Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maji

Hon. Mohamed Lujuo Monni

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Chemba

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maji

MHE. MOHAMED L. MONNI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi nami nichangie kwenye Wizara hii muhimu sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, takwimu ambazo zimetolewa na Wizara ya Maji zinaonyesha asilimia 72 ya watu waishio vijijini sasa wanapata maji, lakini kwenye wilaya yangu sidhani kama asilimia 42 inafika. Nilikuwa nategemea sana mradi mkubwa wa Bwawa la Farkwa na kwenye mradi huo tayari Serikali ilitoa zaidi ya shilingi bilioni 7.8 kuwahamisha watu, lakini cha ajabu zaidi, haukutengewa hata shilingi moja kwenye bajeti hii. Wasiwasi wangu mkubwa ni kwamba sasa wale watu wanaenda kurudi pale na hakuna namna tena ya kuja kuwaondoa.

Mheshimiwa Naibu Spika, yapo mambo mengi, kulikuwa na migogoro mingi sana kwa ajili ya kuhakikisha watu wale wanahama pale. Sasa hili jambo limenishtua sana. Nilitamani wakati Waziri anakuja ku-wind-up aniambie kwanini hawakutenga fedha angalau kidogo kwa ajili ya bwawa lile? Ninaamini, ili tuweze kutatua changamoto ya maji kwenye Makao Makuu ya nchi, ilikuwa ni lazima tuanze haraka sana utekelezaji wa mradi ule kwa sababu mradi ule ni katika miradi ya maji ya kimakakati tuliyonayo.

Mheshimiwa Naibu Spika, naiomba sana Wizara, Wilaya yangu ya Chemba ni katika Wilaya ambazo ni kame kweli kweli na ndiyo maana tumejaribu kufanya miradi mingi ya maji na miradi mingine inashindikana hasa ile ya kuchimba visima. Nasi tunaamini, namna peke yake ya kutatua changamoto za maji kwenye wilaya ile ni kujenga bwawa hili kwa haraka sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, nilitaka kusema pia, kuna changamoto nyingine ambazo zinashangaza sana. Tuna visima ambavyo vilichimbwa mwaka 2014. Katika visima vile, wakati huo Halmsahauri siyo RUWASA; walitangaza tenda kwa ajili ya usambazaji. Mkandarasi akapatikana, lakini mpaka leo hii hawajasaini mkataba wa yale maji wasambaze. Mpaka leo, kuanzia mwaka 2014! Vile vile maji yale yamechimbwa kilometa sita kutoka vijiji vilipo. Kwa hiyo, haina faida yoyote kwa sababu lazima watu waweke punda kwenda kuchota maji kilometa sita.

Mheshimiwa Naibu Spika, nami naiomba Wizara ya Maji ikashughulikie visima vile vitatu ambavyo ni Chandama, Mapango na Machiga. Watu wengi ambao hawajasoma kule kijijini wanashindwa sana kuelewa, inawezekanaje mkachimbe maji, mtangaze tenda, mkandarasi apatikane, halafu msisaini afanye kazi? Wanashindwa kuelewa, nini kinaendelea pale? Naomba Waziri wa Maji atakapokuja ku- wind-up hotuba yake ya mwisho, aseme chochote ili watu wa kule watuelewe.

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine, nimeona mmenipa visima kadhaa vya maji; mmeonyesha kwenye jedwali kwamba tutapata visima 13 kwenye bajeti hii, lakini mmetenga shilingi milioni 180. Ni ukweli usiopingika kwamba kwa namna ambavyo Wilaya ya Chemba ilivyo dry milioni 180 haziwezi kuchimba visima 13. Sana sana zitachimba visima vinne. Sasa takwimu hizi ni za kwenda kumgombanisha Mbunge na watu wake, kwamba tumetajiwa vijiji ambavyo vinaenda kupata maji, lakini kiuhalisia ni kwamba maji kwa bajeti hii haiwezekani. Namwomba Mheshimiwa Waziri, anapotenga fedha angalie na Wilaya zenyewe na namna gani unaweza kupata maji kwenye mazingira haya? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna changamoto nyingine hii inaitwa ya manunuzi. Tulipata mradi pale Chemba Mjini na tuliambiwa mradi ule una shilingi milioni 250, lakini mpaka leo umeshindwa kutekelezwa. Ukimwuliza Meneja wa RUWASA, tangu mwezi wa 11 anasema watu wa manunuzi hawajaleta vifaa mpaka leo, miezi sita. Nami nikisimama jukwaani nawaambia ndugu zangu tumepata fedha milioni 250 tunaweka sawa mambo ya maji hapa. Jambo dogo kama hilo, tunatumia miezi sita kununua vifaa vya maji, sijui mabomba, mnatuweka kwenye wakati mgumu sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, nawashukuru sana, juzi baada ya Waziri wa TAMISEMI kuja pale, mmetupa shilingi milioni 150. Siku mbili tu kaja, ametoa shilingi milioni 150 kwa ajili ya kuhakikisha maji yanapatikana pale hospitali. Nawashukuru sana, lakini nawaomba msisubiri mpaka Mheshimiwa Waziri aje, tukiwaambia sisi, ndio tumewaambia mahitaji ya watu waliopo kule.


Mheshimiwa Naibu Spika, hilo pia nilitaka niseme, tuachane na utaratibu kwamba manunuzi lazima yafanyike HQ, kila mtu ukimuuliza yanafanyika HQ, sisi tuko Dodoma HQ Dar es Salaam tunahitaji vifaa vya milioni 20 tunasubiri mpaka watu wa Dar es Salaam waje wanunue, hii haiwezi kuwa sawa hata kidogo. Nimwombe Waziri abadili utaratibu au aweke utaratibu ambao ni rafiki ili tunapopitisha bajeti vifaa vile vipatikane kwa haraka zaidi.

Mheshimwa Naibu Spika, nataka pia niongelee juu ya uchakavu wa miundombinu ya maji iliyopo katika wilaya yangu. Tuna miradi mizuri kabisa ambayo imekuwepo kwa muda mrefu, changamoto kubwa tuliyonayo sasa maji hayapatikani. Shida ni ndogo tu, wakati mwingine unaona


mradi unahitaji milioni 30 tu, lakini kata nzima inashindwa kupata maji kwa sababu tu eti fedha za kukarabati miundombinu milioni thelathini mpaka uende kuomba Wizarani.

Mheshimiwa Naibu Spika, jana nilikuwa nimefanya ziara kwenye Kata moja ya Nahoda, tenki limepasuka, tenki lenyewe kulinunua ni milioni moja, watu zaidi ya vijiji sita zaidi ya miezi mitatu hawapi maji. Nimwombe sana Waziri lazima tuwe na utaratibu rafiki ambao unawezesha pale matatizo yanapotokea, pale changamoto za maji zinapotokea waweze kuzitatua kwa urahisi na kwa haraka zaidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo nakushukuru sana kwa kunipa nafasi. (Makofi)