Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Temeke
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. ABDALLAH A. MTOLEA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kukupa uwezo wa kunipa nafasi ya mimi kuchangia bajeti ya Wizara hii ya Viwanda na Biashara kwa niaba ya wananchi wa Temeke na kwa maslahi mapana ya Halmashauri ya Manispaa ya Temeke.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumekuwa tukimsikiliza hapa Mheshimiwa Waziri ni kwa namna gani anapenda kuiona Tanzania ambayo imesheheni uwekezaji katika sekta mbalimbali ili kuifanya nchi hii iwe ya kipato cha kati. Hili ni jambo zuri na kila mtu angependa siku moja kuiona Tanzania hiyo. Wakati pia tunajipanga kuwakaribisha wawekezaji kwa kiasi kikubwa, ni vizuri pia tukawa na mpango maalum wa kuona ni kwa namna gani tutawasimamia wawekezaji hao ili uwekezaji wao uwe na tija kwa Taifa hili na kwa wananchi wa Taifa hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mifano michache ya wawekezaji ambao sasa hivi wapo, inatutia mashaka kweli kweli. Haioneshi kama uwekezaji wao una tija na malengo mazuri kwa Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pale Jimboni kwangu Temeke, eneo la viwanda Chang‟ombe lina wawekezaji wengi, lakini kwa masikitiko makubwa yamekuwa ni maeneo ya mateso kwa Watanzania, maeneo ya mateso kwa wananchi wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wetu wananyanyaswa kwa kiasi kikubwa sana katika viwanda na makampuni hayo, kwa kulipwa mishahara midogo sana, kufanyishwa kazi ngumu kwa masaa mengi, hawana vitendea kazi; unamkuta mtu katika kiwanda pengine cha kuyeyushia chuma hana vifaa vya kufanyia kazi. Yupo tumbo wazi, mikono mitupu, hana mask, anafanya kazi kwenye moto mkubwa kiasi hicho. Wawekezaji wanawaambia kabisa, kama hutaki kazi acha, kuna wenzio 300 mpaka 400 wanasubiri hiyo kazi yako. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, inapofikia mahali wawekezaji wanawanyanyasa wananchi kwa sababu tu kuna tatizo kubwa la ajira, ni lazima tufikirie mara mbili, ni namna gani tujipange tuweze kuufanya uwekezaji huu uwe na tija kwa wananchi wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo hivyo tu, tungependa tuwe na wawekezaji wenye masikio yanayosikia wawekeze kwa kufuata sheria na taratibu za nchi hii. Hapo hapo Chang‟ombe, kuna wawekezaji wamejenga viwanda na ma-godown yao juu ya mifereji ya kutiririsha maji machafu. Yaani wanaziba miundombinu ya kutolea maji mitaani kwa maana ya uwekezaji. Unajiuliza, ni kweli tunasimamia huu uwekezaji? Kwa hiyo, kuna wananchi pale Chang‟ombe kwa muda wa miaka 12 sasa, kila ikinyesha mvua kwao ni mafuriko, kwa sababu tu kuna watu wamejenga magodauni yao na viwanda vyao, wameziba mifereji ya maji na hakuna mtu wa kuwaambia kwamba hili mnalolifanya ni kosa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mbaya zaidi, wanatiririsha maji ya kutoka viwandani yanaingia mitaani unajiuliza hawa wanaoitwa NEMC wako wapi? Wanaandikiwa barua, wanapigiwa simu, hakuna kitu wanachokifanya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni vizuri Mheshimiwa Waziri akafahamu kwamba Taasisi zinazomzunguka zina mchango mkubwa sana wa kuzifanya ndoto za kuifanya Tanzania kuwa nchi ya kipato cha kati, zitimie au zifeli. Ni vizuri akaziangalia tena upya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Kata ya Sandali ambayo nayo ipo katika Jimbo hili hili la Temeke, ambayo inapakana na viwanda vya Vingunguti vilivyoko katika Jimbo la Segerea, kuna mfereji unaotiririsha maji ya sumu yanayonuka vibaya na yanayoathiri mazingira kuanzia Januari mpaka Desemba. Wananchi wa Mitaa ya Mamboleo „A‟, Mamboleo „B‟, Kisiwani, Usalama wakijenga nyumba ukaezeka bati leo, baada ya miezi sita, zile bati zinakuwa zimetoboka zote na ukizigusa zile kuta za nyumba, yale matofali yanamong‟onyoka. Sasa jiulize, afya za wananchi wa hapo zikoje? Kama mabati yanatoboka hivyo, afya za wananchi zikoje? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni vizuri Mheshimiwa Waziri akimaliza bajeti yake hapa, afanye utaratibu afike Temeke ajionee. Twende nikakuoneshe yanayofanyika, uone wananchi wanavyoteseka na uwekezaji ambao tunautaka uingie sasa hivi. Upite na kwenye ma-godown uone. Kwa mfano, kwenye viwanda labda vinavyotengeneza unga, wakisikia watu wa TBS wanakuja, siku hiyo utatengenezwa unga maalum kwa ajili ya kuwaonesha TBS, lakini siyo ule unaotengenezwa kila siku. Kwa hiyo, kumbe hata afya zetu kwenye hizi bidhaa zinazozalishwa, ni matatizo (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile kuna raia wengi wa kigeni wasiokuwa na documents za kukaa hapa nchini, wamefungiwa kwenye hayo ma-godown wanafanya kazi ambazo Watanzania wangezifanya. Kwa hiyo, kuna miradi mikubwa ya watu, kuwaficha watu, kuwatumikisha wakidhulumu nafasi za Watanzania. Lazima tuyatoe haya, ndiyo uwekezaji utakuwa na tija. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuna hawa watu wa viwanja vya biashara vya Saba Saba na uwanja wa Mpira wa Taifa; uwanja mkubwa wa Taifa na Uwanja wa Uhuru; hawa watu hawalipi kodi. Hawalipi malipo wanayostahili kuilipa Halmashauri ya Temeke. Hawalipi property tax wala service levy.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili Halmashauri iweze kutekeleza majukumu yake ya kuboresha huduma za kijamii ni lazima ikusanye kodi. Unapokuwa na wawekezaji au watu wanaofanya biashara ambao hawakulipi, unakuwa ni mzigo mkubwa. Naomba Mheshimiwa Waziri kwa nafasi yake, aongee na hawa watu wa Saba Saba na Uwanja wa Taifa. Tumewapelekea invoice kwa muda mrefu na hawajalipa. Sasa akawaambie nitawajazia watu siku siyo nyingi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitawakusanya wananchi wa Temeke twende tukazuie kufanya biashara zao, twende tukazuie mechi zisichezwe Uwanja wa Taifa. Najua tutapigwa sana mabomu, lakini I am very proud kwamba watu wa Temeke wakilitaka lao, hawaogopi mabomu. Kwa hiyo, tutayafanya hayo endapo wataendelea kukaidi kutulipa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunatumia fedha za Halmashauri kusafisha yale mazingira baada ya mechi kuchezwa, baada ya maonesho ya Saba Saba; kwa nini tutumie fedha yetu na wao hawataki kuchangia? Hatuhitaji uwekezaji wa namna hiyo. Kwa hiyo, wafikishie taarifa, waambie kwamba tutakuja tuyafanye hayo. Tutazuia moja kati ya maonesho Uwanja wa Saba Saba, lakini tutazuia moja ya mechi Uwanja wa Taifa nao waione hasara. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba sana Mheshimiwa Waziri, wakati wengine wanahitaji viwanda, sisi Temeke tunahitaji masoko. Tuna viwanja vikubwa vya kujenga masoko kwenye kila Kata na wafanya biashara wako tayari kufanya biashara katika masoko hayo. Tuletewe wawekezaji watujengee masoko ya kisasa na fedha yao itarudi haraka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, waambie NSSF waache kujenga madaraja, waje wawekeze kwenye masoko, fedha yao itarudi haraka sana. Waambe National Housing waache kwenda kujenga majumba maporini wanahangaika kutafuta wapangaji, waje kuwekeza sokoni.
MHE. ABDALLAH A. MTOLEA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru.