Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

Hon. Masache Njelu Kasaka

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Lupa

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

MHE. MASACHE N. KASAKA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi niweze kuchangia hotuba nzuri iliyowasilishwa na Mheshimiwa Waziri. Nimpongeze kwa hotuba nzuri, nipongeze Manaibu Waziri pamoja na watendaji wote. Sina shaka na uzoefu wa Mheshimiwa Waziri kwa kuwa alikuwepo kwenye Wizara hii kama Mtendaji Mkuu, kwa hiyo, ninaimani mambo mengi ambayo ameyaeleza hapa anayafahamu vizuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kuongea kwenye barabara, kwa kweli kwenye bajeti hii ambayo imesomwa leo, barabara yetu ya Mbeya - Chunya - Makongorosi zimetengwa takribani bilioni 13, lakini hizi bilioni 13 hizi zote, zitaenda kuishia kwenda kulipa madeni ya wakandarasi ambao wamefanya hii kazi. Barabara hii imekamilika kutoka Mbeya mpaka Chunya na sasa hivi inaendelea Chunya – Makongorosi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kipande cha Mbeya – Chunya kimeshakuwa na mashimo, tumeshakuwa na viraka. Mheshimiwa Waziri alikuja wiki mbili zilizopita alikuja akaona na nilimwambia kwamba, standard za barabara anazojenga inakuwaje na hii barabara toka imekamilika ina miaka karibu mitatu tu na hii bado iko chini ya uangalizi wa mkandarasi, lakini tayari imeshakuwa na viraka, sasa sijui miaka mitano mbele itakuwaje. Kwa kweli sisi watu wa Chunya tulihitaji sana hii barabara kwa kiwango cha lami, lakini kiwango ambacho kilijengwa mpaka sasa hivi tuna wasiwasi zaidi ya miaka mitano inayokuja.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo na mimi nitoe ushauri standard za viwango vya barabara za TANROADS ziwe kimoja ile layer ya juu inayojengwa iwe moja kwa barabara zote za TANROADS. Sio barabara hii inawekwa tabaka hili na barabara nyingine inamwagwa tu lami na baadaye zinawekwa kokoto juu, kwa hiyo magari yakija kupita barabara zile zinakuwa na mashimo. Pia tujue kwamba barabara ya lami inapokuwa imetengenezwa eneo Fulani, maana yake matumizi ya ile barabara yanaongezeka, kama ilivyo kwa barabara ya Mbeya – Chunya – Makongorosi. Barabara hii waliweka makadirio ya chini ya kupita magari, sasa hivi magari ni mengi mno ndio maana imeanza kuwa na viraka.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia ujenzi wa barabara ya kuanzia Makongorosi – Rungwa – Mkiwa, hii imekuwa story sasa ya muda mrefu, kila siku inazungumzwa hii barabara, kila siku upembuzi yakinifu unaendelea. Kwenye bajeti hii zimetengwa hapa kuanzia Makongorosi – Rungwa wameonyesha hapa kilomita 50, lakini bado wanasema mpaka fedha zitakapopatikana! Pia kama hiyo haitoshi, hata upande wa kuanzia Ipole kuja mpaka Rungwa hivyo hivyo zimetengwa kiasi cha kilometa 56, lakini mpaka fedha zitakapopatikana. Kwa hiyo, kwa mtindo huu hatuwezi kwenda tukafika.

Mheshimiwa Naibu Spika, hizi barabara zimeahidiwa kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi, tumeinadi Ilani hii kwa nguvu zote, tumewaaminisha na kuwaambia wananchi wetu. Kama fedha hazipatikani maana yake tutarudi kule kule kila siku. Sasa najiuliza hapa, sisi watu wa Mkoa wa Mbeya sisi tulikosea wapi? Maana yake barabara ya kuanzia Igawa - Mbeya Mjini mpaka Tunduma, hivyo hivyo fedha hakuna. Barabara za kuanzia Mbeya Mjini kwenda Makongorosi mpaka Rungwa, fedha hakuna. Vilevile ya Makongorosi, Mkwajuni mpaka Mbalizi, fedha hakuna na ndugu yangu Mheshimiwa Ally amezungumza ya kwenda mpaka Kasumulu kule, fedha hakuna. Sisi Mbeya kuna mradi gani wa barabara ambao fedha imetengwa kwa mwaka huu?

Mheshimiwa Naibu Spika, nimwombe Mheshimiwa Waziri, sisi watu wa Mbeya tuna shida sana ya hizi barabara. Naomba waangalie vizuri bajeti hii angalau na sisi watu wa Chunya kuanzia Makongorosi ili na sisi watu wa Tarafa ya Kipembawe kule nao waweze kuona lami kwa mara ya kwanza. Naomba sana Waziri akayafanyie kazi haya, atakapokuwa anahitimisha hoja yake tuweze kupata majibu mazuri zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nizungumze kidogo kwenye upande wa kiwanja cha ndege. Nimeona hapa kwenye bajeti hii nzuri ambayo Mheshimiwa Waziri ameisema ina maneno mazuri sana. Kiwanja chetu cha Songwe kimekuwa kila mwaka kinaongelewa habari ya kuwekwa taa, kila mwaka inaongelewa habari ya kuweka tabaka la juu, kila mwaka inaongelewa habari ya jengo la abiria na mwaka huu pia takribani karibu bilioni tisa zimetengwa, hatuna uhakika kwa maelezo ya miaka ya nyuma, je, hizi fedha zitatoka?

Mheshimiwa Naibu Spika, niseme kwamba, kwa kiwango hiki cha pesa ambacho kimetengwa, badala ya mambo mengi kufanyika kwenye kile Kiwanja cha Songwe, basi angalau mambo mawili tu yafanyike. Liboreshwe jengo la abiria, lakini pia ziweze kutengenezwa zile taa za kutua ndege pale, hayo mambo mengine ya kutengeneza fensi na mambo ya matabaka mengine yatafuata baadaye, ili twende awamu kwa awamu, kuliko fedha hiyo kidogo ambayo inatolewa yote iende kufanya kazi pale haitaonekana nini ambacho kimefanyika. Hii iende pia kwenye viwanja vingine ambavyo vimetengewa fedha kwa mwaka huu wa fedha.

Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumze kidogo upande wa bandari. Bandari yetu hii kuna uwekezaji mkubwa sana umefanyika na kama tunavyojua, bandari ni lango kubwa la uchumi. Geti Na.1 mpaka Na.7 limeweza kutengenezwa, kina kimeweza kuongezwa na sasa hivi tunaona geti la Na.7 na Na.8 yanaendelea na Geti Na. 12 na Na. 13 yanaendelea na usanifu wake. Hii ni kazi nzuri, tuipongeze Serikali kwa namna nzuri ambayo inafanya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kama tunavyojua kwa kuwa bandari ndio lango kuu, linachangia kwenye uchumi lakini pia linachangia kuleta ajira, pale kwenye bandari kuna taasisi nyingi takribani zaidi ya 30 ambazo zinaizunguka bandari yetu hii. Kwa hiyo bandari inaweza ikaonekana kwamba ufanisi wake ni mdogo kwa sababu tu hizi taasisi nyingine hazina ofisi palepale bandarini. Kwa hiyo, nashauri hizi taasisi nyingine hizi ziweze kuweka ofisi zao palepale bandarini na ikiwezekana kuwe na dirisha dogo moja ambalo taasisi zote zitakuwepo pale. Hapo ndipo ufanisi wa hii bandari utaweza kuonekana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nishukuru Waziri Mkuu alikuja juzi pale na akawaambia watu wa TRA wawe na ofisi palepale bandarini, sio mtu anatoka pale chini bandarini mpaka apande juu kule, tena arudi chini, tunapoteza muda pasipokuwa na sababu.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia, kwa kuwa hii bandari inatoa mizigo na nchi jirani pia, nitoe angalizo, wenzetu wa Zambia wametengeneza sheria, hii sheria inataka mizigo yote inayosafirishwa kwenda Zambia iweze kutolewa na makampuni ya Kizambia yaani zile clearing and forwarding lazima ziombewe zikiwa Zambia, mana yake kampuni za Kizambia ndio ziweze kupata hizi kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kana kwamba hiyo haitoshi mpaka makampuni ya usafirishaji pia yale ya logistic lazima na yenyewe ya kutoka Zambia yaweze kufanya hivyo. Maana yake sasa sisi hapa makampuni yetu ya clearing and forwarding hayataweza kupata kazi, lakini pia na makampuni ya logistic hayawezi kupata kazi, sisi tutabakia na barabara yetu kuharibika, makampuni yote yatafanya kazi huko.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa kengele ya pili imegonga, mengine nitaandika kwa maandishi, naunga mkono hoja. (Makofi)