Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Magu
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. BONIVENTURA D. KISWAGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii ili niweze kuchangia kwenye Wizara hii muhimu ya maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa, naomba kwa namna ya pekee nimpongeze na kumshukuru Waziri wa Maji, ndugu yangu Mheshimiwa Awesso ambavyo anajitahidi sana kuhangaikia kuhakikisha kwamba wananchi wanapata maji katika nchi hii pamoja na Naibu wake na Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, ndugu yangu Sanga. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kama ambavyo wenzangu wamesema hapa, kwa kweli maji ni uhai na hakuna kitu kingine ambacho kila mwanadamu anakitumia kama siyo maji. Kuna vitu vingi vizuri, vitamu duniani lakini wanadamu hawavitumii, lakini kila mmoja anatumia maji. Kwa hiyo, tutakapokwenda kuhakikisha kwamba tunatoa huduma za maji kwenye vijiji vyetu, tutahakikisha kwamba wananchi sasa tunawajengea uchumi ambao wanastahili kuwa nao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, moyo usiokuwa na shukrani hukausha mema mengi. Kwa hiyo, napenda kuishukuru Serikali ya Awamu ya Tano kwa kutuletea mradi wa maji mkubwa katika mji wetu mkubwa wa Magu. Kwa hiyo, Mji wa Magu umepata maji, lakini maji yale ni mengi mno ambayo yanastahili kuhudumia vijiji 32 vyenye takribani wakazi 180,000. Maombi haya tumeshayaleta ili angalau haya maji yaweze kuwafikia wananchi wa Jimbo la Magu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, katika vijiji hivyo 32, kuna Kijiji cha Mahaha ambacho kina wakazi wengi sana; Shishan, Isolo, Kabale pamoja na vijiji vingine; Kungulu, Ndagalu, Salama, Mobulenga, Nyashoshi, Kuhumbi, Misungwi, Sagani, Mwalina, Mwamabanza, Watelesha, Mwamibanga, Iseni, Bugabu, Chandulu, Vijinjibili pamoja na Nyahanga. Ni vijiji 32 vyenye wakazi 182,000. Vijiji hivi vikipata maji tutakuwa tumewakomboa sana wananchi wa vijiji hivyo na hasa akina mama ambao wanaamka usiku wa manane kwenda kuchota maji. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, unajua wazalishaji wengi wa uchumi kule vijijini ni akina mama, lakini muda wote wanaumaliza kutafuta maji. Anaamka saa nane anakwenda kwenye maji, anarudi saa tano, hana muda hata wa kwenda kwenye mashamba kwa ajili ya kuzalisha kwenye kilimo. Kwa hiyo, naiomba sana Wizara ya Maji, kwa sababu Mheshimiwa Awesso ameshafika Magu pamoja na Sanga, waone namna ambavyo wanaweza kutusaidia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mradi huu kulikuwa na upungufu wa kilometa 24 katika Mji wa Magu pale na ninaamini Rais wetu mpendwa, hivi karibuni atakuja kuufungua huu mradi wa maji. Sasa hizo kilometa 24 zilikuwa zinahitaji shilingi milioni 260. Wakati huo Awesso akiwa Naibu Waziri na Sanga akiwa Naibu Katibu Mkuu, wote wamepandishwa kuwa Waziri na Katibu Mkuu, hebu mwelekeze shilingi milioni 260 ili kilometa 24 katika Mji wa Magu wananchi waweze kupatiwa maji. Kwa sababu, akija kufungua Rais, halafu wananchi wakanyoosha mabango, sasa sijui atafukuzwa Mkurugenzi au DC au atafukuzwa Waziri au Katibu Mkuu? Nami nataka Waziri na Katibu Mkuu mwendelee kuwepo kwenye Wizara hii. Hebu angalieni namna ambavyo mnaweza kusaidia ili wananchi wasiinue mabango. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tuna Mji wa Kisesa pale ambao chanzo chake ni Butimba. Chanzo hiki ni cha muda mrefu na tayari mkandarasi ameshapitishwa. Tatizo kubwa ni exemption ili aweze kutoa vifaa vyake bandarini. Hebu tuliangalie suala hili la exemption kwa sababu ni suala ambalo linakwamisha sana kuendeleza miradi ambayo iko tayari na fedha ziko tayari. Mradi huu utahudumia katika Mji wote wa Rwanyima, Nyamagana kwa ujumla, Buswelu pamoja na Kisesa, Usagara. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba sana kwa sababu mradi huu ndiyo utakaokwenda kutatua changamoto nyingi katika Mji wa Kisesa ukiwa na Kata ya Bujola, ukiwa na Kata ya Bukandwe, ukiwa na Kata ya Bujashi. Kwa hiyo, haya ni maeneo muhimu sana ya kiuchumi na tunaamini kwamba maji yakifika na kwa sababu Mheshimiwa Hayati Rais Dkt. John Pombe Magufuli alitaja Kisesa kwamba iwe Makao Makuu ya Wilaya mpya ya Kisesa, kwa hiyo, maji haya ni muhimu sana, yanasubiriwa na wananchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, haya ni maeneo muhimu sana ya kiuchumi. Tunaamini kwamba maji yakifika, kwa sababu hayati Rais Dkt. John Pombe Magufuli alitaja Kisesa kwamba iwe Makao Makuu ya Wilaya Mpya ya Kisesa. Kwa hiyo, maji haya ni muhimu sana, yanasubiriwa na wananchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, tulikuwa na miradi inayozunguka Ziwa Viktoria vijiji 16. Wataalam wa Wizara ya Maji walifika na tayari upembuzi yakinifu umekwishafanyika. Tulikuwa na matarajio kwamba mradi huu ungekuwa umeanza bajeti hii ya fedha tunayoendelea nayo, lakini mradi huu haujaanza. Vijiji hivi viko kabisa kwenye maeneo ambayo Ziwa Victoria linapita pale. Vijiji hivi ni Shinembo, Bundilya, Nyamhanga, Inolelo, Mwamanga, Kigangama, Lutale, Kayenze, Kageye, Itandula, Rangi, Matale, Ihushi, Sese na Busekwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, wakati Mheshimiwa Waziri anakuja ku-wind up hapa atueleze kwa sababu ni ahadi ya wananchi kwamba tutakwenda kutatua kero za maji na kumaliza kabisa ili wananchi waweze kupata huduma ya maji safi ili angalau wananchi wawe na matumaini ya kutosha kwa Serikali yao.
Mheshimiwa Naibu Spika, niunge mkono hoja kwa sababu namwamini Waziri pamoja na Naibu na Katibu Mkuu Wizara ya Maji. Ahsante sana. (Makofi)