Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Songea Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. LEONIDAS T. GAMA: Mheshimiwa Naibu Spika, nami naungana na wenzangu kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri kwa hotuba nzuri na kwa mpango mzuri. Labda nianze mwanzoni tu niseme naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimefurahishwa sana na mpango mzima wa ujenzi wa viwanda kwa kuzingatia na uzalishaji na hasa dhamira ya Serikali ya kutumia viwanda kwa ajili ya kuinua kilimo. Ukiangalia kwenye mpango ni kwamba, viwanda hivi vinatazamiwa vijengwe ili kuwawezesha wakulima wazalishe zaidi na malighafi ya mkulima ndiyo itumike katika uendeshaji wa viwanda hivi. Kwa hiyo, naomba nichukue nafasi hii kuipongeza sana programu hiyo. Nafikiri itasaidia sana kwa wakulima wetu ambao kwa muda mrefu ama wamekuwa wakizalisha wasipate masoko au wanapozalisha, uzalishaji unapungua kwa sababu ya kukosa masoko hayo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa sisi Songea, Jimbo langu la Songea Mjini na Mkoa wa Ruvuma kwa ujumla tunazalisha sana mahindi. Kwa takwimu za mwaka 2015 tu inaonyesha wananchi wa Mkoa wa Ruvuma walizalisha zaidi ya tani 685,000, lakini uwezo wa NFRA wa kununua mazao hayo ulikuwa ni chini ya tani 50,000. Kwa hiyo, maana yake wakulima walibakiwa na zaidi ya tani 600,000. Ukichukua tani ambazo wametumia kwa chakula, hazivuki tani 300,000 na kwa maana hiyo tani 300,000 za mahindi yao zimepotea, hazina soko. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nataka niungane na Serikali, niombe rasmi kwamba, Serikali ifanye juhudi za makusudi kwa wakulima kama wale kuwawekea viwanda vya usindikaji. Kwa hiyo, naomba Serikali ione umuhimu wa kuweka viwanda vya usindikaji Songea ili uzalishaji wa mazao ya mahindi uweze kupata vile vile soko la usindikaji kutokana na viwanda vitakavyowekwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo, usindikaji unahitaji umeme, viwanda vinahitaji umeme. Mji wetu wa Songea na Mkoa wetu wa Ruvuma kwa ujumla hauna umeme wa uhakika. Kwa hiyo, sambamba na hilo, Serikali ione umuhimu wa kuhakikisha umeme wa grid ya Taifa unafika Songea ili uweze kusaidia juhudi hizi za kuanzisha viwanda. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Songea tulikuwa na uzalishaji mkubwa sana wa zao la tumbaku. Kama ilivyo Tabora, vivyo hivyo Songea, lakini uzalishaji wa tumbaku umepungua sana hasa baada ya kiwanda pekee ambacho kilikuwa kinasindika tumbaku katika Mji wa Songea kufungwa kutokana na kuhamishwa, usindikaji kwenda Mkoani Morogoro. Kwa niaba ya wananchi wa Songea, naomba Serikali isimamie kurejesha kiwanda kile ili kuongeza uzalishaji wa tumbaku ambao umepungua sana baada ya kiwanda kile kusimama.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mji wa Songea kwa kukosa kiwanda cha tumbaku hauna kiwanda cha aina yoyote. Kwa hiyo, Songea maana yake mzunguko wa pesa ni mdogo, hali ya upatikanaji wa pesa ni mdogo, wananchi wanategemea kilimo tu na kilimo ambacho hakina viwanda vinavyoweza kusindika. Kwa hiyo, maana yake wananchi wa Songea ni wananchi maskini sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza sana Mheshimiwa Waziri Mkuu, alipofanya ziara mwezi wa 12 katika Mkoa wa Ruvuma, alipata nafasi ya kutembelea kiwanda hiki na ametoa maelekezo rasmi kwamba kiwanda kile kiangaliwe ili kiweze kufufuliwa. Naomba nichukue nafasi hii kumwomba sana Mheshimiwa Waziri anayeshughulikia Viwanda, ndugu yangu Mheshimiwa Mwijage, aone namna ya kufufua kile kiwanda ili uzalishaji wa zao la tumbaku urudi upya. Hivi sasa bado uzalishaji upo, lakini kwa kiwango kidogo sana; hasa ndugu zetu wa Namtumbo, zao kubwa la biashara walilokuwa wanategemea ni zao la tumbaku; na vile vile Songea kuna maeneo ambayo yanalima zao la tumbaku. Kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Mwijage afanye juhudi hizo.
Mheshimiwa Naibu Spika, namwomba Mheshimiwa Waziri Mwijage kama kuna uwezekano aone namna ya kufuta ile kauli yake. Kuna kauli moja aliitoa hapa, nadhani tarehe 19 ile mwezi uliopita; alisema, anawaomba wananchi wa Lindi wazalishe muhogo kwa wingi, umepata soko China. Sasa kwa maelezo haya ambayo ameyatoa, tukipeleka muhogo China, maana yake tunahamisha ajira kuzipeleka China. Kwa nini tusifanye utaratibu, kama viwanda vya kuchakata muhogo vipo China, visije Tanzania vikajengwa kule Lindi au Songea ili mchakato wa usindikaji wa muhogo ufanyike Tanzania badala ya kufanyika kule China? Kwa hiyo, niseme simuungi mkono Mheshimiwa Mwijage katika hilo la kusafirisha muhogo kwenda China badala yake muhogo usindikwe hapa hapa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho naomba sana Mheshimiwa Mwijage, tunaomba viwanda Songea, lakini viwanda hivi haviwezi kuja endapo hatutakamilisha zoezi la kukamilisha ulipaji wa fidia katika eneo la EPZA ambapo pale Songea Mjini lipo eneo la Mwenge Mshindo, eneo limeshatengwa, wananchi zaidi ya 1,015 hawajalipwa fidia zao, lakini wananchi hawa wamefanyiwa tathmini mwaka 2008, mpaka sasa ni miaka nane. Nina imani kwamba gharama walizokuwa wanadai 2008, leo zitakuwa zimepanda zaidi. Kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Waziri afanye juhudi ya hali ya juu ili wananchi walipwe fidia zao ili nafasi ile ipatikane kwa ajili ya kuwekeza viwanda.
Mheshimiwa Naibu Spika, hivi karibuni wananchi wale wamefanya mikutano kule, wana wasiwasi kweli juu ya maeneo yao; wanashindwa kuyaendeleza, wanashindwa kufanya shughuli zozote za maendeleo. Juzi walikuwa wameamua kufanya maandamano ya kuja Dodoma. Nikiwa hapa Bungeni nimejulishwa hivyo na nimefanya juhudi za kuwazuia.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Waziri atakapohitimisha hoja yake, anipe uhakika wa lini wananchi wangu wa Songea, hasa eneo la Mwenge Mshindo na maeneo mengine yanayozunguka pale, watalipwa fidia zao ili waweze kuondoka katika eneo lile? Kama kuna uwezekano, Serikali ifanye utaratibu wa kuwapatia maeneo mengine ili watakapokuwa wametoka pale, wawe na uhakika wanakwenda wapi na wanakwenda kuendesha maisha yao katika maeneo gani?
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, naomba nirudie kuunga mkono hoja na naomba hizo hoja zangu ambazo nimezisema, namtaka Mheshimiwa Waziri anijibu pale atakapohitimisha. Ahsante sana.