Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Busega
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. SIMON S. LUSENGEKILE: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru kwa kunipa nafasi na mimi kuchangia Wizara ya Maji. Kipekee sana nimpongeze sana rafiki yangu Mheshimiwa Aweso kwa kazi kubwa anayofanya pamoja na Naibu Waziri na Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji. Wanafanya kazi kubwa, tunaona kazi zao wanazofanya, kweli zimekuwa ni kazi za msingi. Niwaambie tu kwamba wananchi hasa wananchi wa Busega wana imani kubwa nao kwa sababu wameona mageuzi makubwa ambayo wameyafanya kwenye Wizara ya Maji kwa huo muda mfupi ambao wamekuwa kwenye madaraka.
Mheshimiwa Naibu Spika, mageuze hayo ni Pamoja na namna ambayo wamefanya kuhakikisha kwamba wanapunguza gharama za ujenzi wa miundombinu ya maji, kwa sababu tumeona kuna sehemu zingine ambazo wameenda, gharama zimeshuka, unakuta BOQ ilikuwa bilioni mbili lakini kwa sababu wamenda pale mmefanya revision ya budget zimeshuka mpaka kufikia hata bilioni 1.6. Haya ni mageuzi makubwa sana ya kimkakati ambayo wameamua kuyafanya kwenye Wizara yenu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kipekee pia nimshukuru sana Waziri Mkuu, Mheshimiwa Kassim Majaliwa alipokuja pale kwangu Mkura aliahidi kutupatia mradi wa maji na sasa mradi tayari umeshaanza kazi, tayari wakandarasi wako pale wanafanya kazi. Kwa kweli, tunawapongeza sana na muda ujao naamini kwamba mradi huu utaanza kutoa maji. Nimwombe tu rafiki yangu Waziri, bado kuna shida ya fedha pale. Naomba apeleke fedha ili mradi ule ukamilike kwa wakati na naamini kabisa kwamba Mheshimiwa Waziri ni msikivu na kwa sababu ni kijana na kwa sababu Wasukuma ni wakarimu aende pale akaangalie namna mradi unavyotekelezwa ili umalizike kwa haraka sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia nizungumze suala moja ambalo limekuwa likinipa shida kidogo. Kuna baadhi ya miradi ambayo inaenda kutelekezwa kwenye kata, lakini unakuta kata moja ina vijiji vine, lakini mradi unakuwa wa vijiji vitatu, kijiji kimoja kinabaki. Hili limekuwa ni tatizo na niishauri Wizara, kama wameamua kupeleka mradi kwenye kata, basi ni nzuri kata nzima kumaliza vijiji vyake vyote ili kisibaki kijiji na ikaonekana kama wametengwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, nina mfano, kwenye Kata ya Kiloleli yenye vijiji vinne, Kijiji kimoja kimeachwa, Kijiji cha Ilumya, lakini kwenye Kata ya Mwamanyili, Kijiji kimoja cha Milambe ambako Mbunge anatoka kimeachwa. Kwenye Kata ya Mkura, Vijiji viwili kwa maana ya Mwang’ale na Chabutwa vimeachwa. Kwa hiyo, nafikiri kwamba tunapokuwa tunafanya designing ya mradi kwenye kata husika basi ni vizuri kata nzima iweze kuchukuliwa na vijiji vyote viweze kupata maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia nimefurahishwa sana na namna ambavyo wameanza kuleta mkakati wa mradi mkubwa wa maji wa Ziwa Viktoria kwenda Itilima ambao kwa awamu ya kwanza utaanza na Busega, utaenda Bariadi lakini pia utaenda Itilima. Mradi huu ni mradi mkubwa na ndiyo mradi pekee ambao uta-solve tatizo la maji kwa Wilaya ya Busega, Wilaya ya Bariadi na Wilaya ya Itilima.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimwombe Mheshimiwa Waziri, kwamba, moja ya mradi ambao unatakiwa macho ya Waziri yaende hapo ni huu mradi mkubwa sana, kwa sababu hii miradi mikubwa unapokuwa umemalizika ni mradi ambao utahudumia wananchi wengi. Pale kwangu Jimbo la Busega zaidi ya vijiji 42 vinaenda kupitiwa. Mradi huu kwa Mkoa wa Simiyu utapita kwenye vijiji 256.
Mheshimiwa Naibu Spika,naomba na nimeona Waziri tayari ameweka kwenye Mpango bilioni 19 kwa ajili ya kuanza kati ya bilioni 400. Nimwombe kwamba awekeze sehemu hii ili wananchi wengi, zaidi ya 200,000 wa Wilaya ya Busega waweze kupata maji kupitia mradi huu.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninavyokwambia sasa Wilaya ya Busega wananchi wanaopata maji safi na salama ni asilimia 52 wengine bado hawapati maji safi na salama na kijiji cha mwisho ni kijiji chenye kilometa 42, leo tunazungumza kuleta maji Dodoma zaidi ya kilometa 800 tunaomba na sisi utukumbuke kwenye kilometa 42 nao waweze kupata maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja asilimia mia moja. Mheshimiwa Aweso karibu Usukumani, karibu Busega. Ahsante. (Makofi)