Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. NEEMA G. MWANDABILA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuweza kuchangia. Awali ya yote, napenda kutoa pongezi zangu za dhati kwa moyo mkunjufu kabisa kwa viongozi wa Wizara hii, Mawaziri, Makatibu kwa namna ambavyo wamekuwa wakifanya jitihada kubwa kuhakikisha tunapata maji katika maeneo yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kabla sijachangia kile ambacho kinaugusa moyo wangu sana nilitaka nitoe kama taarifa kwa Wizara hii kwamba ile miradi ya maji waliyoiweka kule Tunduma maji hatupati na kisingizio ni kwamba fedha za kununua LUKU hakuna. Naambiwa kwa wiki fedha inayotakiwa ni karibu shilingi 700,000 hadi shilingi 1,000,000. Kitu ambacho siamini kabisa kwamba Wizara mpaka sasa imeshindwa kukaa na watu wale kule chini kuweza kuweka utaratibu mzuri wa kuhakikisha tunapata maji. Hata hivyo, tunawashukuru sana kwa ile miradi ya maji, tunaamini kama mambo haya madogo madogo atayazingatia tutaweza kupata maji kwa uhakika. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia naomba Wizara iweze kukaa na wale watu wahakikishe Mji kama Mpemba unaokua kwa kasi uweze kupata maji. Ni mji unaokuwa kwa kasi lakini mpaka saa hizi maji hakuna na wanategemea mradi wa kutoka Ileje kuja Tunduma kitu ambacho najua mradi huo hautakamilika leo. Niikumbushe Wizara kwa kuiomba kwamba ule Mradi wa Maji kutoka Ileje kuja Tunduma ambao ni karibu shilingi bilioni 17 tu, mtusaidie tuweze kufanya kazi haraka kulingana na mahitaji ya Mji wa Tunduma. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia nilitaka kuiomba Wizara kuhusiana na maji Wilaya ya Ileje. Maji yanayotoka ni machafu, yana takataka kitu ambacho siamini kama Wizara inashindwa kutoa chujio la kuchuja maji katika Kata ya Itumba ili tuweze kupata maji masafi. Hata sisi tungependa kuonekana tuna nguo safi, nadhifu na hata yale mashuka kwenye hospitali kule ya wilaya yawe basi yana mvuto kwa sababu maji yale yanapelekea hata mashuka kwenye hospitali ile yanakuwa machafu. Alikuja Mheshimiwa Mollel, Naibu Waziri wa Afya aliona hali halisi na namna mashuka yanavyoharibika katika hospitali ile ya wilaya kutokana tu na kwamba maji ni machafu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, napenda sasa kujielekeza kwenye hoja ambayo kwa kweli inaniumiza na inatia uchungu sana ninapokuwa nikiifikiria. Katika shule zetu nyingi maji hakuna. Tarehe 8 Machi, nilipata nafasi ya kwenda kwenye shule mbili ya Chikanamlilo na Mpakani Sekondari, Chikanamlilo ipo Wilaya ya Momba, tulikuta watoto wanaugua matumbo kwa sababu hakuna maji. Nimshukuru Mheshimiwa Condester aliweza kuwapatia zile taulo za kike zenye dawa ili wale Watoto zaidi ya mia moja waweze kupona ule ugonjwa uliokuwa unawasumbua wa matumbo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nilipopewa hii changamoto pale kwamba maji hakuna nilijaribu kufuatilia, uzuri wake tulikuwa na Mheshimiwa DAS pale. Maji katika Kata ya Ndalambo yapo shida ikaonekana ni kwamba shule haiwezi kuvuta yale maji kwa sababu gharama za kulipia yale maji ni kubwa na shule kwa kulingana na pesa inayopata haiwezi kugharamia.
Mheshimiwa Naibu Spika, nikaona sasa hii ni changamoto ya sisi kama viongozi kuichukua na kuweza kuisemea kwamba Wizara ya Maji na hizi taasisi nyingine mfano hii Wizara ya Elimu waweze kukaa, wajadiliane, waangalie kwanza ni kwa namna gani hizi shule ziwe na uhakika wa maji? Nilitamani kama viongozi tuje na sheria ya kwamba maji kwenye shule iwe kigezo kimojawapo cha kuhakikisha shule inasajiliwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, imagine tangu asubuhi mtoto anaenda shuleni, hanawi mikono, atatamani ale kitu, atalamba mikono; penseli zenyewe wanalamba, watoto wataacha kuugua? Kwa hiyo, niseme kwamba kwa hili ningependa kabisa Wizara ya Maji ichukue kama changamoto ya msingi na ikiwezekana kwenye miradi yake ya msingi, waongeze mradi ambao utakuwa mahususi kwa ajili ya taasisi ambazo zinahudumia watu wengi ambazo ni shule, vituo vya afya, mahospitali na vitu kama hivyo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kwa sababu Sheria ya Maji imetaja wazi kabisa kwamba maji ni haki ya kila mwananchi, maji ni huduma ya msingi, usafi wa mazingira ni huduma ya msingi ya wananchi, watuangazie katika eneo hili. Kwa sababu, kutibu maradhi yatokanayo na uchafu ni gharama kubwa sana, pia kitendo cha kutokuwa na uhakika wa maji kinasababisha watoto washindwe kusoma vizuri. Hii ni kwa sababu sehemu wanazoenda kutafuta maji ili waje wamwagilie tu kwanza maeneo yao pale ni shida; na maji ya kuja kusafishia tu madarasa yao inakuwa ni shida. Kwa hiyo unakuta mtoto anachoka kuchota maji. Badala ya kukaa atulie kusoma, anawaza tu dumu lake la maji atunze vipi? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, baada ya kusema hayo, naomba niseme nashukuru. Mchango wangu unaishia hapo kwa leo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. (Makofi)