Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto

Hon. Noah Lemburis Saputi Mollel

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Arumeru-Magharibi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto

MHE. NOAH L. S. MOLLEL: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia katika Wizara hii ya Afya…

NAIBU SPIKA: Kila Mbunge anayeitwa anachangia kwa dakika tano.

MHE. NOAH L. S. MOLLEL: Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru pia Mwenyezi Mungu mwingi wa Rehema aliyenipa fursa hii ya kusimama kwenye Bunge lako hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakwenda moja kwa moja kwenye suala la ukosefu wa dawa kwenye hospitali zetu. Suala hili limekuwa ni tatizo kubwa. tunajua Serikali imejitahidi sana kwenye masuala ya miundombinu, lakini bado tuna changamoto sana kwenye suala la ukosefu wa dawa. Akina mama wanateseka na watoto, wazee wanateseka. Nilikuwa naomba suala ambalo litamfanya Waziri wa Afya na timu yake nzima wasipate usingizi, wasilale usiku, ni suala la ukosefu wa dawa katika hospitali zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kama ni suala la ukosefu wa dawa kwa sababu ya hujuma, labda wizi kwenye hospitali zetu, naomba hili suala kwa kweli; akina mama na watoto wanateseka, wazee wanakosa dawa na wagonjwa wengine wanakosa dawa hospitalini. Wale wanaoiba dawa hospitalini, basi mwaangalie na kuwaangazia macho sawa sawa kwa sababu katika jambo hili la ukosefu wa dawa kwenye hospitali, ni sawa sawa na kumsindikiza mgonjwa katika mauti.

Mheshimiwa Naibu Spika, mtu anapokwenda hospitali na akakosa dawa, matumaini ya kuishi duniani tena hakuna. Kwa hiyo, nawaomba sana suala hili tuliangalie kwa umakini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hayo, suala la ukosefu wa madaktari, hili nalo ni changamoto kubwa. Watu wanapokwenda kwenye hospitali wanakosa madaktari, hii bado ni changamoto kubwa mno. Naomba Serikali kwa sababu imetangaza ajira hizo, iendelee kuongeza kasi kubwa kuhakikisha kwamba tunapata madaktari wa kutosha na manesi wa kutosha kwenye hospitali zetu ili kuokoa akina mama wajawazito na watoto na wazee. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la wazee kupewa barua ya kwenda kupata dawa kwenye Dirisha la Wazee bado na yenyewe ni changamoto. Wazee hao wanateseka, hakuna dawa. Nilikuwa naomba Serikali iangalie hiyo Sera ya Wazee na yenyewe kwa sababu bado kuna changamoto kubwa, wale wazee wanateseka. Ni vizuri wakaja na mpango mahususi wa kuhakikisha kwamba wazee hawa badala ya kupewa barua kwa Mtendaji wa Kata na Mtendaji wa Kijiji, ni bora wapewe Bima ya Afya, hata kama ni hii iliyoboreshwa, nao wapate iwe ni sehemu ya kuweza kuhakikisha kwamba wazee hawa wanaangaliwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kweli, tuko hapa lakini tunapata matatizo makubwa kwenye majimbo yetu kwamba wananchi wanalia dawa hakuna, wazee wanateseka, watoto wanateseka, akina mama wanateseka, wajawazito na wagonjwa wengine.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kweli, naomba sana, sana sana Serikali yetu Sikivu ya Chama cha Mapinduzi, katika kutekeleza Ilani ya Chama cha Mapinduzi chonde chonde; na Mheshimiwa Mama Samia Suluhu Hassan alipokuja hapa Bungeni alituambia yeye ni mama, kwa hiyo, machungu ya mama anayajua vizuri. Kwa hiyo, naendelea kuiomba Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mheshimiwa Mama Samia Suluhu Hassan ijitahidi sana katika suala la dawa; na Mheshimiwa Waziri usilale usingizi kwa sababu, wamama hawana dawa.

Mheshimiwa Naibu Spika, hospitali kama tuna majengo halafu hatuna dawa ni sawa na hakuna hospitali, lakini tukiwa na dawa; hospitali ndiyo dawa. Kama tukiwa na majengo hata maghorofa, kama hakuna dawa, hospitali hakuna; na unafuu wa maisha haupo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nasema tena kwamba suala la motisha kwa madaktari na lenyewe ni jambo ambalo Serikali iliangalie kwa makini kwa sababu wale watu wanafanya kazi usiku na mchana, saa 24. Ni sawa na kazi ya jeshi. Wanajeshi wanafanya kazi usiku na mchana kama madaktari. Kwa hiyo, nawaomba pia suala la motisha kwa madaktari na manesi wetu ni suala la msingi na la muhimu sana ili waweze kuwa na moyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, bado narudia kusema, suala la wizi wa dawa, lazima Waziri asilale usingizi kwa sababu kukosekana kwa dawa ni tatizo kubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana na ninaunga mkono hoja. (Makofi)