Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maji

Hon. Abeid Ighondo Ramadhani

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Singida Kaskazini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maji

MHE. ABEID R. IGHONDO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipatia fursa hii angalau niseme mawili matatu kwenye mjadala huu wa Wizara hii ya Maji. Awali ya yote, kutokana na muda naomba nitambue kazi nzuri inayofanywa na watendaji pamoja na Mawaziri wa Wizara hii. Kwa mantiki hiyo, niishukuru Serikali kwa miradi mikubwa ya maji ambayo imekwishakamilika na inatoa maji hivi sasa kwa upanuzi mkubwa wa njia za maji pamoja na miundombinu katika Kijiji cha Halunyangu, Kijota, Mgori, Mangida, Mughamu pamoja na Msisi. Miradi hii kwa kiwango kikubwa imeondoa adha kwa wananchi ambao walikuwa wanapata tabu kweli kweli wanapohitaji huduma ya maji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika bajeti hii nashukuru na naipongeza Serikali kwa kutupatia fedha kwa ajili ya miradi mikubwa minne ya maji. Kijiji cha Mwighanji, Mitula, Migugu na Ughandibe. Hatua hii ni nzuri sana na naomba sana Serikali ihakikishe miradi hii inakamilika kwa wakati kama ambavyo imepangwa. Kwa mazingira hayo, naomba sasa DDCA, ambao ni Wakala wa Uchimbaji Visima vya Serikali wafike mara moja kwa ajili ya kuanza kazi ili wananchi wetu waondokane na adha ya kupata taabu ya maji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia nitambue pia mchango wa wadau, taasisi binafsi kwenye upatikanaji wa maji katika Jimbo la Singida Kaskazini. Naomba nitambue Shirika la Rehema Foundation, Silver Crescent ya kutoka Nchini Uturuki ambao kwa kushirikiana na Mbunge tangu aanze kazi miezi sita sasa amefanikiwa kukarabati visima 23 ambavyo vilikuwa vimekufa kabisa lakini na kuchimba visima virefu vinne katika Kijiji cha Kinyamwenda, Makuro, Maghandi na Itamka.

Mheshimiwa Naibu Spika, ombi kubwa katika hili, visima vile vinatoa maji ya kutosha kuanzia lita 10,000 kwa saa moja. Ni ombi kwamba maji haya yasambazwe. Naiomba Wizara kwa kushirikiana na RUWASA, maji hayo yasambazwe ili yawafikie wananchi wengi kwenye vijiji vingi badala ya kubaki pia yanatolewa kwenye centre tu ile pale kilipo kisima.

Mheshimiwa Naibu Spika, changamoto kubwa sasa ambayo naiona kwenye miradi mingi ya maji, Singida Kaskazini pamoja na maeneo mengine ni suala la ufuatiliaji. Ufuatiliaji ni tatizo kubwa sana. Unakuta kisima kimetengenezwa leo kinakaa miaka 20 hakijawahi hata kutembelewa siku moja kuangaliwa changamoto zake. Kwa hiyo, visima vingi vimekufa. Mathalani, visima hivi 23 ambavyo mimi Mbunge kwa kushirikiana na wadau tumevikarabati, vilichimbwa mwaka 1980 na Shirika la TCRS. Kwa hiyo, niombe sasa Wizara ya Maji wawe na tabia ya kufuatilia miradi, ku-cross checkā€¦

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. ABEID R. IGHONDO: Lah! Naunga mkono hoja ingawa bado nilikuwa na mengi ya kusema hapa. (Makofi)