Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto

Hon. Dr. Dorothy Onesphoro Gwajima

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Nominated

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto

WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuchukua fursa hii kuwashukuru Waheshimiwa Wabunge wote waliochangia kwa kuzungumza na kwa maandishi wakati wa uwasilishaji wa hotuba yangu.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kumshukuru sana Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii, Mheshimiwa Stanslaus Nyongo, Mbunge aliyewasilisha maoni na ushauri wa Kamati kuhusu utekelezaji wa maagizo ya kamati kwa mwaka 2020/2021 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara yangu kwa mwaka 2021/2022 na kuipongeza Wizara yangu, nasi tunamshukuru kwa kututia moyo. Pongezi hizo nimezipokea kwa niaba ya watumishi wetu wote wa sekta ya afya.

Mheshimiwa Naibu Spika, kabla ya kutoa majibu ya hoja mbalimbali za Waheshimiwa Wabunge, napenda niwatambue Waheshimiwa Wabunge 34 waliochangia jumla ya hoja 57 katika hotuba yangu ambapo Waheshimiwa Wabunge 29 wamechangia kwa kuzungumza na wengine wameendelea leo ambao tumewarekodi kama sita na Waheshimiwa Wabunge watano wamechangia kwa maandishi. Nina imani kwamba wengine bado wanaendelea na tutuzidi kuzipokea na tutazifanyia kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, naomba pia niwashukuru na kuwatambua waliochangia wakati wa hotuba ya Waziri Mkuu, Mheshimiwa Kassim Majaliwa, Mbunge ambao ni Waheshimiwa Wabunge 26 ambapo pia tumepokea michango yao na tutaifanyia kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, naomba niwashukuru sana Manaibu Waziri wangu wote wawili kwa michango yao mizuri waliyoitoa kujibu hoja hizi kama utangulizi, kabla sijaendelea sasa kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, hoja ni nyingi, nzuri zina tija, zina mashiko na zinafaa kufanyiwa kazi; na nyingi zinaweza kufanyiwa kazi vizuri kabisa pasipo hata kuwa na gharama kubwa sana, tukaweza kuleta mabadiliko. Wametufungua mawazo, wametutia moyo, nasi tunaahidi kwamba tumepokea. Mimi mwenyewe nilikaa hapa jana nikaandika sana, nina kila kitu, kama tutaweza kuwasilisha kwa maandishi wataona kwamba kila mmoja tumemtendea haki.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu michango ni mingi; na kwa sababu yote ni ya muhimu; na kwa sababu muda unaweze usitoshe naomba nijielekeze kwenye maeneo makubwa ambayo wengi sana yamewagusa, naamini hata ambao hawakuchangia kwa kuongea au kwa maandishi, itakuwa hizi zimewagusa.

Mheshimiwa Naibu Spika, haya ni masuala mazima ya dawa.nikimaliza hapo nitakwenda kwenye masuala ya upatikanaji wa watumishi; nikitoka hapo nitagusia masuala ya CAG na MSD kuhusu masuala ya Covid kupitia uzalishaji wa PPE, (Personal Protective Equipment), uliweza ukafanyika na ufafanuzi wake ni upi? Nitagusia kidogo kuhusu miradi ya ujenzi wa hospitali na tunahitaji na hospitali hizi zikamilike ili Muswada wa Sheria ya Bima ukute huduma zinapatikana. Muda ukiniruhusu nitakwenda kwenye maeneo mengine yote.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu suala la uhaba wa dawa, iliripotiwa kwamba kutoka kwenye hoja za Kamati. Hii imezalishwa na hoja za Kamati, lakini pia Waheshimiwa Wabunge waliochangia kwa mdomo nao wamesema. Kuhusu uhaba wa dawa nchini iliwasilishwa kwamba katika mwaka wa 2021kiasi cha shilingi bilioni 200 kilihidhinishwa na Bunge kwa ajili ya dawa lakini hadi kufikia Machi, 2021 ni asilimia 26 tu ya fedha hizo zilikuwa zimetolewa. Hivyo bajeti inayoidhinishwa na Bunge iwe inatolewa kikamilifu na kwa wakati.

Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara yangu inakiri kwamba mwaka huu 2020/2021 ilitenga hizo shilingi bilioni 200, ambazo ziliidhinishwa na Bunge lako Tukufu kwa ajili ya kugharamia masuala ya dawa na vifaa na vifaa tiba na vitendanishi. Kiasi cha fedha kilichotolewa mathalani sasa kufikia Aprili, 2021 kimeshabadilika, figure sasa inasoma shilingi bilioni 151.38 na kiasi kilichobaki kama cha shilingi bilioni 50 hivi, tayari tumeshaongea na Wizara ya Fedha, tutapatiwa mwishoni mwa mwezi huu Mei ili tukaendelee kununua dawa ambazo zilikuwa zimebakia. Kwa hiyo, Serikali itatimiza lengo lake. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara imepokea ushauri na maelekezo ya Kamati katika kuendelea kuimarisha utoaji wa huduma za kinga ambapo pia inahusiana na dawa zitakazohusiana na kudhibiti magonjwa mbalimbali eneo hili. Hata hivyo, hali ya upatikanaji dawa muhimu jana nilisema ilifikia asilimia 75, lakini ukweli ukiangalia, suala la upatikanaji wa bidhaa za afya siyo ajenda ya kuongeza bajeti kama nilivyosema. Kama tusipoangalia mambo mapana sana eneo hili hapa tutakuwa kila siku tukiongeza hii bajeti tunajikuta dawa zimekwisha.

Mheshimiwa Naibu Spika, tumefanya utafiti kwenye Halmashauri zote 184, tumefanya utafiti kwenye hospitali zetu 28 za mikoa, vile vile tumetumia uzoefu ukiwemo wangu mwenyewe nilipokuwa Singida ambapo tulifanya sana mambo haya ya dawa, tumeshirikiana na wadau wetu wote na wataalam wetu wote. Kwa pamoja tumesema lazima tujirekebishe na kujirekebisha huko kuna watu watachukuliwa hatua na wengine wameshachukuliwa, kama MSD, 24 wamefukuzwa kazi na wawili wameshushwa mishahara.

Mheshimiwa Naibu Spika, kule kwenye Halmashauri, katika Hospitali za Mkoa, taarifa tayari imeshakwenda kwenye vyomba vya sheria kwa ajili ya kuwachukulia hatua. Hii ni kwa sababu kuna uzembe mkubwa sana tena hapa ni wa hatari, nimeuambatisha kwenye kiambatisho changu cha hotuba niliyoiwasilisha jana.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tukishamalizana; yaani tunakwenda sambasamba kwamba waliokutwa na hizi hatia za kuwa wamefanya ubadhirifu, wamepoteza, wamedokoa, vyombo vya sheria tumeshawakibidhi taarifa, wanafanya kazi zao. Hawa ni PCCB, watajua wafanye nini. Vile vile mwajiri na waajiri wote wanaohusika, wanachukua hatua zao kwa sababu kuna Sheria za Ajira za Utumishi wa Umma dhidi ya mtu aliyebainika na hayo makosa.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia tumechukuwa dimension nyingine ya kwenda kwenye vyombo vya taaluma, yaani Mabaraza na Bodi; lazima tuulizane kwamba hivi unakuwaje mwanataaluma ambaye uzingatii taaluma yako? Wengi wanajitetea kwamba ni uchache wa watumishi, lakini tunakuta matatizo kama haya hata kwenye vituo vikubwa ambavyo watumishi mashallah, wana nafuu, lakini mtu unamwuliza maswali anashindwa kujitetea. Kwa hiyo, tunataka tushughulike na hili suala zima.

Mheshimiwa Naibu Spika, siyo hivyo tu, kuna dimension nyingine, lazima tuwekeze mazingira ya uwekezaji wa viwanda kuwa mazuri. Jana nilisema viwanda vimeongezeka nchini, sasa tunaongelea hesabu; vilikuwa tisa, sasa viko 11; 16 viko kwenye hatua ya ujenzi na 15 vinajengwa. Maana yake nini? Bei ya kununua hizi bidhaa za afya nje ya nchi sasa itakuwa ni ndogo kwa sababu tutakuwa tunanunua hapa ndani. Kwa hiyo, tunaweka mazingira rafiki na mwongozo uko tayari na ndiyo umetufikisha hapo ili hawa wanaowekeza wawekeze hapa nchini na hela yetu hii tunayosema ni ndogo tuitumie vizuri tupate mzigo mkubwa zaidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia tunaangalia dimension ya ajira kwa watumishi, wataalam wanaohusiana na dawa. Ni kweli utakuta kwenye zahanati au kwenye vituo vya afya watalaam wale ni wauguzi tu, hajasomea dawa. Wakati mwingine unaangalia kumbebesha hili tatizo. Kwa hiyo, kwenye ajira nitakazozisema hapa, tunaangalia Wafamasia pamoja na Wafamasia Wasaidizi tuweze kuwaongeza, tuwapeleke kwenye maeneo yale ambayo yana huduma kubwa zaidi ukilinganisha na yale madogo wataweza kuwafanyia supervision wale wa chini yao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, dimension ni nyingi, TEHAMA tumeshajitahidi. Tumefunga TEHAMA, nimeeleza kwenye hotuba yangu; tunataka tuziboreshe zaidi kiasi kwamba tukienda kwenye ule mfumo tuione dawa inaishia pale kwa mgonjwa yule. Pia tumeboresha prescriptions za dawa kwamba zinakuwa na leaf tatu; leaf ya kwanza, yaani stakabadhi moja, unapewa wewe mgonjwa uondoke nayo, stakabadhi moja anakaa nayo daktari aliyekuandikia, stakabadhi moja inakaa kwenye dirisha la dawa. Hiyo stakabadhi inakuwa na simu ya yule mgonjwa. Yule daktari tutamwuliza, wewe uliandika panadol ngapi mwezi huu mpaka kitabu hiki kimeisha chenye leaf labda 500.

Mheshimiwa Naibu Spika, hapa tutaona, tutaenda kufanya reconciliation na dirishani, tukitaka tutampigia mpaka mgonjwa tujue. Sasa tutashangaa kama daktari ameandika makopo 20, lakini wagonjwa aliowaona ni wagonjwa wanaoweza wakatumia makopo mawili au kopo moja. Mifumo hii midogo midogo iliachwa, leo hii ukienda pale mtu anapewa dawa tu kama njugu hapewi ile risiti na akipewa haendi nayo nyumbani; lakini benki ukienda unaweka hela zako wewe mwenyewe, unapewa na risiti upeleke nyumbani kwenu ushahidi. Tunataka tuurudishe ule mfumo wa control and cheques ili tuanze kulinda hizi rasilimali zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, dimension nyingine ambayo ningependa kuiongelea hapa, suala la kununua dawa, tunaratibu utekelezaji wa mwongozo wa cost sharing; yaani ni kwamba zamani tulikuwa na mwongozo lakini sasa hivi tumeuboresha. Ni kwamba utakuwa ukinunua hizi dawa, tunawezesha ile revolving yake iweze kuonekana. Zamani tulikuwa tunasema asilimia 67 tunazoweza kuzitumia kwenye eneo la dawa, lakini watu wanakuja wanakwenda chini ya hapo; data zinatuonyesha mtu anatumia asilimia chini ya asilimia 50 (less than 50) hata asilimia 25. Ameletewa bidhaa za dawa, akawapatia wateja, wakachangia pesa, lakini hakurudisha kwenda kununua dawa, definitely mtaji uta- Collapse, kwa sababu inatakiwa iwe revolved.

Mheshimiwa Naibu Spika, tukajiuliza huwezi ku- revolve dawa peke yake, lazima uende kwenye dimension ya quality care; uboreshe huduma ili wateja wanaokuja pale pia wawe akina sisi ambao tukiugua na kadi zetu za bima, tunaamua kwenda hospitali zile za akina fulani badala ya kwenda zile za kwetu. Kwa sababu ukienda pale unajibiwa vibaya, mazingira mabovu, hupendelei. Kwa hiyo, tunakuwa tunapata watu wa msamaha kama wale niliowasilisha data jana kwamba kwenye Regional Referral Hospital shilingi bilioni nne, kwenye hospitali zetu kubwa za kibingwa, shilingi bilioni 30.

Mheshimiwa Naibu Spika, hizi ni barriers za management system.zinazosababisha hata huo mtaji wa dawa ukija unaenda kuwapatia watu wasio na bima, kwa sababu wenye bima wameondoka, bima inakuwa inakwenda kwenye vituo vingine na kwenye Serikali hamna kitu; lakini tuna watumishi wetu badala ya kufanya kazi kwenye vituo vyetu na wenyewe wanaondoka, wanakwenda kule private. Kwa hiyo, kuna vurugu nyingi sana hapa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kupitia Bunge lako Tukufu, niwape moyo kwamba tumedhamiria kuboresha eneo hili hapa kwa kuangalia determinants zote zinazosababisha mtaji wa dawa uyumbe ili tuondoke kwenye dhana ya kwamba Hazina ziko pesa, tutaongeza, tutaongeza; tuweze kufanya revolving kwa kutumia fursa ambazo wenzetu wa private wanafanya na wanaweza kulipa maji, majengo, mishahara, promotion bila kelele kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, haya yote ili yatekelezeke na yasiwe hadithi, tumeamua kufungamanisha kwenye mikataba ya uwajibikaji kwamba sasa tutageuza sasa hizi ziwe Score Card Performance Criteria ili huyu anayepewa kazi hiyo aweze kutekeleza na kupimwa. Hata hivyo tunajiuliza, hizi dawa zinapotelea kule kwenye Halmashauri, determinant gani nyingine tumeiacha? Ni elimu. Tumefurahi sana kuona leo Wabunge wanaongelea habari ya dawa na wanakiri wenyewe kwamba kweli zinaibwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunasema kule Halmashauri tuna mageti yote ya ulinzi, tuna Kamati ya Huduma za Jamii, tuna Kamati ya Mipango na Fedha ya Baraza la Madiwani, tuna Bodi zetu na tuna Kamati za vituo. Huenda hawaelewi. Ripoti zikiletwa hawawezi kugundua viashiria vya upotevu wa dawa au ubadhirifu. Tutawapa elimu hawa wakiwemo Wabunge ambao pia ni Madiwani, wataweza kuwa na uwezo wa kubaini nini kinaendelea hapa na kuchukuwa hatua kwa wakati.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sasa nijielekeze kwenye madeni yote ya dawa. Ilitolewa hoja hapa kwamba, kwa nini yasifutwe na Wizara ya Fedha? Serikali imeendelea kulipa madeni kwa kadri yanavyohakikiwa ambapo hadi mwezi Aprili, 2021 imeshalipa jumla ya shilingi bilioni 16.3 na hivyo kubaki kiasi cha shilingi bilioni 260.7. Kati ya deni hilo, shilingi bilioni 31.9 ni deni la vituo vya kutolea huduma za afya na shilingi bilioni 228.7 linatokana na utunzaji na usambazaji wa bidhaa za afya za miradi misonge. Serikali haijafikia utaratibu wa kulifuta hilo deni, lakini imedhamiria kuendelea kulipa deni hilo ili kuiboreshea bohari ya dawa (MSD) iweze kuimarisha mtaji wake.

Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo, naomba niseme mbele ya Bunge lako Tufufu kwamba madeni haya yatalipwa na Serikali kupitia Wizara ya Fedha na imeshaanza, lakini tumeweka utaratibu mzuri, vituo vyetu vinadaiwa visinyimwe dawa kule MSD. Kuna makubaliano tu wanawekeana pale, wanakuwa wanazichukuwa zile dawa ili na wenyewe wajenge uwajibikaji wa kwenda kusimamia hiyo rasilimali kama nilivyosema. Usipofanya hivyo, unakuta mtu anakosea fomu ya bima, takribani shilingi bilioni 2.4 hazijalipwa na bima kwa sababu walipohudumia wateja wa bima badala wajaze vizuri ili hizo hela zikalipwe kule, wakakosea halafu hawakuulizana hata kuulizana kwa nini tumekosea, tujirekebishe wapi? Ikawa ni mtindo, ni trend hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tunataka na wao tuwafundishe kwamba watakuwa wanalipa kidogo kidogo bila kunyimwa dawa, lakini waende kwenye uwajibikaji uliotukuka kuangalia determinants zote hizi ili kesho tuwe na uongozi wenye ubunifu katika kusimamia rasilimali za Umma.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu kiwanda cha Simiyu Medical Product kuna hoja ilitolewa hapa. Hoja hii imeshafanyiwa kazi na tuko kwenye hatua za mwisho za kukamilisha uanzishaji wa kiwanda kitakachozalisha bidhaa zitakazotumika katika vituo vya kutolea huduma za afya zinazotumia malighafi yetu ya Tanzania yaani pamba. Serikali kupitia Hazina inakamilisha taratibu muhimu kabla ya kuanza ujenzi wa kiwanda husika Mkoani Simiyu. Tutalisimamia hili kwa sababu mifuko iliyokuwa inafadhili imekubaliana na imeshawekana sawa, sasa ilikuwa ni utaratibu tu ya kwamba hizo hela zitakapotolewa zitaweza vipi ku-revolve. Hili tunalifanyia kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kulikuwa na ushauri kuhusu mifumo ya kieletroniki; nimesema hii tutahakikisha tunaiimarisha sana katika vituo vyetu, hivi sasa ngazi ya Taifa vituo saba vinatumia mifumo ya TEHAMA maana ni vituo vyote; kwa ngazi ya mikoa vituo 14 kati ya 28 vinatumia mifumo ya TEHAMA; katika ngazi ya huduma ya msingi, Halmashauri vituo 971 kati ya 7,279 vinatumia hiyo mifumo. Kwa sababu tumeanza kutengeneza mifumo hii kwa wataalam wetu wa ndani, itakuwa rahisi sana kuipeleka kule kwa kasi kubwa katika kipindi hiki ili tuweze kuboresha ufuatiliaji wa taarifa zetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kidogo niongelee kuhusu masuala mazima ya rasilimali watu. Katika upande wa rasilimali watu, kulikuwa na hoja kwamba kuwepo na mkakati wa makusudi wa kuajiri watumishi wa sekta ya afya na Serikali hususani Ofisi ya Rais, Menejementi ya Utumishi wa Umma, ihakikishe inatoa vibali vya ajira kwa watumishi wa afya hasa ikizingatiwa kuwa kuna wataaalam wengi mtaani. Ndiyo kuna wataalam wengi mtaani ambao tumewasomesha wenyewe lakini hatujaweza kuwapatia kazi na ni wa kada mbalimbali.

Mheshimiwa Naibu Spika, hapa tumejiongeza. Pamoja na kuajiri watumishi wapya kila mwaka, idadi yao kweli bado haikidhi kama nilivyosema. Kwa hiyo, sasa hivi tuna hivi vituo vyetu ambavyo havifanyi kazi. Tuna wastani wa watumishi 2,800 wanastaafu kila mwaka ambapo tumekuwa hatufanyi replacement kwa kasi. Kama mlivyosikia leo hapa Mheshimiwa Mbunge wetu mmoja alichangia kwamba kumetokea matangazo ya kazi, tuna nafasi takribani 3,337 ukijkumlisha za Wizara ya Afya pamoja na Ofisi ya Rais, TAMISEMI ambapo hizi ni replacement, ndiyo zimetangazwa na ndiyo tunaendelea kuzifanyia kazi ili kusukuma upatikanaji wa watumishi walioajiariwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kibali chetu cha ajira 2021 maombi ya kibali cha ajira mpya ili kuajiri jumla ya watumishi 13.3 pamoja na kibali cha ajira mbadala hiki nilichokisema sasa hivi, kimetolewa ili kuziba nafasi hizo. Tukaona kwamba hapana, tusiendelee tu kwenye kutegemea kuajiri, lazima tujiongeze, tufanyeje ili kuongeza speed ya wenzetu ambao hawana kazi waweze kupata kazi? Tumetayarisha mwongozo, upo kwenye mapitio ya mwisho katika vyombo vyetu Serikali ili tuweze kuwaajiri watumishi wetu kwa mikataba wakati tunasubiri ile ajira kuu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mwongozo ule ukipita, tutaweza kumchukuwa mtumishi tukamwajiri kwa mkataba na anaweza akalipwa nusu ya mshahara wa mtu aliyeajiriwa kama mapendekezo yatapita, kwa hiyo, tutaweza kuwawatia moyo wasikae nyumbani kupoteza ujuzi walionao, wawepo na sisi kadri Serikali inavyopata uwezo, tunazidi kuwachukuwa. Uwezo huo wa kuajiri asilimia 100 lazima tukubaliane tu ni changamoto, siyo tu Tanzania, ni kote kule. Sijui ni wapi walishafika asilimia 100, kwa sababu tunazaliwa kwa asilimia 2.7 kwa mwaka, yaani ni kama vile watu milioni tatu. Unatengeneza hospitali tatu za mikoa, zinazohitaji ikama ya watu 600; sasa, hapa lazima tukubali kuja na huu ubunifu ili tuweze kwenda na mabadiliko ya sayansi na teknolojia katika mustakabali mzima wa kukuza Taifa letu.

Mheshimiwa Naibu Spika, tumegundua kwamba ukiacha suala la ajira lazima pia hapa tuangalie dimension ya productivity. Unakuta tunao watumishi, ukienda kufuatilia productivity yao ipo chini, au sehemu nyingine wako wengi sana, sehemu nyingine wako wachache sana. Wamekaa kwenye maeneo ya mijini; unakuta wako wengi kwa namba au skills pale ziko nyingi. Tunafanya assessment, tunaitaga WISN, ambayo ni Workload Indicator of Staffing Needs ili tuone wingi wa kazi pale walipo ili tuweze kuwasambaza kwenda kwenye maeneo mengine ambayo yana uhitaji mkubwa kuliko hapo.

Mheshimiwa Naibu Spika, hii tunaiita redistribution, ilifanyika katika mikoa 11 ambapo ilisaidia kuwapeleka watumishi kwenye ngazi za zahanati na vituo vya afya na maeneo mengine yenye uhitaji. Mikoa iliyotumia mfumo huu ni pamoja na Iringa, Pwani, Tanga, Mwanza, Shinyanga, Dodoma, Morogoro, Ruvuma, Songwe Mara na Lindi; na tunaendelea.

Naomba nigusie hoja ya CAG. Ilitolewa kwamba ripoti ya CAG imebaini kuna changamoto katika ununuzi na uendeshaji wa mtambo wa kuzalisha barakoa MSD na je, Serikali ina maelezo gani kuhusiana na suala hili? Nimefanya ufuatiliaji, tumefanya ufuatuliaji pamoja na wenzangu wote na taarifa ifuatayo naomba kuiwasilisha kwako.

Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na changamoto ya upatikanji wa barakoa nchini na duniani wakati wa janga lilipokuwa kwenye kasi kubwa Covid 19 Serikali kupitia bohari ya dawa (MSD) iliamua kununua kwa dharura mtambo wa kuzalisha barakoa wenye thamani ya dola za Kimarekani 108,700. Mtambo huo ulianza kufanya kazi mwezi Agosti, 2020 ambapo uwezo mtambo huo wakati huo ilikuwa ni kuzalisha barakoa 48,000 kwa siku.

Mheshimiwa Naibu Spika, mtambo ulipoanza kufanya kazi ilibainika kuwa compressor yake ilikuwa na uwezo mdogo wa kufanya kazi, hivyo watumishi walipatiwa mafunzo ya kutumia mtambo huo ili kuweza kufanya kazi kwa ufanisi. Hivyo, baadaye, baada ya compressor hiyo kuwa imeshanunuliwa uzalishaji katika miezi mitatu ya mwanzo, Agosti, Septemba, ni kweli ulikuwa mdogo lakini baadaye ulipanda kwa 148,000 kwa siku. Kutokana na uwekezaji wa mahitaji ya barakoa kwa vituo vya kutolea huduma za afya sasa vituo hivi vinapata pale MSD.

Mheshimiwa Naibu Spika, niseme tu maneno machache kwamba, sisi kama nchi, masuala haya ya barakoa, masuala ya gloves, gowns, protective gear, ni lazima tufike mahali tujihami sisi wenyewe. Hivi ni vitu vya dharura, vinahitajika ICU, vinahitajika kwenye dharura zetu zote zingine zile za majanga, tuna matishio ya Ebola, tuna matishio ya vipindupindu na mambo kama hayo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo ilikuwa ni sawa na tija kufanya haya maamuzi ili ile inunuliwe iweze kufanya kazi pale. Hata huko tunakokwenda, huenda tukanunua hata mitambo mingine ya kufanya ulinzi wa wataalam wetu, maana ukitegemea nje katika nyakati kama hizi ndipo unapouziwa barakoa moja shilingi 100,000 unaanza kutengeneza hoja nyingine tena, ilikuwaje, zile hela zinakuwa hazitoshi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo naomba ieleweke tu kwamba taarifa sahihi ni kama nilivyotoa. Huo mtambo capacity yake kwa sasa ni hiyo na ulikuwa ni muhimu na tunahitaji mitambo kama hiyo ili ulinzi wetu katika eneo la afya uwe mzuri zaidi badala ya kutegemea nje ambako zikija tena tunasema hazina viwango.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niongelee kidogo kuhusu miradi ya ujenzi. Miradi ya ujenzi tunayo mingi, niliripoti jana miradi 22 kwenye Kiambatisho Na. 14. Hapa ilitolewa hoja kwamba kule Katavi mkandarasi hayuko site licha ya kwamba alitakiwa akabidhi mradi Januari, 2021; kule Hospitali ya Mkoa wa Simiyu nako anasuasua; mradi wa Tumbi nao, EMD nao hauko vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mradi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Katavi unatekelezwa na Mkandarasi SUMA – JKT. Baada ya kuufuatilia na kuona changamoto zake ambazo zilifanyiwa kazi ikapelekea mpaka kubadilisha consultant, nimekaa kikao mimi mwenyewe na SUMA – JKT na wale maafande wote tukakubaliana kwamba mradi huo wa Katavi lazima ukamilike kwa wakati. Tunahama kutoka kwenye conventional contracting tunakwenda kwenye force account, maana tumeona kule ndiyo kuna tija tutaweza kusimamia ukilinganisha na utaratibu uliotumika mwanzo ili tuweze kwenda na wakati, ifikapo Desemba au mapema Januari mwakani mradi huu uwe umekamilika uanze kutoa huduma. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mradi wa Tumbi ulikuwa na matatizo, nilitoa maelekezo kwamba ufanyiwe ukaguzi wa kina, kwa sababu ni hatari sana kuja kufikia mahali umemaliza mradi halafu ukakuta kuna tatizo. Taarifa RAS ameifanya, ameikamilisha ataileta na hela zao, bilioni tatu, zipo, tutaziomba zitoke ziende kumalizia kulingana na ile taarifa imesemaje. Hatuwezi kuishia tulipoishia.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo kwa kifupi miradi yote hii ambayo inaleta changamoto na sisi tumeamua kupambana na hizo changamoto, ikibidi kwa ku-review ile mikataba tuweze kwenda kwenye force account ku- accelerate speed ya kwenda mbele.

Mheshimiwa Naibu Spika, kulikuwa na suala kuhusu kumalizia Wodi ya Saratani Bugando. Hii Wodi ya Saratani Bugando ni muhimu sana, tena itapunguza msongamano sana katika Hospitali yetu ya Ocean Road, lakini itawapunguzia wananchi mzigo wa kwenda Ocean Road, kuhama na ndugu zao waje, gharama zinakuwa kubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, tumetenga fedha kwenye mwaka huu ambazo ni kama bilioni 1.8, tutazitoa. Tutaangalia kama tutaweza kwenda na kasi ya kumaliza hizo hela kwa wakati ili hela isilale ili tuweze kufanya mpango kupitia Kamati yetu ya Bajeti. Ni suala la kuomba tu kibali kwamba hawa wamekwenda na kasi inayotakiwa tuweze kuona namna gani tutafanya reallocation ndani ya Fungu la Wizara ya Afya, Idara Kuu ya Afya kuweza kuhakikisha ile wodi inakamilika. Maana vinginevyo, kama hatutafanya hivyo, tunaendelea kuwaumiza hawa wananchi na kuendelea kuiumiza Ocean Road kwa wagonjwa ambao wangeweza wakatibiwa huko waliko.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu Hospitali yetu ya Kwangwa iliyoko Mara kwamba ikamilishwe mapema, kwani ikikamilika inamuenzi Hayati Mwalimu Nyerere. Ni kweli, Wizara imedhamiria kukamilisha hospitali hii. Inajengwa kwa jengo moja ambalo lina vitalu vitatu; Kitalu A, Kitalu B na Kitalu C. Kwa sasa jengo la Kitalu C limekamilika na huduma za afya ya mama na mtoto zinaendelea kutolewa.

Mheshimiwa Naibu Spika, tumetenga bilioni 11 katika bajeti ya fedha ya mwaka 2021/2022 kwa ajili ya kuendeleza ujenzi wa jengo la Hospitali ya Mkoa wa Mara, Kitalu A na Kitalu B, ujenzi wa jengo la kuhifadhia maiti, jengo la kufulia na kuboresha mazingira yanayozunguka Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mara, kwa hiyo tuko serious kwenye eneo hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, naona muda wangu umekwisha, nimalizie tu neno moja kuhusu madirisha mangapi ya kutolea huduma kwa wazee. Tuko serious na wazee; kama juzi tulipokuwa na Mheshimiwa Rais niliweza kusema kwamba tumekwenda mbele, tumefanya kikao na mitandao inayoratibu shughuli za wazee ambayo ni taasisi zao mbalimbali.

Mheshimiwa Naibu Spika, tumeona kwamba madirisha ta wazee yasiwe tatizo. Tumekwenda kuteua watu watatu kila kituo; Muuguzi yupo, Daktari yupo na Nesi yupo, hawa tutawavalisha ma-T-shirt yanaitwa Nakupenda Sana Mzee. Watakuwa wakifika pale hata kama watumishi ni wachache hakuna dirisha maalum, apokelewe kama VIP, apelekwe kwenye chumba ambacho kitamuona huyu mzee. Mwenyekiti wa hii shughuli ni mimi mwenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo tayari wataalam wangu wameshakusanya haya majina na numbers zipo kule, mdogomdogo tumeshaanza. Sisi wenyewe ni wazee watarajiwa, tupende kukutana na mambo ambayo tulijiandalia sisi wenyewe huku wakati tukiwa vijana.

Mheshimiwa Naibu Spika, Sera ya Wazee tunaifanyia mapitio ili ije kuwa sheria ambayo itatambua haki zao kisheria.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, naomba kuwasilisha hoja na yote mengine yaliyosemwa sisi tumeyapokea, wanaoniomba niambatane nao kwenye majimbo yao niko tayari, baada ya Idi tunakwenda wote tukayaone yaliyoko huko.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana na naomba kutoa hoja. (Makofi)

WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, naafiki.