Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kishapu
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. BONIPHACE N. BUTONDO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi iliniweze kuchangia katika Wizara hii muhimu inayoshughulikia masuala ya miundombinu na hasa barabara zetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza, naomba niwapongeze Mawaziri; kwa maana ya Waziri pamoja na Naibu Mawaziri, Katibu Mkuu pamoja na watendaji wote katika Wizara hii. Kazi wanayoifanya ni kubwa lakini kusema kweli changamoto bado ni nyingi. Tunahitaji kuongeza nguvu zaidi kuhakikisha kwamba barabara zinapitika kwa sababu msingi wa uchumi wetu unahitaji sana kuimairisha miundombinu na hasa barabara.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunafahamu kama Tanzania hii tumeamua kusimama na kuamua Tanzania yetu iwe ni Tanzania ya viwanda. Viwanda hivi bila kuwa na barabara nzuri, uhakika wa viwanda vyetu kuzalisha na kuwa na ufanisi bado utaendelea kuwa ni hadithi. Pia tunafahamu kwamba bila barabara nchi yetu inategemea kilimo na kilimo ndiyo uti wa mgongo, wakulima wetu wataendelea kupata shida ya kusafirisha mazao na hivyo na wao wataendelea kutokupata tija katika shughuli yao ya kilimo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa ujumla shughuli zote za kijamii, ziwe huduma za afya na maeneo mengine kama hatujajipanga vizuri katika eneo hili la miundombinu bado Tanzania tutaendelea kusuakusua kwenda mbele katika shughuli za kimaendeleo. Kwa hiyo eneo hili ni eneo muhimu sana, hivyo Serikali nchi nzima bila kujali eneo fulani ama maeneo ya mijini, iwe vijijini ni lazima igawanye sawa hii keki kama Waheshimiwa Wabunge wenzangu ambavyo wamechangia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nataka nizungumzie katika bajeti ya hii ambayo tunaijadili, kusema ukweli katika eneo langu na hasa Kishapu unaweza ukaona ni kana kwamba hakuna barabara yoyote mpya ambayo imeweza kuwekewa fedha hapa. Kuna barabara ambayo hapa imeainishwa ni Barabara ya Kolandoto yenye urefu wa kilometa 62.4. Barabara hii ya kutoka Kolandoto ambayo inakwenda mpaka Mwanuzi hizi kilometa 62 sote ni mashahidi ni kilometa nyingi sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, unaweza ukaona labda ni fedha ambazo zimewekwa kwa ajili ya kushika kifungu ni bilioni mbili, bilioni mbili hizi zinakwenda kutengeneza kilometa ngapi? Ni mambo ambayo unaweza ukashangaa. Barabara hii ni barabara ambayo imekuwepo hata katika Ilani ya mwaka 2015 - 2020, lakini barabara hii haikuweza kutengewa fedha, lakini katika kipindi hiki imetengewa peke yake, jumla ya shilingi bilioni mbili peke yake. Fedha hizi ni kwa ajili ya kufanya nini?
Mheshimiwa Naibu Spika, wakati mwingine wananchi wetu wanaweza kufika mahali wakasema hii ni habari ya utani. Walikuwa wanataka majibu sawasawa katika hatua ile ya majumuisho ya mwisho ya Mheshimiwa Waziri kwamba nini mpango wa Serikali kwa sababu fedha hizi ni fedha za ndani lakini kama pengine kuna mikakati ya kupata fedha za nje nataka nipate majibu sawasawa na vinginevyo naweza nikaona kwamba wananchi wetu wanaendelea kuvunjika imani.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Rais, aliyekuwa Rais wetu Marehemu Dkt. John Pombe Joseph Magufuli alisema kwamba barabara hii ni lazima tuitekeleze na akawakumbusha wananchi tuliweka kwenye mpango katika kipindi kilichopita hatukutekeleza tunawahakikishieni tunakwenda kuitekeleza. Kwa hiyo hii ni ahadi ya Mheshimiwa Rais, lakini kwa sababu imo kwenye Ilani yetu ya Chama cha Mapinduzi ni lazima tujipange tuhakikishe kwamba barabara hii tunaitekeleza.
Mheshimiwa Naibu Spika, unaweza ukaona katika barabara nyingine ya Mwigumbi kwenda Maswa, hii ni barabara ya lami ambayo ipo tayari. Kitu ambacho kinasikitisha pengine labda nipate majibu katika, ukiangalia kwenye bajeti hii barabara hii imetengewa bilioni 50.3, sasa bilioni 50.3 hizi sijajua ni kwa ajili ya nini kwa sababu barabara hii ilishakamilika na kuna maeneo ambayo yalikuwa mabovu yalishafanyiwa matengenezo. Kwa nini fedha hizi zisingepelekwa kwenye barabara hii ya kutoka Kolandoto kwenda Mwanuzi kuja Kishapu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa haya ni mambo ambayo pengine nataka nijue hizi bilioni 50 ni kwa ajili ya kufanya nini? Kwa sababu tunaendelea kutoa pesa nyingi tunazipeleka kwenye barabara ambayo tayari ilishatengenezwa. Wakati mwingine inaweza ikaleta tafsiri ni mianya rahisi ya kuweza kutumia fedha bila kuwa na maswali mengi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo nilitaka nataka nizungumze hili, nipate majibu mazuri kwamba hii bilioni 50 kwa barabara hii ya Mwigumbi kwenda Maswa ni kwa ajili ya nini wakati barabara hii imekamilika. Juzi ilipata matatizo ikafanyiwa maintenance, lakini bado imewekewa fedha nyingi huku barabara ya Kolandoto kwenda Kishapu imewekewa bilioni mbili, nataka tafsiri na maelezo kuhusiana na hili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo nataka nizungumzie ni suala zima la uwanja wa ndege wa Shinyanga. Mkoa wa Shinyanga tuna shughuli za madini pale Mwadui, lakini tuna wachimbaji wadogo katika Mji wetu wa Maganzo pamoja na eneo lingine, eneo lote linalozunguka maeneo ya Maganzo na wananchi wanazo fedha, lakini Shinyanga tunalima pamba, habari ya fedha kwetu siyo tatizo. Kwa hiyo, habari ya usafiri wa ndege wala hata sisi kwetu siyo habari mpya kwa sababu ni watu ambao tunazo fedha bwana. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Uwanja wa Ndege wa Shinyanga imekuwa ni hadithi, hadithi. Kila mwaka kipindi kilichopita ilikuwemo kwenye Ilani, ilikuwemo sijui kwenye bajeti mbalimbali, uwanja wa Shinyanga unaenda kukarabatiwa, kila mwaka ni habari ya hadithi hizi. Jamani katika Wizara hii kuna matatizo gani? Uwanja huu mimi niwaambieni hata kipindi kile ambacho kiwanja hiki kilikuwa kinafanya kazi, kati ya viwanja ambavyo vilikuwa na abiria wengi sana kipindi cha nyuma, kimojawapo ni Kiwanja cha Shinyanga. Sasa sijajua kama wanapiga hesabu ama tunaendelea kujenga viwanja vingine tu bila kuangalia uhalisia na historia ya viwanja vipi ambavyo vinakuwa na wateja wengi.
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nipate majibu mazuri kwamba kiwanja hiki kinakwenda kutengenezwa kweli? Unaweza ukaangalia fedha zilizowekwa peke yake ni bilioni 3.6, naziona ni fedha kidogo na kiwanja kile tumekiacha kwa muda mrefu, kilikuwa na uharibu mdogo, lakini viwanja vya aina hii vimeendelea kuharibika, kwa rafiki yangu kule Mhata kuleā¦
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Butondo kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Esther Matiko.
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nimpe taarifa Mheshimiwa mzungumzaji kwamba ni kweli kabisa nakubaliana naye kwamba Serikali haiangalii viwanja ambavyo vina; mosi, vinakuwa vina historia lakini pia vinaweza kuchangia pato kubwa kwenye uchumi wa Taifa, mfano uwanja wa ndege wa Musoma ambapo anatoka Baba wa Taifa, tuna madini kule, tuna ziwa, tuna Mbuga za Wanyama na vitega uchumi kibao lakini mpaka sasa hivi unasua sua tu, nilikuwa naomba nikupe hiyo taarifa Mheshimiwa. (Makofi)
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Butondo unapokea taarifa hiyo.
MHE. BONIPHACE N. BUTONDO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kweli kwa sababu hoja ya Mheshimiwa Matiko ni ya maslahi mapana kabisa ya Taifa letu nimeipokea taarifa yake.
Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa nataka nizungumzie kwa Mheshimiwa Mhata, Kiwanja kile cha Masasi ni aibu, ni moja kati ya maeneo ambayo nilitaka nizungumze kwa uwazi. Kiwanja kile kilifikia hatua mbaya, hata kile kipindi tunakwenda kumhifadhi cha mzee wetu, ilifanyika kazi ya kuchoma nyasi zile, ndiyo ile helikopta ikatua pale. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunavisahau viwanja vikongwe na viwanja ambavyo tumekuwa tukisema mwaka kila baada ya mwaka kwamba vitakwenda kukarabatiwa. Hii ndiyo habari ambayo wanazungumza wenzangu, Mheshimiwa Mwenisongole amezungumza kwamba keki hii
ni lazima tuigawanye katika usawa. Kwa hiyo nataka niiombe sana Wizara, tusije tukajenga tafsiri ya kwamba kwa kweli kuna baadhi ya maeneo watu wengine wanapendelewa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hata katika hotuba hii maeneo mengine tusingependa kuyafungua na kuzungumza, baadhi ya maeneo yamepewa fedha tena fedha nyingi, lakini baadhi ya maeneo mengine hatuna fedha, pengine inaweza ikaleta tafsiri nyingine.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo nataka hili nilizungumze naikumbusha Wizara kwamba iwe makini kuhakikisha kwamba maeneo yote hasa ya msingi yanatazamwa na fedha zinapelekwa kwa ajili ya kusaidia wananchi katika maeneo hayo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine ambalo nataka nilizungumzie, ni kuhusiana na daraja. Lipo daraja moja ambalo limejengwa katika Jimbo langu la Kishapu. Daraja la Buzinza, Kishapu - Buzinza na daraja lile linaunganisha pia Wilaya ya Igunga. Daraja hili limejengwa kwa thamani ya shilingi bilioni 2.3, lakini tangu daraja hili litengenezwe leo ni zaidi ya miaka mitatu daraja hili limekamilika, lipo katika Mto Manonga, lakini baada ya kukamilika daraja hili halifanyi kazi kwa sababu nyakati za masika kushoto na kulia yaani unapokuwa unavuka na unapokuwa unavuka upande mwingine mto ule unatakiwa ujengelee sasa barabara. Kivuko cha kutoka huku na kivuko cha kutoka huku, kwa sababu ule ni mto.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa ni sawa na kwamba Serikali imekwenda kutupia zile fedha halafu barabara hiyo haina maana yoyote. Niombe sana Wilaya ya Igunga na Wilaya ya Kishapu iunganishwe kupitia daraja hili vinginevyo ni sawa na kwamba tumezimwaga zile fedha na hakuna maana yoyote ya kupeleka hizo fedha. (Makofi)
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
NAIBU SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa, kengele ya pili imegonga.
MHE. BONIPHACE N. BUTONDO: Mheshimiwa Naibu Spika, ilikuwa ya kwanza.
NAIBU SPIKA: Imeshagonga ya pili, ahsante sana.
MHE. BONIPHACE N. BUTONDO: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja. (Makofi)