Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

Hon. Francis Isack Mtinga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Iramba Mashariki

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

MHE. FRANCIS I. MTINGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru kwa kupata nafasi hii muhimu sana ya kuchangia Wizara ambayo inabeba uchumi wa nchi hii. Kwa sababu miundombinu ndiyo inayobeba kila kitu; mazao, products za viwanda na kila kitu.

Mheshimiwa Naibu Spika, niende moja kwa moja kwanza kwenye jimbo langu. Jimbo langu kwa barabara za TANROADS ina mtandao wa kilometa zipatazo 234.5, lakini katika mtandao huu neno lami kwetu sisi ni msamiati kwa sababu kuna kilometa 2.5 tu tena tumezibahatisha tu kwai le barabara inayokwenda Mwanza kwa kuibia kidogo pale Igugulu, kilometa mbili katika mtandao mzima wa barabara za TANROADS, kilometa 234. Sisi watu wa Mkalama lami kwetu ni msamiati.

Mheshimiwa Naibu Spika, na katika barabara za TARURA, takribani kilometa 647 mtandao, hatuna hata robo kilometa ya lami. Sasa tunapofika kwenye suala hili la bajeti kama mwenzangu alivyotaka kuruka sarakasi hapa kwa kweli haka kamgawanyo ka bajeti katika nchi hii inabidi sasa kawe kanaangaliwa kwa vipaumbele.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu wakati wenzetu wanaomba bajeti za kuziba viraka vya lami ambazo wameshazitumia mpaka zimechakaa sasa wanataka wazibe, sisi hatuna hata kipande cha lami. Kwa hiyo, inapofika wakati huu kwa kweli sisi tunaporudi kwa wananchi wetu wanatuuliza hivi ninyi Bungeni kule mna nchi yenu tofauti, mbona wenzenu wana lami za kutosha, sisi tutatembea kwa vumbi mpaka lini? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, unapofika wakati huu wa kugawa hizi bajeti lazima tuangalie vipaumbele. Hii habari ya kusema fedha zikipatikana zitajengwa, fedha zikipatikana, sisi mnatupa wakati mgumu, na sisi tuna wananchi ambao wanataka kula matunda ya nchi yao nzuri inayoongozwa na mama yetu Samia Suluhu Hassan. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ipo barabara ambayo ipo kwenye Ilani, inayoanzia pale Iguguno inapita kwenye Makao Makuu ya Wilaya Nduguti inakwenda mpaka Simiyu kupitia daraja la Sibiti ambalo limejengwa kwa fedha nyingi za nchi hii. Barabara hii ukiacha tu kwamba inaunganisha mikoa miwili; Mkoa wa Simiyu na Mkoa wa Singida na wote tunatambua kwamba Mkoa wa Singida ndiyo Mkoa ambao unalima Alizeti kwa wingi na ninyi mnafahamu tatizo kubwa la mafuta katika nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile wote mnafahamu kwamba Mkoa wa Simiyu ni miongoni mwa mikoa mikubwa inayolima Pamba katika nchi hii. Kwa hiyo, tunapoongelea barabara hii ya Simiyu – Singida kuunganishwa kwa lami, tunaongelea uchumi wa nchi hii. Tunaongelea kuondoa changamoto za nchi hii. Kwa hiyo, naomba katika vipaumbele vya Wizara barabara hii ambayo ipo kwenye Ilani inayounganisha mikoa; hii sera ya kuunganisha mikoa ilianza tangu Awamu ya Nne, sisi bado hatujaunganishwa kati ya Mkoa wa Simiyu na Mkoa wa Singida. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba barabara hii iwekwe kwenye umuhimu wa kipaumbele, hii habari ya kusubiri, najua Mheshimiwa Waziri anaweza akaja na majibu mepesi tu, kwamba fedha ikipatikana; naomba aje na majibu yanayoeleweka katika barabara hii ili nasi tuondoke kwenye unyonge wa kutokuwa na lami. Kwa kuanzia basi, angalau kwa kipaumbele, hata zile kilometa 42 tu za kutoka Iguguno mpaka Makao Makuu ya Wilaya zipate lami. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Mkoa wa Singida Wilaya pekee ya Mkalama ndiyo inayounganishwa na vumbi na Makao Makuu ya Mkoa. Hata kwenye Kamati pale nimesikia wanasema vipaumbele, Makao Makuu ya Wilaya, kuunganishwa na Mkoa kwa lami. Kwa hiyo, angalau hizi 42 basi zije kwa bajeti ya dharura angalau tupate kilometa 42 za lami kutoka Makao Makuu ya Wilaya mpaka Makao Makuu ya Mkoa, kwa kuanzia katika barabara hii ambayo ipo kwenye Ilani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nami sitaruka sarakasi, lakini kwenye kushika shilingi nikipata nafasi kama hamjaja na maneno mazuri kuhusu barabara hii kwa kweli tutaungana na Mheshimiwa Flatei, yeye akiruka sarakasi mimi nagaragara chini. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba tena nirudi kwenye Jimbo langu. Lipo daraja linajengwa katika Mto Ndurumo, daraja la msingi; daraja lile linasuasua sana. Waziri sijui kama litaisha na ni muhimu sana, lakini kwa sababu daraja lile linaendelea, pale kuna daraja la dharura la jeshi ambalo linatumika. Namwomba Mheshimiwa Waziri na Walinzi wa Ulinzi pia, daraja lile la jeshi ambalo lipo pale, baada ya daraja kubwa kukamilika, daraja lile liendelee kuhifadhiwa kwa udharura wake ndani ya Mkalama, lisiondoke kwa sababu lipo bonde kubwa la mto ambalo linatenganisha vijiji karibu vitatu; vya Yulansoni, Lelembwe na Mulumba ambapo wanakuwa kisiwani wakati wa masika na watoto wanakufa wakati wa kwenda shuleni kule Katani ambapo Kata ipo Kinyangire na bonde lile linatenganisha.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba daraja lile la jeshi liendelee kuhifadhiwa kwa udharura wake, lakini ndani ya Mkalama lipelekwe katika bonde hili la Yulansoni. Wananchi wa eneo lile wana uchumi mkubwa lakini barabara imekuwa ni shida na hatuna kivuko. Kwa hiyo, daraja lile la jeshi litakapokamilika daraja hili kubwa, libaki pale Mkalama katika eneo la Yulansoni.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niende kwenye eneo pia la TANROAD. Najiuliza sana, TANROAD kila mkoa wapo na wanapata bajeti, lakini pale kwangu Mheshimiwa Flatei alikuwa analalamika kwamba barabara zake ni za vumbi, lakini mimi ninapotoka Mkalama naenda kwa jirani yangu Manyara, kwa Mheshimiwa Flatei; ninapotembea na barabara za vumbi za Mkoa wa Singida, unapofika tu, “Sasa unaingia Manyara,” nakutana na utofauti kabisa wa barabara; za kwangu za TANROAD Singida zina mashimo, lakini ukiingia TANROAD Manyara unakuta nzuri. Kwa hiyo, nikaona hapa kuna uzembe katika suala la kusimamia Wakandarasi wanaokarabati hizi barabara. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Mheshimiwa Waziri mwangalie vizuri Meneja wa TANROAD Singida, ukarabati wa barabara za TANROAD mkoa wangu wa Singida zifanyike vizuri kwa fedha ndogo inayopatikana. Hata timing ya kutengeneza hizi barabara; unakuta barabara inatengenezwa wakati wa mvua. Bado hata Mkandarasi hajaondoka, ile iliyotengenezwa imeshabebwa na maji. Sasa sijui hizi program zao za utengenezaji zimekaaje! Naomba ziangaliwe vizuri; na kile kidogo cha ukarabati kinachofanyika kiweze kudumu na wananchi wafurahie. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ile imetengenezwa juzi tu pale, sasa hivi ni mashimo, lakini ukiingia Manyara unakuta barabara safi. Hii inaonyesha kabisa kuna uzembe katika suala la utendaji. Wengine wanafanya vizuri, fedha ni hiyo hiyo, usimamizi unakuwa mbovu. Naomba hili lifike na walisikie, najua watakuwa wameshalisikia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kuongelea jimbo sasa niuongelee mkoa wangu. Singida tuna uwanja wa ndege na kwa bahati nzuri katika hotuba ya Rais iliyopita uliongelewa ni katika viwanja 11 vitakavyojengwa. Nataka niombe, katika vile viwanja 11, Uwanja wa Mkoa wa Singida unatakiwa upewe kipaumbele cha pekee, kwa sababu ni uwanja ulio jirani na Makao Makuu ya Nchi. Uchukuliwe kama uwanja wa dharura, pale inapotokea tatizo katika Uwanja wa Makao Makuu ya Nchi, uwanja wa dharura ulio karibu unapaswa kuwa uwanja wa Singida. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, leo hii ikitokea tatizo, ndege inabidi irudi Dar es Salaam kilometa zaidi ya 500, wakati hapa Singida ni kilometa 240. Kwa hiyo, naomba Wizara iangalie uwanja wa Mkoa wa Singida kama uwanja wa dharura. Hii ni Makao Makuu ya Nchi, wanatua Mabalozi hapa, wanatua Marais wa nchi mbalimbali hapa; litakapotokea tatizo lolote la kianga, uwanja pekee wa dharura ni uwanja wa Singida.

Kwa hiyo, naomba uwanja huu katika vile viwanja 11 wenyewe utazamwe kwa jicho la tofauti kama uwanja wa emergence pale linapotokea tatizo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nilitaka nisisitize hilo katika suala la Mkoa wangu wa Singida. Nawashukuru sana, najua ujumbe umefika. Kama ambavyo nimesema, Mheshimiwa Flatei akiruka, mimi nitagaragara, namwomba Mheshimiwa Waziri aje na majibu ya kutosha katika maeneo haya ya Mkoa wangu wa Singida. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi. Naunga mkono hoja. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. (Makofi)