Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Magu
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. BONIVENTURA D. KISWAGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia hotuba ya bajeti ya miundombinu. Kuna lugha pale mbele nilitoa, nilikosea kidogo ni ulimi tu nadhani itafutwa kwenye Hansard siwezi kuchongea wizara hii kubwa na muhimu kwa Taifa letu. Najua sisi Kiswahili tulikijua shuleni hatukukijua kabisa nyumbani. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze Waziri na Naibu Waziri wa Uchukuzi kwa sababu tunajua kwamba kabla ya kuwa Waziri alikuwa alikuwa Katibu Mkuu kwenye Wizara hii, miradi yote ambayo ameisimamia ni miradi ya kielekezo. Kwa hiyo, tunaamini kwamba kwenye bajeti yake kadri alivyojipanga atafanya vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia tumpongeze Katibu Mkuu na yeye tunajua kwamba yuko vizuri katika wizara hii na atafanya kazi vizuri sana. Pamoja na wasaidizi wao anayesimamia reli Bwana Kadogosa, anayesimamia bandari Bwana Erick, anayesimamia TEMESA Bwana Masele, anayesimamia ndege Bwana Majingi na anayesimamia Ndugu yangu Mfugale naye yupo vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, uchumi wowote duniani ili ukue unategemea miundombinu, miundombinu ya reli, miundombinu ya barabara, miundombinu ya ndege na meli. Kwa hiyo, ujenzi wa reli ya Standard Gauge ulivyoanza Dar es Salaam na Morogoro – Makutupora na sasa Mwanza – Isaka kuna ulazima wa haraka sana kuanza ujenzi wa reli kutoka Makutupora – Tabora na Tabora - Isaka ili kuhakikisha kwamba vipande hivi vinakuwa na maana ya kuleta uchumi kwenye taifa hili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu tutakapokamilisha kutoka Dar es Salaam mpaka Makutupora, tukikamilisha Mwanza – Isaka, tukawa na gape hapa katikati hatutakuwa tumejenga uchumi unaostahili katika Taifa letu. Namshukuru sana Mheshimiwa Rais wakati anahubia Bunge alisema vipange vyote hivi vianze. Sasa niombe waziri mshaurini Mheshimiwa Rais hata kama ni mapato ya ndani, hata kama ni kukopa kwa sababu deni letu ni himilivu tukope ili tuweze kuunganisha vipade hivi ili tuweze kuleta uchumi kwa nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunahitaji ndege ya mizigo, Hayati Dkt. John Pombe Magufuli aliahidi kwamba atanunua ndege za mizigo. Wanalalamika sana watu wa Kusini wanaolima matunda, tunalalamika sana sisi wa Kanda ya Ziwa tunaosafirisha Samaki na matunda pamoja na mbogamboga tunahitaji ndege ya mizigo ili kuhakikisha kwamba biashara zinafanyika kutoa mazao yetu hapa na kwenda Nchi za Nje. Kwa hiyo, naamini kwamba msimamizi wa Shirika la Ndege ajiweke vizuri, aishauri vizuri Serikali ili tuhakikishe kwamba tunanunua ndege hiyo mpya ya mizigo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunajua kwamba tunayo mahitaji makubwa sana ya barabara zetu kama ambavyo wenzangu wamesema. Nina barabara ya Magu, Bukwimba, Ngudu ambayo ipo kwenye Ilani yetu ya Chama cha Mapinduzi ukurasa wa 74 na hii barabara inahitaji kujengwa tu kwa sasa. Lakini nimeona kwenye hotuba ni kwamba Serikali inatafuta fedha hata mwaka jana Serikali ilikuwa inatafuta fedha. Ina maana utafutaji wa fedha huu haukamiliki? Barabara hii ikaweza kujengwa? Mwaka jana mmetafuta fedha na mwaka huu mnatafuta fedha, maana na mwaka kesho mtatafuta fedha, tunakamilisha lini hii barabara! Kwa sababu tunaamini kwamba baada ya standard gauge kukamilika hii barabara ndiyo itakayosafirisha shehena za mizigo kupeleka Nairobi.
MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Kiswaga kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Tabasam.
T A A R I F A
MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nimweleza msemaji, ni kwamba barabara hii ya Magu, Ngudu – Kwimba hadi Hungumalwa imeahidiwa na Marais wanne haijawahi kutokea katika nchi hii. Ameahidi marehemu Mkapa ameahidi, ameahidi Mheshimiwa Kikwete, ameahidi Mheshimiwa Marehemu Magufuli na ikaahidikiwa na Mheshimiwa Samia, haijawahi kutokea sasa nafiriki labda tu ifutwe. Mheshimiwa Kiswaga. (Makofi/Kicheko)
NAIBU SPIKA: Sasa Mheshimiwa Tabasam tunaifutaje barabara. Mheshimiwa Kiswaga endelea.
MHE. BONIVENTURA D. KISWAGA: Mheshimiwa Naibu Spika, siungi mkono kufuta, lakini naunga mkono kwamba imeahidiwa na Marais wanne. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunaomba sasa tupate hizo fedha, Lakini kuna barabara ya Magu mpaka Mahaha, barabara hii inafungua uchumi kutoka Simiyu mpaka Magu Mwanza iliahidiwa na Rais Dkt. John Pombe Magufuli mwaka 2015. Waziri ninakuomba barabara hii uione kwa macho mawili ili uweze kuitengea fedha itekelezwe kwa lami kwa sababu ni barabara muhimu sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunashukuru kwamba design sasa inaendelea barabara ya daraja pale Sukuma itatusaidia pia kuendeleza barabara hii. Tuna barabara ya Kisamba – Sayata, Simiyu hii ni barabara ambayo ina sifa za kuingizwa kwenye TANROADS, lakini haijaingizwa kwenye TANROADS miaka yote tunaomba pamoja na ya Kabila Isolo, Isawida kule Itilima hizi niombe tu waziri kama itakupendeza uzikasimu zihudumiwe na TANROADS kwa sababu uwezo wa TARURA ni mdogo sana kusimamia hizo barabara. Nikuombe sana hizi barabara ni barabara muhimu sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nina barabara kutoka Nyanguge Airport, barabara hii inapunguza msongamano kwa sababu ni barabara ambayo inatokea Musoma inapita Nyanguge kwenda Kayenze mpaka Airport inapunguza msongamano wa Jiji la Mwanza. Nalo hili liko kwenye upembuzi yakinifu na ninaamini kwamba imeshakamilika kwa ajili ya kuwekewa lami. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye Ilani ya CCM ukurasa 83, tumeahidi kwamba tutatengeneza kivuko cha Ijinga – Kahangala. Ninashukuru kwenye hotuba ninaona kuna maandalizi kivuko hiki ni muhimu sana kwa wananchi wangu wa Ijinga na Kahangala pamoja na visiwa vyote vya Ukerewe ambavyo vina vua samaki pamoja na mazao mengine itasadia sana kusaidia wananchi hawa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna daraja la Simiyu, daraja la Simiyu lile linaunganisha Simiyu na Mwanza katika barabara kuu ya kutoka Nairobi, Mwanza mpaka Rwanda, kwa hiyo, hili ni daraja muhimu sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimeona hapa maelezo hayajaniingia vizuri kichwani labda uangalie Mheshimiwa Waziri uone namna ya kulijenga daraja hili la Simiyu ili kuondoa adha ambayo wakati wote wananchi wanaosafiri watanzania wanapata shida sana. Ni pamoja na kukijenga kipande cha kutoka Nyanguge kwenda Ramadi kimeharibika kabisa na wewe unakijua hebu tuona namna ambavyo tunaweza kusaidia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru sana na niunge mkono hoja. Nawapongeza wote katika Wizara ya Ujenzi. (Makofi)