Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mbulu Vijijini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
2
Ministries
nil
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuongea mchana huu wa leo. Kwanza napenda nimpongeze Mheshimiwa Waziri ndugu yangu Awesso na dada yangu Mheshimiwa Eng. Prisca kwa kazi wanazofanya kwenye Wizara hii. Ninakupongeza kwasababu ninajua jinsi ambavyo umesumbuka na Wizara hii, tangu ukiwa Naibu Waziri na sasa Waziri. Nataka nikupe moyo najua kuna changamoto, Biblia inasema namna hii kwenye kitabu cha Mwanzo mstari wa 1 na nikuambie tu unashughulika na kazi ya uumbaji ujue hilo unapotafuta maji. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mwanzo anasema kwenye mstari ule wa 1, hapo mwanzo Mungu aliumba mbingu na nchi, nayo nchi ilikuwa tupu na giza lilikuwa juu ya uso wa vilindi vya maji, na roho ya Mungu ilitulia juu ya uso wa maji. Kwa hiyo, Mheshimiwa Awesso jua unazungumza na unafanya kazi katika hali ya uumbaji. Nakumbuka unapotembea kutafuta maji, unaposaidia kuipa maji nchi ujue kwamba unasumbuka na kazi ambayo Mungu aliifaya hapo mwanzo. Na nikuombee Mungu akusaidie katika hayo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini sasa umekuja Mbulu Vijijini nakushukuru, sasa ujue hiyo kazi Mbulu Vijijini inahitajika sana hiyo ya uumbaji kutafutia watu maji na katika slogan zetu tumewahi kusema maji ni uhai. Kwa hiyo, bwana, tusaidie tupe uhai katika Mbulu Vijijini. Ninashukuru nimeona kwenye bajeti imetengwa bilioni 2,300,000,000/= hii ni wazi kwamba, tunafanya kazi hii na niishukuru sana Serikali umetusaidia sana kwenye visima vya pale Haydom. Sasa kuna ahadi ya Mheshimiwa Rais ameitoa pale Samia Suluhu Hassan ya kutoa maji katika Ziwa Madunga kuleta katika Mji wa Dongobesh. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba nishauri kiujumla, hii kuchimba visima naomba Wizara iangalie Je. ni njia sahihi ya kuwapatia watu maji? Maana visima vidogo vidogo wanavyochimba ninahakika katika maeneo mengi visima vile vimekufa kwasababu, tu maji maeneo mengine yanachimbwa na wanakutana na mwamba basi hela inakuwa imetumika zaidi. Kwa nini Wizara isiende ikachukue maji kwenye sehemu yenye ziwa ikapeleke kwenye vijiji pakawa na usambazaji, kuliko kila mahali kuchimba visima ambavyo baadaye vinakauka na hali kadhalika Serikali inakuwa imeharibu hela pale.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo niombe Wizara ione namna hii kwamba, tunapochimba visima hivi vinatusaidia sana? Au kuchukua maji kwenye Ziwa na kuyasambaza? Nadhani tukichukua maji kwenye maeneo yenye Ziwa tukasambaza maji, fedha ya Serikali itatumika na watu wengi watapata maji kwa maeneo mengi. Sasa niombe kwenye bajeti yetu naona kuna vijiji umeviweka vingine si vya Jimbo langu na nimeshakuambia tangu jana wataalam wako waangalie, waweke visima vilivyo na majina yaliyopo kwenye Jimbo langu la Mbulu Vijijini. Naomba nikutajie sina hakika kama Hansard itashika lakini najua tutaongea baadaye.
SPIKA: Haya mjiandae Waheshimiwa Wabunge anataja majina. (Makofi)
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Spika, kuna kisima cha Gembaku, kuna kisima Getanyamba, Qaloda, Edahagichani, Maheri, Maretadu, Endadubu, Galoda, Dotina, Labay, Ng’orati, Garbabi, Qatabela, Qheteshi, Endaanyawish na Endaharqadat. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sasa ndugu yangu mpendwa hivi ndio vijiji vyangu, lakini vijiji ulivyoviweka sio vya kwangu kabisa, angalia kitabu chako cha bajeti. Wataalam waangalie vijiji walivyoweka si vya kwangu lakini waviweke basi hivi nilivyovitaja kwasababu, najua ndivyo vilivyoombwa katika bajeti toka Wilayani.
Mheshimiwa Spika, nikushukuru sana naamini atakuwa amevishika na ndugu yangu Awesso ni kijana mzuri sana na slogan zako nazipenda. Bwana sikufichi na kule kwetu nawapongeza sana wataalam wa maji wamejitahidi sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, maji katika Mkoa wa Manyara kuna shida kubwa sana ni asilimia 53 kwa Mkoa wa Manyara unaopata maji. Kwa hiyo, ni chini ya asilimia ya nchi. Lakini pia, Jimbo la Mbulu Vijijini tuna asilimia 59 si mbaya sana lakini si nzuri sana. Lakini ukiangalia pale Haydom Mheshimiwa Aweso, uliahidi mwenyewe kisima kichimbwe mpaka leo kisima hakijachimbwa bwana. Haydom pale tuna asilimia 52 tu ya wakazi wanapata maji basi nikuombe sana angalia maeneo hayo. Lakini Haydom na Dongobesh tumeomba mtusaidie tupatieni Mamlaka ya Maji kwasababu, kuna jumuiya ya watumia maji wana hela nyingi sana pale zaidi ya milioni 400, ukiwaacha wale wananchi watumie ile hali ya watumia maji hainogi sana kwa sababu pale hawana wataalam wanaofanya kazi hiyo sio wakuajiriwa.
Mheshimiwa Spika, lakini Haydom na Dongobesh tumeomba mtusaidie tupatieni Mamlaka ya Maji kwa sababu kuna Jumuiya ya Watumia Maji wana hela nyingi sana pale zaidi ya shilingi milioni 400, ukiwaacha wale wananchi watumie utaratibu ule wa watumia maji hainogi sana. Nasema hivyo kwa sababu pale hawana mafundi na wataalam wanaofanya kazi hiyo sio wa kuajiriwa kwa hiyo kudhibiti ile fedha kwa kweli hali si njema. Nikuombe sana uone jambo hili kwa sababu ni mji mkubwa unakua na kuna hospitali kubwa ya Rufaa ya Haydom.
Mheshimiwa Spika, suala kubwa zaidi ni units za maji, imekuwa kero sana katika Mji wa Haydom na Dongobesh, unit imekuwa Sh.2,000. Mheshimiwa Waziri utakapofikia hatua ya kupelekea pre-paid machine za kulipia maji, nikuombe kabisa anzia na hiyo miji ya Haydom, nafikiri mambo yatakwenda vizuri sana.
Mheshimiwa Spika, suala lingine DDCA wamechimba visima tisa hawajapeleka maji yaani wamechimba pump wakazifunika. Niombe wazipeleke zile pump ili watu wapate maji. Wananchi wanapoangalia pump inakuwa taabu.
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, naunga mkono hoja. (Makofi)