Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa mwaka wa Fedha 2016/2017

Hon. Taska Restituta Mbogo

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. TASKA R. MBOGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kuniona. Kwa sababu ni mara yangu ya kwanza nasimama mbele ya Bunge hili Tukufu, naomba nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa uhai na leo hii mimi Taska Restuta Mbogo nimesimama hapa nachangia hoja. Napenda kuwashukuru wananchi wangu wa Mkoa wa Katavi hususan akinamama walionichagua na kuniwezesha mimi kuwa Mbunge wa Viti Maalum ndani ya Bunge hili Tukufu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda niwapongeze Waheshimiwa Wabunge wote wa vyama vyote mliomo humu ndani, mliofanikiwa kuja ndani ya Bunge hili Tukufu. Napenda nimpongeze Rais Mheshimiwa Dkt. John Joseph Pombe Magufuli kwa kuchaguliwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na napenda nikipongeze Chama cha Mapinduzi kwa kupata ushindi mkubwa na kuongoza Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda nimpongeze Mheshimiwa Waziri wa Viwanda kwa hotuba yake nzuri, lakini ninayo machache ya kuchangia kuhusu hotuba yake. Kwanza kabisa, napenda nichangie suala la viwanda. Tunaposema kwamba tunakwenda kwenye nchi ya viwanda tunatakiwa tuwe na maji ya kutosha, tuwe na miundombinu bora kama barabara, reli ambazo zinapitika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikitolea mfano mdogo tu, kule kwetu Katavi hatuna miundombinu ya barabara mizuri, reli yenyewe ni ya kusuasua, siyo reli ambayo inaweza ikabeba mzigo mkubwa wa kiwanda. Kwa maana hiyo ni kwamba, hata kama kiwanda kinajengwa kule, bado tutakabiliwa na miundombinu mibovu ambayo iko katika Mkoa wetu wa Katavi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Katavi inaunganika na Mkoa wa Rukwa na Mkoa wa Kigoma, lakini huwezi kusafirisha mazao kutoka Mkoa wa Katavi kuyapeleka Mkoa wa Kigoma kwa barabara kwa sababu barabara hiyo haipitiki, ni barabara ya vumbi.
Pia huwezi ukasafirisha mazao ukayatoa pale Mkoa wa Katavi ukayapeleka Mkoa wa Rukwa kwa sababu barabara ile ni ya vumbi ina vipisi vipisi tu vya lami ambavyo havijakamilika. Kwa hiyo, kama tunakwenda kwenye nchi ya viwanda, nchi yetu ya Tanzania tunapaswa pia tuangalie miundombinu hiyo iwe bora, maji yawepo ya kutosha. Kule Katavi ni pale Mjini tu ambako ndiyo kuna maji, lakini sehemu nyingine wananchi wanatumia bado maji ya visima. Kwa hiyo, naomba suala hili la maji pamoja na barabara liangaliwe kabla ya hivyo viwanda. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, Mkoa wetu wa Katavi ni Mkoa ambao hauna kiwanda hata kimoja; na tangu nchi hii imeumbwa hakujawahi kujengwa kiwanda hata kimoja, hata kiwanda cha kiberiti hakuna, wala cha sindano. Kwa hiyo, napenda Mheshimiwa Waziri anapokuja kutoa ufafanuzi, labda atuambie kwamba kule Katavi ataanza kutujengea kiwanda cha kutengeneza nini? Kwa sababu Katavi tunazo fursa nyingi; sisi ule Mkoa tunayo asali ya kumwaga, naweza nikatumia neno “ya kumwaga.” Tunazo karanga nyingi sana; tunayo tumbaku; tunao mpunga unalimwa. Ina maana mchele kule kilo ni shilingi 1,200/=, tunayo mahindi ambayo mpaka yananyeshewa na mvua nje. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Serikali iangalie utaratibu wa kujenga viwanda vinavyohusiana na hayo mazao. Kwa Mfano, Serikali ikijenga Kiwanda cha Kuchakata Asali, asali itapakiwa vizuri, itapelekwa nje. Asali inaleta pia nta; ile nta ni zao zuri sana ambalo likipelekwa nje ya nchi linaweza likaleta mapato kwa nchi yetu ya Tanzania. Nta inatumika kwa mambo mengi; inatumika kutengeneza mabegi, viatu; ina manufaa mengi ambayo ni pamoja na gundi zinazotumika maofisini. Mazao hayo yangeweza kuongeza kipato cha mwananchi wa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukija kwenye suala la tumbaku; inalimwa kule Katavi, Tabora lakini Kiwanda cha Tumbaku kipo Morogoro. Sasa inamkatisha tamaa mwananchi kulima tumbaku. Tumbaku yenyewe ina grade 72. Yule classifier anapofika pale anai-grade ile tumbaku, anaweza akamwambia mtu kwamba hii tumbaku yako nanunua kilo moja kwa sh. 500/=, lakini kama Kiwanda cha Tumbaku kingekuwa karibu, kwa mfano, kingejengwa Tabora au hapo Katavi, kingeweza kuwanufaisha wananchi wote ambao wanalima hilo zao la tumbaku.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia naomba Mheshimiwa Waziri angefikiria suala la kuleta kiwanda cha kutengeneza mafuta kama ya alizeti. Tunalima alizeti sana kule, pia tunalima karanga nyingi, tusingeweza kuagiza mafuta ya nje hayo ambayo yanakuja yamechakachuliwa hujui hata kama ni mafuta yametengenezwa na nini, unaambiwa tu ni vegetable oil. Tungeweza kutumia mafuta ya alizeti, tukatumia mafuta ya karanga na wananchi wakapunguza cholesterol mwilini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Mikoa yetu ya Katavi, Tabora na Rukwa ni Mikoa ambayo ina ardhi safi sana, ambayo kuna sehemu nyingine ardhi ile tangu imeumbwa na Mwenyezi Mungu hamna binadamu ambaye ameweza kukaa. Naomba Mheshimiwa Waziri wawekezaji wanapokuja, jaribuni kuwapeleka pia mikoa ya pembezoni. Najua mnatuambia kwamba ile ni mikoa ni ya pembezoni ya mwisho wa dunia, lakini ni mikoa ambayo inazalisha mazao mengi sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wawekezaji wanapokuja kutaka kuwekeza Tanzania msiwape tu ramani za kusema kwamba wawekeze Dar es Salaam au wawekeze Arusha, wapelekeni pia na mikoa ya pembezoni. Mikoa ya pembezoni kwa mfano kule Katavi, hiyo ardhi mwekezaji anapokuja, akichukua akalima mahindi yake akatengeneza unga na pia hayo mahindi akatengeneza mafuta ya mahindi ambayo ni mazuri sana kwa kupikia chakula, ambapo pia mwekezaji angeweza kuongeza pato na kuweza kuajiri vijana na kupunguza matatizo ya vijana ambao hawana kazi kwa sababu kiwanda kitakuwa pale, kitaajiri wale vijana ambao watafanya kazi pale. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Katavi pia unazo mbao nyingi. Hili tatizo la Madawati ambalo sasa hivi Serikali inakabiliana nalo, lingeweza kutatuliwa. Kwa mfano, kama Serikali ingekuwa imewekeza ikaleta Mwekezaji mmoja akajenga Kiwanda cha Mbao kule Katavi ambapo kunapatikana mbao nzuri sana ya mninga ambayo hata mdudu anaogopa kuitoboa, ina maana madawati yangetengenezwa kwa wingi kwa sababu mbao zinapatikana nyingi sana, tungeweza kuondoa tatizo la madawati ambalo linawakabili wanafunzi na watoto Tanzania hii yote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mbao ni nyingi sana kule Katavi, Tabora na Rukwa; pia asali ni nyingi sana maeneo hayo. Naomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja na majumuisho atuambie ni lini atatuletea hivyo viwanda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda pia kumwambia Mheshimiwa Waziri kwamba hao Maafisa Biashara ambao wameajiriwa kwenye Ofisi za Halmashauri, wajaribu kuwa wanaenda kutoa elimu ya biashara kwa wananchi, kwa sababu muda mwingi wanautumia ofisini na kutumia computer. Wanatakiwa Waonane na wananchi wawape elimu ya biashara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu wao wanakuwa wana-chat kwenye computer, wanataka kufanya kazi kwa mtandao, lakini mwananchi wa kawaida hayuko kwenye computer, anataka asikilize ile elimu ya biashara na hiyo elimu iweze kumsaidia yeye na kuweza kujiinua kwenye biashara yao. Kwa sababu pia wao wanalipwa mshahara kwa ajili ya kuwa Maafisa Biashara wa Halmashauri, lakini huwa siwaoni wakitoa hiyo elimu ya biashara kwa wananchi, wanatumia muda mwingi kukaa ofisini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.