Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa mwaka wa Fedha 2016/2017

Hon. Kabwe Zuberi Ruyagwa Zitto

Sex

Male

Party

ACT

Constituent

Kigoma Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. KABWE Z. R. ZITTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia bajeti ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji na nina maeneo machache kama matatu au manne hivi kama muda utakuwa umeniruhusu ili niweze kuchangia uboreshaji wa hotuba hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza katika Hotuba ya Msemaji wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Mheshimwa Komu, amezungumzia suala zima la discrepancy iliyopo kati ya vitabu vya Wizara, vitabu vya Wizara ya Fedha, kwa maana ya kitabu Na. 4 cha maendeleo na randama ya Wizara ya Viwanda na Biashara kuhusiana na mradi wa General Tyre, ambapo mpango wa maendeleo unasema fedha zitakazotengwa ni shilingi bilioni mbili, randama ya Viwanda na Biashara inasema fedha ni shilingi milioni 500 na kitabu cha bajeti ya maendeleo kinasema shilingi milioni 150.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niikumbushie hoja hii kwa sababu nadhani ni hoja muhimu sana ili tuweze kufahamu tunapopitisha bajeti hii ni nini hasa tunachokipitisha. Kwa sababu ni vyema tukajua ni shilingi milioni 150 itakayopitishwa na Bunge, ni shilingi bilioni mbili ambayo ipo kwenye Mpango wa Maendeleo kwa ajili ya General tyre au ni shilingi milioni 500 iliyoko kwenye randama ya vitabu vya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, nami nataka kurejea kauli ambayo Wabunge wenzangu Wamezungumza kwamba tunataka kujenga viwanda gani, kwa sababu ni lazima tuwe na focus na tuweze kuhakikisha kwamba tunaendana na ile focus ambayo tumeiweka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nilipokuwa napitia hotuba ya Waziri, nimeona katika Ibara ya 191 ya hotuba yake, anazungumzia malengo ya mwaka 2016/2017. Katika haya malengo yote, sioni lengo ambalo linaelekeza nchi yetu kwenda kuzalisha bidhaa ambazo wananchi wengi wanazitumia na hapa nazungumzia sukari, mafuta ya kula na nguo. Hizi ni bidhaa ambazo wananchi wanazitumia kila siku. Hata hivyo, katika malengo tisa ya mwaka wa 2016/2017 ya bajeti ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, sioni jambo hilo. Sasa nashindwa kuelewa, Wizara haioni kwamba kuna tatizo katika maeneo hayo na kwamba tuna haja ya kufanyia kazi jambo hili?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kinachonisikitisha zaidi ni kwamba kuna tatizo la Wizara kutokusomana; yaani Wizara ya Kilimo inachokisema, hukioni kwenye Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji. Viwanda vyetu sisi kimsingi vinategemea sana malighafi za kilimo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hapa nina hotuba mbili, nina hotuba ya Wizara ya Kilimo na nina hotuba ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji. Katika hotuba ya Wizara ya Viwanda na Biashara, sukari siyo priority kabisa. Haitajwi kabisa! Katika hotuba ya Wizara ya Kilimo ukurasa wa 25, 44 na 63, anazungumzia mikakati ya kuondokana na tatizo la uhaba wa sukari. Mpaka kwenye kiambatanisho namba sita cha hotuba ya Wizara ya Kilimo, kuna mikakati na miradi mingi na mpaka mradi wa Mheshimiwa Kawambwa ambao ameuzungumzia leo wa Bagamoyo na changamoto zake, imeelezwa. Hiki unachokisoma huku, haukisomi Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa napenda kujua, Mheshimiwa Kaimu Waziri Mkuu yuko hapo, cabinet haikukaa kuweza kuwianisha Kilimo na Viwanda? Kwa sababu Waziri wa Kilimo akilima miwa, haiwezi kuwa sukari bila viwanda. Ukiangalia humu, miradi ambayo imeainishwa kwenye Wizara ya Kilimo, ni miradi ambayo inaweza kuzalisha tani milioni moja na nusu za sukari. Maana yake ni kwamba tutaweza kutumia ndani na kuuza nje na kwa bei ya sukari ya jana, tunaweza tukauza mpaka Dola za Kimarekani milioni 500 kulingana na miradi ambayo iko humu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini hiyo miradi ambayo ipo humu, huioni kwenye viwanda. Tunasema kwamba sisi tunachokitaka ni kuanza na bidhaa za kilimo ili wananchi wetu wapate ajira tuongeze thamani na kadhalika na nadharia za uchumi zinaonesha hivyo.
Sasa Waheshimiwa Wabunge wenzangu, naomba tukubaliane kitu kimoja ambacho kimo ndani ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, hata tukimpitishia Waziri fedha zake zote sasa hivi, tutarudi mwakani, sifuri. Kwa sababu hakuna tutakachoweza kuki-solve. Iwapo Wizara ya Kilimo na Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, wakioanisha mipango yao, ndani ya miaka mitatu hatuna shida ya sukari tena nchini. Wala hatutamwangaisha tena Mheshimiwa Rais kutembea barabarani anatoa amri kuhusu sukari.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais anatoa amri kuhusu sukari kwa sababu Mawaziri hawafanyi kazi yao. Kwa sababu matamko ambayo Mheshimiwa Rais anayazungumza kuhusu sukari, ni matamko ambayo yalipaswa kuzungumzwa na Mawaziri. Kama kungekuwa na coordination kati ya Wizara ya Kilimo na Wizara ya Viwanda na Biashara wala tusingekuwa na shida leo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nawaomba Waheshimiwa Wabunge, kwa mujibu wa ibara ya 69 ya Kanuni zetu za Bunge, Mbunge anayependa mjadala unaoendelea juu ya hoja yoyote uahirishwe hadi wakati wa baadaye, anaweza kutoa hoja kwamba mjadala sasa uahirishwe na atataja mjadala huo uahirishwe hadi wakati gani na pia atalazimika kutoa sababu, kwa nini anataka mjadala huo uahirishwe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachokiomba Waheshimiwa Wabunge na hapa tuwe beyond party politics, yaani tuwe zaidi ya Vyama vyetu. Nawaomba tuiombe Wizara ya Kilimo na Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji ziende zikakae, wafanye marekebisho ya Bajeti ya Viwanda na Biashara, halafu ndiyo baadaye turudi, kujadili suala zima la Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji. Vinginevyo hapa tunakuwa tumecheza. Bahati mbaya sana, tumeshapitisha Wizara ya Kilimo. Ilitakiwa zote mbili hizi, tusizipitishe kwanza, wakae, wazungumze watuletee program. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nawaomba Waheshimiwa Wabunge kwa mujibu wa Kanuni ya 69 ya Bunge, mjadala huu wa Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji uahirishwe. Hulikuti jambo hili kwenye sukari peke yake, unalikuta kwenye nguo, Wizara ya Kilimo inazungumzia pamba, lakini uzalishaji wa pamba umeporomoka kwa asilimia 47. Wizara ya Viwanda inasema itaimarisha viwanda vya nguo, utatoa wapi pamba ya kuingiza kwenye viwanda vya nguo. Pamba imeshuka by six and seven percent. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji haijazungumza kabisa suala la bidhaa ya mafuta ya kula. Leo hii ukitembea unakwenda Singida, unawakuta wananchi wetu wanapigwa na jua barabarani wanauza mafuta kwenye madumu. Mafuta ya alizeti leo bei yake ni kubwa kuliko bei ya petroli katika Soko la Dunia, lakini hamna mpango, hakuna links kati ya kilimo na viwanda.
Kama tunataka tuzungumze kuwafurahisha wananchi kwamba tunakwenda kwenye uchumi wa viwanda tuendelee kupitisha hii bajeti. Kama tunataka angalau Bunge hili lifanye value addition katika kazi ambayo Serikali inafanya, tuombe hawa ndugu zetu watoke, Wizara ya Kilimo na Wizara ya Viwanda waende wakakae wawianishe mipango yao watuletee tuweze kupitisha. Tukipitisha hivi hivi, hatutaweza kufanya chochote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba nitoe hoja kwamba mjadala wa Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji uahirishwe ili Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji na Wizara ya Kilimo waende wakakae waweze kuwianisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho kabisa, viwanda vinahitaji vivutio. Nitatoa hoja mwishoni. Kuna umuhimu mkubwa sana, maana yake nasikia sasa hivi kuna mvutano kati ya Wizara ya Fedha na Wizara ya Viwanda kwa ajili ya kutoa vivutio kwenye viwanda vya kimkakati. Sasa Mheshimiwa Rais yuko barabarani, anapiga kelele kuhusu sukari; mwekezaji anataka kujenga kiwanda cha sukari; mnatakiwa mkubaliane mtoe vivutuo kiwanda kile kiweze kujengwa, Wizara ya Fedha inakataa. Maana yake nini? Kwa hiyo, Mheshimiwa Rais analaghai wananchi? Haiwezekani! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ndiyo maana nasema kuna haja kubwa sana hawa watu wakakae tena. Naomba nitoe hoja kwa mujibu wa Kanuni ya 69, kwamba Bunge hili liahirishe shughuli za Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji mpaka hapo watakapoainisha mipango ya kilimo na mipango ya viwanda na biashara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nitoe hoja na naomba mniunge mkono Waheshimiwa Wabunge.