Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maji

Hon. Daniel Awack Tlemai

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Karatu

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maji

MHE. DANIEL A. TLEMAI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi hii niweze kuchangia bajeti hii ya Wizara ya Maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Mji wa Karatu upatikanaji wa maji ni kwa asilimia 33 ambayo unaunganishwa na bwawa mbili, moja iko kwenye eneo la Patom na nyingine iko kwenye eneo la Bwawani. Na eneo hili la Bwawani limejaa maji na borehole lile haifanyi kazi, na Mheshimiwa Naibu Waziri alituenzi kutembelea Jimbo la Karatu na ukiangalia Mji wa Karatu ni wa kitalii na upatikanaji wa maji ni asilimia 33. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo hili la Bwawani waliomba shilingi milioni 440 kwa mwaka jana na mwaka huu lakini kilichopatikana ni milioni 175 katika eneo hili la Bwawani katika Mji wa Karatu. Kuna eneo lakini Ayalabe, Kata ya Ganako, waliweza kuomba 599,131,000 lakini kilichopatikana ni 168,000,000, hizi zingine bado hazijapatikana.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika bajeti hii ya mwaka huu kwa Wilaya ya Karatu Wizara imetenga shilingi bilioni mbili na milioni sabini na saba. Sasa hofu yangu ni kwamba kama mwaka jana tuliweza kuomba milioni 599 ikapatikana milioni milioni 168 na wakati huo katika eneo hili la Bwawani waliomba milioni 440 na ikapatikana milioni 175, hofu yangu ni kwamba katika upatikanaji wa pesa, na kama ingeweza kupatikana bilioni mbili ambayo sasa umetenga kwenye bajeti ya mwaka huu wa 2021/2022, kwamba sasa kama inaweza kupatikana hiyo bilioni mbili angalau changamoto katika Mji wa Karatu na maeneo mengine ya vijijini ingeweza kupungua kidogo.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Mji ule wa Karatu wakazi wako 62,300, uhitaji wa maji ni lita milioni tano lakini upatikanaji kwa sasa ni 1,680,000, sasa wangeangalia kidogo katika Mji wa Karatu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika eneo hili la Mji wa Karatu, eneo la Bwawani limejaa maji, na kule wameomba shilingi milioni 175 ambayo kwa sasa hivi haijaweza kwenda kufanya kazi kutokana na eneo lile kujaa maji, wanaomba ile milioni 175 ambayo sasa ililetwa kwa ajili ya Mji wa Karatu eneo la Bwawani iende katika eneo lile la Ganako ambako sasa kule kazi inaweza kufanyika kwa sababu kule kuna borehole mbili katika eneo hili la Ganako.

Mheshimiwa Naibu Spika, ombi langu kwa Waziri ni kwamba hii shilingi milioni 175 ambayo kwa sasa huwezi kufanya kazi katika Bonde lile la Bwawani iende sasa katika eneo lile la Ganako ili angalau uhitaji wa maji uweze kuongeza. Mradi huu wa Ganako ukikamilika upatikanaji wa maji pale unaweza kwenda kwenye asilimia 61. Ombi langu kwa Wizara ni kwamba ile shilingi milioni 175 ambayo kwa sasa Mji wa Karatu pale Bwawani hauwezi kufanya kazi kutokana na maji yamejaa pale na Mheshimiwa Naibu Waziri alitembelea eneo lile sasa iende katika eneo hili la Ganako ili angalau tutoke kwenye asilimia 33 twende asilimia 61. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika eneo hili la Bwawani maji yanajaa mara kwa mara na watu wanashindwa kupata maji kutokana na eneo lile kujaa maji. Tuliomba Wizarani shilingi milioni 40 kuhamisha pampu pale kwenda kwenye eneo lingine la juu kidogo ili angalau wananchi wasiendelee kuteseka. Niwaombe watu wa Wizara waweze kutupatia shilingi milioni 40, ni hela ndogo sana, ili tuweze kuhamisha ile borehole. Mheshimiwa Naibu Waziri ni shahidi ametembelea maeneo yale na amejionea kwamba kipindi cha mvua watu hawawezi kupata maji katika Mji wa Karatu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Mji wa Karatu maeneo ya vijijini kuna mradi wa World Bank wa vijiji 10, huu mradi una zaidi ya miaka 10 kila siku ni ukarabati maji hayapatikani. Nafikiri katika eneo hili tumetengewa shilingi bilioni 2, kama itapatikana mradi huu wa World Bank kwa vijiji 10 katika eneo la Karatu Vijijini maji yanaweza kupatikana ili na kule kijijini tuweze kufika asilimia kubwa kidogo kuliko tuliyonayo sasa hivi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika eneo lile la Karatu Vijijini upatikanaji wa maji katika Tarafa ya Bulumbulu ni wa njia ya mtitiriko na katika eneo hili wametenga shilingi milioni 520 ikipatikana kwa muda nafikiri tutakuwa tumepiga hatua kidogo kule kwetu Karatu. Mimi sina mashaka maana Waziri ameanza vizuri na namtakia kila la kheri ili angalau eneo hili la maji tuweze kulipatia ufumbuzi vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mji wa Karatu tunaomba sana hii shilingi milioni 40 tuweze kuipata lakini vilevile tunaomba hii shilingi milioni 175 iweze kwenda eneo lile la Ganako ili angalau wananchi wale wa Karatu waweze kutoka kwenye asilimia 33 kwenda asilimia 61.

Mheshimiwa Naibu Spika, tuna miradi mbalimbali katika eneo letu la Karatu. Kuna mradi huu wa Mang’ola Juu ambao ni wa World Bank ambao kwa sasa wametenga shilingi milioni 100. Vilevile kuna mradi huu ambao unaenda Laja/Umbangw ambao umetengewa shilingi milioni 519. Mradi wa Chemchem umetengewa shilingi milioni 200 na mradi wa Gidbaso ambao umetengewa shilingi milioni 180.

Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, kuna mradi huu wa Makhoromba ambao umetengewa shilingi milioni 240. Vilevile kuna mradi wa Kwa tom ambao umetengewa shilingi 65. Pia kuna mradi huu wa Gendaa ambao umetengewa shilingi milioni 45 na mradi wa Endala ambao umetengewa shilingi milioni 136. Pia kuna mradi wa Kilimatembo, Rhotia, Rhotia Kainam, Lositete, Kitete na Marera ambao umetengewa milioni 520 na mradi wa Chemchem, Kambi ya Simba, Huduma, Bashay, Endesh na Endagem umetengwa shilingi milioni 50.

Mheshimiwa Naibu Spika, jumla ya fedha kwa jimbo langu ni Sh. 2,412,900,135. Fedha hizi zikipatikana kwa Jimbo la Karatu tutapiga hatua zaidi ya kimaendeleo kwa sababu Mji wa Karatu ni Mji wa kimaendeleo na utalii na sisi si wachovu ni wakulima wazuri tu ambao tunaleta mchango mzuri katika eneo la mapato ya Serikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru na pia naunga mkono hoja. (Makofi)