda kuvitoza bei kubwa, hatutafikia malengo haya.

Mheshimiwa Naibu Spika, naamini kwamba, kwa moto ambao Mheshimiwa Waziri anaenda nao na akishirikiana na Wizara nyingine kama Fedha na Wizara ya Maendeleo ya Jamii naamini kabisa tunaenda kutengeneza jumuiya za uhakika ambazo zinaenda kusimamia miradi ya maji katika maeneo yetu ya pembezoni, hasa vijijini. Miradi hii ambayo inatengenezwa ikawa na ownership ya wananchi, lakini pia ikawa endelevu.

Mheshimiwa Naibu Spika, changamoto kubwa ambayo tunayo ya miradi yetu ya maji huko vijijini ni kwamba, Serikali hata inapoweka fedha haiwi endelevu kwa sababu, hata jumuiya za maji kule haziwezeshwi, hazielimishwi, hazipatiwi msaada wa uwezeshaji, ili wajue majukumu yao, lakini pia wangalie miradi ambayo inawekezwa kwa fedha nyingi za Serikali kuwa endelevu.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha na naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)