Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maji

Hon. Deodatus Philip Mwanyika

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Njombe Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

3

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maji

MHE. DEODATUS P. MWANYIKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia katika hoja iliyo mbele yetu ya Wizara ya Maji. Nianze kwa kumpongeza Waziri na watendaji wote ndani ya Wizara hii kwa kazi kubwa wanayoifanya katika kuhakikisha Watanzania wanapata maji. Naelewa kwamba ni kazi ngumu na tunaelewa kwamba ina changamoto nyingi lakini niseme tu kwamba kazi hii wamepewa ni lazima wafanye kwasababu iko ndani ya Ilani ya Chama Cha Mapinduzi kwamba wananchi wa Tanzania wa vijijini kwa asilimia 82 watapata maji na asilimia 95 watapata maji ifikapo mwaka 2025. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hayo maneno ndani ya Ilani watu wa Njombe bado yanatutatiza Mji ya Njombe Wabunge wengi hapa wamelalamika na wanalalamika kwamba hawana maji ni tatizo kubwa lakini wengi wanalalamika kwa vile wana uhaba wa maji, lakini Njombe ni tofauti.

Mheshimiwa Naibu Spika, sisi tuna maji ya kutosha, tuna maji mengi, tuna mito inapita kati kati ya mji wetu wa Njombe upande wa huku kula Agafilo upande huku kuna mto mwingine wa Ruhuji lakini tuna visima ukichimba tu unapata maj. Pia tuna maji ya chemichemi lakini cha kushangaza ni kwamba bado mji wa Njombe tatizo kubwa kero kubwa kuliko zote ni maji, hatuna maji ya kutosha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi wa Njombe wanapata maji kwa kiwango cha asilimia kama 60 tu na wakati wa kiangazi inakuwa mbaya zaidi, sasa niseme ni aibu lakini ni aibu ambayo lazima tuishughulikie. Kumekuwa na miradi midogo midogo ambayo Serikali imekuwa ikiitekeleza kwa ajili ya kutoa tatizo hili na Rais alipotembelea Njombe Marehemu Mungu Amrehemu mara mbili alipouliza shida yenu hapa ni nini wananchi wa Njombe walisema ni maji mwaka 2015 akigomea alisema shida yenu nini watu wakasema ni maji alipokuja tena kuomba kura akawauliza watu wakamwambia hatujapata maji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri Prof. Mbarawa alikuwa pale aliitwa na akasema kwamba atahakikisha ndani ya miaka miwili maji yanapatikana ni miaka mitano sasa wananchi wa Njombe mjini hawana maji tunaongelea mjini. Jimbo la Njombe Mjini lina kata 13 kata 10 ni za vijijini na Kata tatu ni za mjini naongelea kata za mjini hazina maji sijaenda hata vijijini bado, tatizo ni kubwa tunafahamu kabisa kuna mradi mkubwa ambao umekuwa ukiongelewa lakini sisi wana Njombe tunapata wasiwasi bado hata na mradi huu mkubwa ambao tunasema wa miji 28.

Mheshimiwa Naibu Spika, na sababu kubwa ni kwa vile tulikuwa ndani ya miji 16 au 17 scope yake ilikuwa inaeleweka sasa tunaongelea miji 28. Kwa hiyo, fedha zilizotengwa ni hizo hizo miji imeongezeka shida kubwa ya Njombe kwa miradi ya nyuma ilikuwa ni kwamba bado ilikuwa ni miradi ambayo haiwezi kutatua tatizo kwa kiasi kikubwa tukaambiwa huu mradi mkubwa unakuja kumaliza tatizo tunapata wasiwasi kama kweli mradi huu utamaliza tatizo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nimuombe Waziri atuhakikishie wana Njombe kwamba maeneo yote yaliyokuwa kwenye scope yatapata maji, maeneo ya Magoda yatapata maji, maeneo ya Lunyanyu yatapata maji Chuo Kikuu cha Lutheran kitapata maji, maeneo ya Ngalange yatapata maji na maeneo ya Msete yatapata maji, mji wa Njombe ni katika miji inayokuwa haraka sana katika Tanzania ukuaji wake ni karibu asilimia 3.5 ni kidogo juu ya average kwakweli na kuna eneo la Nundu linakuwa kwa kasi kubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaomba sana Mheshimiwa Waziri hata kama scope imebadilika watu wa Njombe wawaangalie kwa tofauti kwasababu ni mji mpya ni Mkoa mpya, Mikoa mingi iliyoongezwa ina miradi mingi ya maji, hapa Njombe hatujawahi kupata mradi mkubwa hata mmoja wa Serikali, na ndio maana Rais alisema wazi Njombe tutahakikisha maji yanapatikana na Mheshimiwa Prof. Mbarawa ni shahidi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo jingine tuna mradi mwingine mkubwa ambao umekuwa ukiendeshwa kwa takribani miaka mitano sasa miaka sita unaitwa EGOGWI ninashukuru kwamba mradi huo umeonekana katika bajeti ya Mheshimiwa Waziri lakini bado ni kwa kiwango kidogo sana cha fedha, mradi huo ni kama wa bilioni nne wakati Mheshimiwa Rais Mama Samia anapita katika maeneo ya Njombe kuomba kura alisimamishwa eneo ambalo mradi unapita na akaahidi kwamba maji yatapatikana katika eneo hili. Nimkumbushe Mheshimiwa Waziri kwamba kwakweli ahadi ya Mheshimiwa Rais ambaye wakati huo alikuwa ni mgombea ilikuwa ni kwamba maji lazima yatoka. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini nipende kusisitiza mradi ule ni moja ya miradi ambayo hadi leo haijakamilika kwasababu ninaamini ni uzembe wa watendaji waliopita ndani ya Mamlaka ya maji wakati ule ilikuwa chini ya halmashauri kwakweli tunauhakika kabisa na tunaomba tunapokwenda mbele wataalam wafanye stadi za kutosha za maeneo kujua kama kuna maji ya kutosha na wahakikishe wanatumia hata wananchi wa kawaida kuwaeleza kwamba jamani pamoja na stadi zetu eneo hili lina maji ya kutosha.

Mheshimiwa Naibu Spika, wataalam kwenye Mradi wa EGOGWI waliambiwa kwamba chanzo hicho mnachotaka kuweka vijiji zaidi ya nane hakitoshi lakini walibisha matokeo yake pipe zimewekwa maji hayatoshi scope imebidi ianze kuandaliwa upya, ninadhani ni matumizi mabaya ya fedha za Serikali. Kwakweli Mheshimiwa Waziri tunawashukuru sana Watendaji ambao wako RUWASA kwa sasa maana yake wameweza kuja na mradi mpya ku-scope upya hilo eneo na kuja na mradi mpya ambao unatupa moyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini watendaji waliopita nadhani ni vizuri kauli ya Rais ianzie hapo kuhakikisha mnashughulika nao maana yake wapo na wapo kwingine na huko watafanya hivyo watafanya hivyo watatengeneza miradi isiyotoa maji na fedha za Serikali zinatumika, ni vizuri tukachukua hatua. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nipende kuongelea mradi mwingine mdogo wa mji wa Njombe eneo la Kibena, tunaishukuru Serikali ilitumia fedha za kutosha kwa kiasi fulani kuleta maji katika mji wa Kibena Kata ya Ramadhani. Lakini kilichotokea ni kwamba ndani ya mradi huo mdogo maji yameweza kuja kwa maana Serikali imeweza kuongeza Capacity ya pumps imejenga Intech mpya imeongeza mabomba ukubwa wake kutoka inchi tatu mpaka inchi tisa, sasa kuna maji ya kutosha na hospitali yetu ya Wilaya ya Njombe ya Wilaya inapata maji ya kutosha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini cha kushangaza na cha kusikitisha ni kwamba eneo lile lina wananchi wengi waliounganishwa ni wananchi kama 3,000 bado kuna uhitaji wa watu wengine 3,500. Hapa niliuliza swali la msingi nikaomba kwenye swali la nyongeza kwamba tunaomba eneo la Kibena ile project ambayo maji ni mengi yanaonekana yanamwagika iongezewe fedha kidogo basi ili distribution line iweze kuenea na watu wapate maji kuliko wao wapo mjini wanaangalia maji kwa macho na maji yanamwagika kwenye matenki sababu tu project ya kwanza ilikuwa ni ndogo haikukamilika, nakuomba Mheshimiwa Waziri uliangalie hilo kwa jicho la huruma kwa wananchi wa Njombe eneo la Kibena ili angalau tupate fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sijaona fedha zimetengwa katika bajeti hii labda kama nimeshindwa kusoma maeneo yote, lakini sijaona eneo lolote ambalo Kibena Project ya kuongezea ili wananchi waweze kupata maji ya kutosha, wananchi 3,500.

Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru sana kwa kunipa hii nafsi na niombe kwa kumalizia kwa kusema tuna matumaini makubwa sana na Mheshimiwa Waziri na wana Njombe wanamatumaini makubwa sana na Mheshimiwa Waziri Mheshimiwa Naibu Waziri na Katibu Mkuu wa Wizara hii wanachapa kazi lakini tutawapima kwa matokeo wana Njombe watawapima kwa matokeo niwatie moyo kwamba bado tunategemea kwamba mtafanya kazi nzuri na mtakamilisha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)