Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mkinga
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. DUSTUN L. KITANDULA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa fursa hii ili nichangie kwenye mjadala wa hotuba iliyopo mbele yetu. Nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu ambaye ametupa uhai na kwamba tunaishi kuwatumikia Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, moja kwa moja, nianze kuishukuru Serikali, kumshukuru sana Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri na timu ya Wizara ya Maji, kwa hiki ambacho kwa mwaka huu nakiona katika bajeti hii. Nimesema mara nyingi kwamba katika Mkoa wa Tanga kama kuna Wilaya inashida kubwa ya maji ni Mkinga. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tumepiga kelele sana kuzungumzia tatizo la maji Mkinga, tulikuwa hatusikikisikiki hivi lakini hizi dalili zinazoziona kwenye bajeti hii namshukuru sana Mheshimiwa Waziri na timu yake. Kwa mara ya kwanza katika bajeti hii Wilaya ya Mkinga tumetengewa shilingi bilioni 5 za maji. Katika historia ya kuwepo kwa Mkinga hizi ndiyo fedha nyingi kwa mara ya kwanza. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, wakati tukisikia wenzetu wana shilingi bilioni 15 au 20, sisi tunashukuru kwamba kwa mara ya kwanza tumepangiwa shilingi bilioni 5. Hatujawaji kuwa na mradi mkubwa wa Kitaifa kwa mara ya kwanza kilio chetu cha kuwekewa maji kutoka kwenye Mto Zigi kimesikika, nawashukuru sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa naangalia vitabu pale nimeona mmetutengea shilingi bilioni 3, nawashukuru sana. Sasa vijiji vile 32 vya Tarafa ile ya Mkinga vinaenda kupata maji ya uhakika. Nawashukuru. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, najua fedha hizi hazitoshi lakini ule uthubutu tu wa kusema hapana tuanze kwa kupeleka shilingi bilioni 3 mimi nawashukuru sana. Niwaombe wakati tunapoenda ku-design bomba lile tuhakikishe inafanyika kwa full capacity. Kwa nini nasema hivi? Ni kwa sababu Mkinga ukanda ule ndiyo wenye potential kubwa ya uwekezaji wa viwanda. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, juzi Mheshimiwa Rais wameingia Memorandum of Understanding na Rais wa Kenya kwa ajili ya bomba la gesi kutoka upande huu kwenda Kenya. Waziri Mkuu alipokuja alituhakikishia kwamba kituo kikubwa cha kuchakata gesi hiyo kitakuwa Mkinga. Nini maana yake? Maana yake tutavutia ujenzi wa viwanda, kile kilichotokea Mkuranga kinaenda kutokea Mkinga. Sasa tujipange tuhakikishe bomba hili linakuwa na uwezo mkubwa ili tusije kuhangaika wakati ujao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, Miradi ya Mbuta na Mwakijembe, nilikuambia Mheshimiwa Waziri kwamba miradi hii sijui kwa nini imesahaulika kuitwa miradi ya kichefuchefu, kwa sababu tumekwenda mimi na wewe unajua, Naibu Waziri amekwenda, miradi hii tangu mwaka 2019 mpaka leo hakuna kinachoeleweka. Kwa mwaka mzima huu wa bajeti hakuna kazi yoyote iliyofanyika kuendeleza miradi hii miwili, hii haiwezi kuwa sawa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimeambiwa ule mradi wa Mwakijembe arbitration ile imeisha lakini sijui kuna kigugumizi gani. Pale Mbuta tumepata mkandarasi alikuwa anatakiwa aanze kazi mwezi Januari ameshindwa vigezo, tumemtafuta mkandarasi wa pili, majadiliano yanaendelea hii itatupeleka mpaka kuisha mwezi wa sita, mwaka mzima miradi hii itakuwa hiajafanya chochote, haiwezi kuwa sawa. Naomba tuongeze jicho kuangalia jambo hili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile nakushukuru kwamba kuna miradi kadhaa imetengewa fedha. Mradi wa Kwantili, Churwa, Muheza, Mihunduro, Bangamwevengero, Mchangani tuna shilingi milioni mia moja na kitu. Kuze, Kibago, Bosha kwa Ntindi, Muze, Kafishe tuna shilingi milioni 173. Bantu, Kwa Ngena, Machimboni tuna shilingi milioni 100. Kidundui, Kwekuyu, Bombo Mbuyuni, Mgambo, Shashui, Emsambia mpaka Vuga tuna shilingi milioni 300 na Ng’ombeni tuna shilingi milioni mia mbili na kitu. Kuboresha ule mradi wa Daruni tuna shilingi milioni 300. Gombero, Vunde, Manyinyi, Jirihini, Dima tuna shilingi milioni 123. Mowa, Zingibari, Mayomboni shilingi milioni 82. Nashukuru sana kwa miradi hii lakini wakati nikushukuru kutengwa fedha hapa ni jambo moja, fedha hizi kwenda katika halmashauri ni jambo lingine. Tunaomba fedha hizi zifike ili tuondokane na tatizo la maji. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, nakushukuru sana. (Makofi)