Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kyela
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. ALLY A. J. M. JUMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Naomba kwa utangulizi nikushukuru sana wewe mwenyewe, Naibu Waziri wa Maji na Mheshimiwa Suma Fyandomo na Bahati kwa kwenda kuwaona wahanga wa mafuriko kule Ipinda. Wanawashukuru sana. Mlichokifanya ni kitendo cha utu Mungu aendelee kuwabariki. Ahsante sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia naomba nikushukuru kwa utangulizi ulioanza nao na ninaomba hata katika hotuba yangu basi haya mambo yaingizwe moja kwa moja kwamba nami nayasema kama ulivyoyasema. Kitendo cha ugawanyaji rasilimali yetu, kufuatana na umuhimu wa sehemu ambapo barabara na sehemu za uchukuzi unaenda ni kitendo ambacho kinatakiwa kizingatiwe sana na Wizara yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimejipanga nizungumzie mambo machache. La kwanza, ni suala la Serikali yetu kutimiza wajibu wake. Serikali kupitia Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi nataka nikiri inatimiza wajibu wake ipasavyo. Hata hivyo: Je, watendaji wetu wanafanya kazi zinazotakiwa? Hapana. Maana Serikali yetu inatoa fedha za matengenezo ya barabara kupitia Mfuko wa Barabara na kwa kweli zinatoka vizuri, lakini wenzetu wanaoenda kuzitumia hizi fedha wanafanya kazi ambayo kwa kweli wanaiaibisha taaluma ya Uhandisi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, zipo barabara nyingi, lakini nitatolea mfano barabara chache tu. Haiingii akilini, barabara inafanyiwa matengenezo, hapa kiraka kinachimbwa, wanatengeneza, lakini ukikaa siku mbili, ukirudi tena hapo hapo unakuta shimo. Naomba tujiulize, tatizo liko wapi? Haya yanapoteza rasilimali zetu sehemu moja kutengenezwa mara mbili.
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, utakuta sehemu iliyotengenezwa ni hiyo hiyo, sehemu inayofuata nayo inaharibika hakuna hata mita moja, sentimita mbili hapo hapo shimo linatokea. Hii barabara tunayoipita ya kutoka Dodoma kuelekea Iringa, kwa kweli wakati mwingine hatutakiwi kuwasimulia hata watoto wadogo, watatushangaa kabisa. Namwomba Mheshimiwa Dkt. Chamuriho, Waziri wetu haya matatizo myaangalie yasiendelee tena.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili, ni suala la ubora wa barabara zetu ambazo zinajengwa. Unashangaa kuna barabara zimejengwa hazina hata miaka kumi, lakini wameshaanza kuweka viraka. Tatizo liko wapi ndugu zangu? Tunapofeli ni wapi? Hivi ma-engineer wetu wako wapi? Tatizo kubwa tunaanza kusingizia eti Mkandarasi ndiye anafanya hivyo. Siyo kweli. Naomba hapa Bunge hili tuelewane vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, anayefanya barabara yetu idumu na iwe nzuri ijengwe kwa viwango siyo mkandarasi, ni msimamizi (consultant). Hao wanaajiriwa na Serikali yetu na wanasimama upande wa Serikali. Sasa nani alaumiwe hapa? Naomba sana, kuanzia sasa nashauri tuwe na standard za ujenzi wa barabara za Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kama tunashindwa kuweka standards zetu basi tudese. Tufanye tutengeneze desa, nami hilo desa ninalo Mheshimiwa Waziri. Desa lenyewe ni barabara ya kutoka Uyole kwenda Kasumuru. Kwa nini tusichukue kama mfano? Kwa nini tusichukue nyaraka zao tukazitumia kama standard ya ujenzi wa barabara za Tanzania? Barabara ile ndugu zangu imejengwa mimi nina ndevu moja; ipo. Mpaka nimefikisha ndevu nne, naiona, miaka zaidi ya thelathini ipo.
Mheshimiwa Naibu Spika, Barabara ya kutoka Iringa kwenda Igawa sasa hivi ina vipara na haitadumu zaidi hata ya miaka kumi ijayo. Naomba tutengeneze standard zetu. Barabara ile ndugu zangu ya Uyole Kasumulu, ikitengenezwa vizuri, ikisimamiwa vizuri ina uwezo wa kuishi miaka mingine kumi. Walijenga SOGEA nina uhakika nyaraka za barabara ile zipo, twendeni tuzichukue, tutengeneze, tuziweke vizuri, iwe ni reference ya ujenzi wa barabara zetu, kila nchi duniani ina reference ya ujenzi wa barabara zake. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niongelee masuala ambayo yanaharibu barabara, mojawapo ni matuta, matuta barabarani yanaharibu barabara zetu. Ndio maana hata ukiangalia matuta yenyewe hayana hata standard, mengine yamekaa kama vichuguu, mengine yamekaa utafikiri ni matuta ya mbatata sasa, tuelewe lipi na ndio maana nataka niseme barabara zetu matuta yanaziharibu. Kwa nini tusifanye utaratibu mwingine? Matuta yana athari nyingi sana kwa uchumi wa nchi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, linapokuwepo tuta ni lazima mtu akamate breki, vipuri vile vya breki hatutengenezi hapa nchini vinatoka nje tunatumia pesa zetu kununua vitu nje ya nchi. Uchumi wetu unapungua. Kila unaposimama ukikanyaga breki unapoanza kuendesha gari, gari linakula mafuta mara ishirini ya lilivyokuwa linatembea. Mafuta hatuna hapa, lakini kitaalam ile lami haiwezi ikastahimili mzigo unaosimama, inastahimili mzigo unaodundadunda. Kwa hiyo, naomba hebu tuachane na haya tutafute njia nyingine ya kuweka hata box cover tu watu wapite chini barabara ipite juu haitasumbua hiyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho, naomba nisemee kidogo barabara moja ambayo inatoka Ibanda kwenda Itungi Port. Meli zimejengwa tunaishukuru Serikali, lakini mpaka sasa meli zinashindwa kupata hata mafuta. Tarehe 13 -17 Aprili, gari la kupeleka mafuta kwenye meli limeshindwa kupita, kwa sababu barabara ni mbovu na barabara hii tangu mwezi wa Disemba, 2019 iko mezani kwa Mtendaji Mkuu atoe kibali.
Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sasa hivi inaenda kutengenezwa, naomba niishukuru Serikali, lakini zaidi ya yote naomba pia Serikali itusaidie watu wanaotembea na vimulimuli wameweka kwenye magari mbele pale kama vile na wao ni rider, jamani tunashindwa kutembea vizuri barabarani, tunaomba Serikali itoe tamko katika hili.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)