Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Bukene
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. SELEMANI J. ZEDI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii ili nami niweze kuchangia kwenye bajeti hii muhimu sana inayohusu barabara zetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama ambavyo Waheshimiwa Wabunge wengi wamesema ikiwemo na wewe mwenyewe, kila mwaka wakati wa bajeti tunakuja hapa, tunajadili na kupitisha orodha ndefu ya barabara, lakini mwaka ukiisha unakuta hata robo ya hizo barabara hazijafanyiwa kazi. Hii imekuwa ni desturi ya miaka yote.
Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa nafikiri nishauri, tujaribu mwaka huu kwa sababu kuliko kuwa na orodha ya barabara 200 ambazo hatuna uwezo wa kuzishughulikia ni afadhali tukawa na barabara hata 50 tu kwa mwaka ambazo tunajua tuna uwezo halafu tukapanga priority tukaona ipi ianze na ipi ifuatie.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama ambavyo umesema, nashauri kwamba mwaka huu fedha tutakazozipitisha kwa ajili ya ujenzi wa barabara mwisho wa bajeti wakati tunapitisha sheria ya fedha ile Finance Bill, tuweke kipengele fulani cha kuzi-ringfence kwamba mwaka huu fedha zitakazotengwa kwa ajili ya ujenzi wa barabara lazima zote zitoke na zikafanye kazi ya kujenga barabara. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu mwaka huu wa fedha tulionao unaoisha mwezi ujao, tulipitisha shilingi trilioni 1.5 kwa ajili ya barabara, lakini mpaka sasa fedha ambazo zimekwenda ni shilingi bilioni 900 tu. Kwa hiyo, kuna shilingi bilioni 600 ambazo hazikwenda kujenga barabara. Sasa hizi shilingi bilioni 600 ambazo hazikwenda kwa mujibu wa taarifa ya Kamati maana yake ni orodha ya barabara ambazo hazikushughulikiwa na ambazo wala hazitafanyiwa kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kule kwangu kuna barabara ile ya Tabora – Mwambali – Bukene – Kagongwa, inaunganisha Mkoa wa Tabora na Kahama, mwaka huu wa fedha unaoisha mwezi ujao, tulitengewa fedha na ikasemwa kwamba itaanza kujengwa kwa kiwango cha lami. Ukiwa umebaki mwezi mmoja, hakuna chochote kilichofanyika. Hakuna hata shilingi iliyopelekwa kwa ajili ya kufanya shughuli yoyote na mwaka huu nimepitia randama, barabara ile ile tena imetengewa fedha na maelezo ni yale yale kwa ajili ya kujengwa kwa kiwango cha lami.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kama mwaka tunaoumalizia ilitengewa fedha, tukapitisha na hakuna chochote kilichochafanyika, nitaaminije kwamba hizi sasa zilizotengwa zitakwenda kufanya kazi? Kwa sababu yatakuwa yale yale!
Mheshimiwa Naibu Spika, ndiyo maana nashauri kwamba kuliko kuwa na orodha ya barabara nyingi na tunatenga fedha nyingi, lakini mwisho wa mwaka hakuna kinachofanyika, kama walivyosema Waheshimiwa Wabunge wengine waliotangulia, ni afadhali tuwe na barabara chache kwa kipaumbele maalum, ambapo tunajua tutaweza kuzi-finance ili ziweze kushughulikiwa badala ya kuwa tunapitisha bajeti, tunaondoka na matumaini makubwa, tunafika huko tunawapa matumaini wananchi wetu, lakini mwisho wa siku hakuna chochote ambacho kimefanyika.
Mheshimiwa Naibu Spika, naishauri Wizara, kwamba kwa mfano kwenye hii barabara yangu, ukienda kuulizia TANROAD Tabora wanakwambia Wizara haijatupa kibali cha kuajiri Mkandarasi au cha ku-float tender. Sasa fedha mwaka huu unaisha zimetengwa, bado mwezi mmoja, kwa mwaka ujao zimetengwa tena. Naiomba Wizara, safari hii toeni kibali kwa TANROADS Tabora ili iweze ku-float tender, kuitangaza ili tuweze kupata mkandarasi aweze kujenga barabara hii muhimu sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu shughuli ambazo zinahitajika kufanyika ni kulipa fidia kwa wananchi ambao wameshapimiwa muda mrefu ili wapishe ujenzi na gharama ya ku-float tender, kui-engage wakandarasi ili mkandarasi aweze kupatikana.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama ulivyosema kwamba barabara kubwa haiwezi kufanya kazi bila zile feeder road zinazotoka vijijini, Jimbo langu nimekuwa nikisema mara nyingi, barabara zinazotoka ndani mashambani ambapo ndipo mazao yanapatikana kwa ajili ya biashara, ni mbovu, haziko vizuri. Kwa hiyo, hii nayo inapokuwa haifanyiwi kazi, basi hali inazidi kuwa mbaya sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, naishauri Wizara, barabara hii ndiyo ambayo inapita mahali ambapo mradi mkubwa wa kujenga coating yard kwa ajili ya mabomba yanayotoa mafuta Hoima - Uganda mpaka Tanga ndipo ile yard kubwa itajengwa pale. Kwa hiyo, barabara hii ndiyo itapitisha mabomba yote yatakayokwenda kupakwa ile rangi maalum ili yakifukiwa chini yasioze; mabomba yote ya kutoka Uganda mpaka Tanga, ile shughuli itafanyikia jimboni kwangu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, barabara hii nashauri Wizara, mkae na Wizara ya Nishati, wale wenye project hii wana-finance baadhi ya huduma ambazo zinakuja pale, kwa mfano umeme unaokuja pale unakuwa financed na project hii, maji yanayokuja pale yanakuwa financed na project hii. Kwa hiyo, hata barabara kwa sababu hayo mabomba yakifika Nzega lazima yachepuke na yaende kama kilometa 40 ndani ya barabara hii ndiyo yafike kwenye hiyo yard. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, mnaweza kukaa na Wizara ya Nishati mkazungumza ili sehemu hiyo ya kilometa 40 kutoka Nzega Mjini mpaka kwenye hiyo yard, ili muweze kushirikiana na mwone namna gani mtaijenga kwa kutumia gharama za pamoja. Kwa hiyo huo ni ushauri wangu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niungane na hotuba ya Wizara pamoja na hotuba ya Kamati kuhusu ujenzi wa SGR na kile kipande cha kutoka Tabora mpaka Isaka pale katikati kuna station kubwa sana ya Bukene ambayo siku zote imekuwa ni station kubwa na ndiyo inahudumia Wilaya nzima ya Nzega na Igunga. Kwa hiyo, pale ni lazima kuwe na logistic kubwa ya kushusha mizigo kwa ajili ya Nzega yote na Igunga yote kwenye huu mradi wa SGR. Sisi kwetu jambo hilo likifanyika maana yake ni ajira kwa wananchi na vijana wa maeneo yale. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi, naunga mkono hoja. Hata hivyo, nashauri kwamba mwishoni wakati wa Finance Bill tuweke kipengele kwamba fedha zitakazotengwa kwa ajili ya barabara ziwe ringfenced na zote zipatikane ziende kwenye miradi ya barabara ili kwa mwaka huu tuangalie effect yake kwa mwaka mmoja, badala ya kutenga shilingi trilioni 1.5 halafu zinaenda shilingi milioni 900, halafu shilingi bilioni 600 zote hazijaenda na barabara zinakuwa hazijashughulikiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana, naunga mkono hoja. (Makofi)