Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maji

Hon. Hamis Mohamed Mwinjuma

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Muheza

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maji

MHE. HAMIS M. MWINJUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa fursa hii na mimi nisema mawili, matatu kwenye hoja iliyopo mezani. Nisije nikafika mwisho muda ukanibana ama nikajisahau niseme kwanza naunga mkono hoja. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote, nichukue fursa hii kuwapongeza watendaji wetu kwenye Wizara ya Maji; Ndugu yangu Waziri Jumaa Hamidu Aweso na Ma- engineer wake, dada Naibu Waziri Maryprisca Mahundi, Katibu Mkuu Eng. Sanga (Mzee wa Mnadara), dada yangu Nadhifa Kemikimba, Mkurugenzi wa Tanga (UWASA), Eng. Upendo Rugongo, Meneja wa Tanga (UWASA – MUHEZA) Eng. Nyambuka na Meneja wa RUWASA - Muheza Eng. Cleophate Maharangata, kusema kweli mnatutendea haki. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunajua matatizo ya maji nchi hii ni makubwa na pengine ndio tatizo kubwa kuliko yote hasa kwa Wabunge wanaotoka Majimbo ya vijijini kama mimi. Mimi natoka Wilaya ya Muheza ambapo kuna changamoto kwenye kila kitu; elimu, afya, barabara na kadhalika. Akitokea mwananchi mwenzangu yeyote wa Muheza hapa ukamuuliza tatizo la kwanza la Muheza ni nini, naamini atakutajia maji. Akina mama wa Muheza kuna mahali nilifika wakaniambia Mheshimiwa ukiweza kuhakikisha tunaweza kuchota maji kwenye mabomba ikifika mwaka 2025 lete shati lako lisimame hapa wewe ukapumzike na tutalipigia kura. Kwa hiyo, ndugu yangu Mheshimiwa Jumaa na wasaidizi wako nafikiri mnajua kama mpaka Ubunge wangu mmeushika kwenye mikono yenu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna kauli ya Kiswahili wanasema kwamba asiyeshukuru kwa kidogo hawezi kushukuru kwa kikubwa. Pamoja na tatizo kubwa la maji Wilaya ya Muheza kusema kweli watendaji hawa wanatusikiliza na wanapanga kuyatatua matatizo haya kwa moyo wao wote. Unaona hata maana ambapo hawawezi kulifanya kwa asilimia 100 lakini ndimi zao zinakuwa laini na unaona unawahangaisha katika kutafuta suluhisho ya matatizo yale. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sisi Muheza tuna Mradi wa Kilongo ambao umetengewa kiasi cha shilingi milioni 778, tuna mradi wa Kwemdimu una shilingi milioni 649; mradi wa Kwemnyefu, Mdogo, Pongwe una shilingi bilioni 6.1 na ule mradi mkubwa kabisa ambao tunaamini unakwenda sasa kutatua tatizo zima la maji Wilaya ya Muheza wa miji 28 ambao sisi tumetengewa bilioni 40. Tunafahamu mioyo yenu ni mizuri na tunafahamu tatizo liko wapi, ni fedha.

Mheshimiwa Naibu Spika, niliombe Bunge lako Tukufu kama kuna kitu ambacho tunatakiwa kufanya kama Wabunge ni kuhakikisha Wizara ya Maji inapewa fedha zote ambazo tumekubaliana hapa. Kwa miaka 10 mfululizo ikiwemo bajeti yao ya mwaka huu wa fedha unaokwisha wamekuwa hawapewa hata asilimia 60 ya fedha ambazo wanaziomba, kKwa mfano, bajeti ya mwaka huu wa fedha wamepata asilimia 54 tu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa ufahamu wangu, tunapoamua kwamba tunatenga fedha kwa ajli ya kwenda kutekeleza miradi ya maji tunakuwa tumeamua kwamba kuna asilimia fulani ya matatizo ya maji ya nchi hii tunakwenda kuyatatua siyo yote. Kwa hiyo, kama tumeamua kwamba tunatenga fedha na zinakwenda kutatua asilimia 20 ya matatizo ya maji katika nchi hii tunapowapa asilimia 50 maana yake tunakwenda kutatua asilimia 50 ya asilimia 20 ambayo tulipanga, tunazidi kujirudisha nyuma.

Mheshimiwa Naibu Spika, Waheshimiwa Wabunge tumeingia kwenye Bunge hili hasa Wabunge wa Vijijini kama mimi tukijua kwamba tatizo kubwa ni maji na kama hatutaikomalia Serikali iwe inatoa fedha zote ambazo zimeombwa na Wizara ya Maji ambazo zimepangwa kutekeleza miradi hii tutatoka hapa matatizo yale hayajakwisha. Sidhani kama hiyo ndiyo namna tunataka kukumbukwa, tumeingia tumekuta tatizo la maji, tutoke tuliache tatizo la maji. Naomba tulikomalie au kwa lugha ya mtaani tunasema kidedea Wabunge wote na ukiwemo Naibu Spika kuhakikisha kwamba Wizara ya Maji inapata sehemu kubwa ya fedha ilizoomba ili miradi hii ya maji iweze kutekelezwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nondo zilikuwa nyingi lakini nashukuru, naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)