Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Geita Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Kipekee naomba nimpongeze Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri na watendaji wote wa Wizara hii kwa kazi nzuri ambayo wameonyesha na wanaendelea kufanya. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nianze alipoanzia Mheshimiwa Katani, mimi ni sehemu ya majimbo ambayo yanatarajia kufaidika na Mradi wa Miji 28 na mji mmoja wa Zanzibar. Kwanza niseme, kama alivyosema kwamba tumekuwa kwenye matumaini tangu mwaka 2015 na nipongeze juhudi ambazo zimefanywa na Serikali, lakini nipongeze zaidi kwa taarifa ambazo ametupatia juzi Mheshimiwa Waziri kwamba sasa wamefikia sehemu, wamekamilisha taratibu zote za manunuzi na wanasubiri sasa fedha hizo ziweze kufika na waweze kuanza kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, jambo moja ambalo tunasisitiza hapa, tuliahidiwa kwamba mradi huu utaanza kabla ya mwaka huu wa fedha kuisha. Sasa juhudi hizo Serikali ndizo wajielekeze nazo kama unaanza mwezi huu, kama unaanza mwezi ujao tunataka kuona wakandarasi hawa wakiwepo site, wakiwepo kwenye maeneo husika ili tupunguze maneno ya kuzungumza kwa wananchi.
Mheshimiwa Spika, katika kila mkutano unaokwenda unazungumzia pesa za miji 28 na kwa bahati mbaya sana tumeshawapa matumaini wananchi kiasi kwamba wanapomwona mtu anachimba kisima wanashangaa kwa nini unachimba kisima wakati tunatarajia maji kutoka Ziwa Victoria. Kwa hiyo nimwombe Mheshimiwa Waziri tumemwelewa sana, tuna imani kubwa naye, lakini jambo la msingi mradi huu uanze katika mwaka huu wa fedha kama ambavyo amekuwa akituahidi na ambavyo alituahidi.
Mheshimiwa Spika, jambo lingine la pili, mwaka jana tulikuwa, tulipewa pesa kwenye bajeti bilioni 1.1 za maendeleo. Mpaka tunaingia kwenye bajeti hii pesa hizo za maendeleo zilikuwa hazijafika. Mwaka huu pia ametoa fedha bilioni 1.1 za maendeleo, napata wasiwasi sasa kama tunatenga haziendi, tunatenga haziendi, usambazaji wa maji kwenye mji wangu unakuwa hauendi kwa kasi iliyokusudiwa.
Mheshimiwa Spika, nimsaidie Mheshimiwa Waziri, GEUWASA wapo pale Geita Mjini, wakati huo huo kuna RUWASA. Kwa hiyo matokeo yake kwenye kata moja kuna GEUWASA, kuna RUWASA. Unakuta mtaa huu GEUWASA wanapeleka bomba, mtaa huo huo na RUWASA anachimba kisima. Kwenye maeneo, Mitaa ya Manga kuna RUWASA wanachimba visima, GEUWASA amefanya survey ya kupeleka bomba.
Mheshimiwa Spika, nataka kushauri, kama GEUWASA Waziri anawaamini na wanafanya kazi vizuri sana, wametoka kwenye bilioni 50 wamefanya mradi kwa bilioni nne. Waziri awape kazi ya Geita Mjini wasimamie wao, hii confusion ya RUWASA, GEUWASA atashindwa ku-coordinate kwa sababu atakuta hizi pesa ndogo anazozipeleka zina authorities mbili za kusimamia. Kwenye kata moja una RUWASA, kwenye kata moja una GEUWASA sioni inawezekanaje kumaliza tatizo la maji kwa sababu kuna watu wawili wa kuuliza maswali.
Mheshimiwa Spika, naomba Mheshimiwa Waziri awape GEUWASA wasimamie au awaondoe GEUWASA awalete RUWASA wafanye kazi pale Geita Mjini. Hii itamsaidia Waziri kuweza kujua value for money ya kazi anayoifanya, lakini kupunguza maswali. Natamani sana kuona GEUWASA wakipewa kazi ile kwa sababu jana amesifiwa mtu wa DAWASA na mimi namsifia kwa kazi nzuri anayoifanya, lakini wale GEUWASA katika kila pesa wanayofanya saving wamekuwa wakiongeza usambazaji wa maji pale mjini. Kila saving wanayoifanya wanaongeza usambazaji. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ukienda Kasamwa, ukienda kwenye kata za pale mjini zina uhaba mkubwa sana wa maji, wanaojua vizuri matatizo ya maji ni GEUWASA. Sasa kwenye hiyo hiyo unapeleka RUWASA kwenye kata hiyo hiyo unapeleka GEUWASA, utajikuta pesa ndogo za Serikali zinashindwa kutoa matunda yaliyokusudiwa.
Mheshimiwa Spika, la mwisho, pale Geita Mjini ni kilometa kama tano kutoka ziwani, mradi mkubwa pekee wa maji ni Mradi wa GGM walioujenga kwa CSR. Kwa hiyo tuna visima visima vingi, usambazaji wa maji kwenye Mji wa Geita katika taasisi nyingi umekuwa ni mdogo sana. Kwenye Kata za Mtakuja tuna vituo viwili vya afya havina maji. Kwenye Kata ya Mtakuja kuna shule za sekondari mbili hazina maji, tunasomba maji kwa kutumia malori.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo wakati tunasubiri huu mradi wa fedha za India naomba sana pesa za maendeleo za kusambaza maji kwenye kata hizi ziweze kutolewa ili hizi kata na Taasisi za Serikali ziache kupeleka maji kwa kutumia malori. Wanaposomba maji kwa kutumia malori inabidi wanafunzi waanze kutumia maji kwa mgao, lita tano kwa masaa 24. Mheshimiwa Waziri unajua wanahitaji kuoga, wanahitaji kufua, kwa hiyo, tunawafanya wanafunzi wetu kuwa wachafu, lakini tunawafanya pia kushindwa kuwasimamia.
Mheshimiwa Spika, nimwombe sana Waziri, naamini kwamba Mfuko wa Maji kama alivyosema mchangiaji aliyetangulia ni mdogo na tumepiga kelele sana kwenye Bunge hili ili kuweza kuuongezea pesa, lakini hizi pesa zilizopo tuzigawe vizuri, tuzisimamie vizuri, kwa sababu zina uwezo wa kuleta matokeo.
Mheshimiwa Spika, kutokana na muda, naomba nikushukuru sana kwa nafasi hii. (Makofi)