Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kaliua
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. ALOYCE A. KWEZI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwanza, naomba nichukue nafasi hii kuwapongeza Wizara hii ya Ujenzi kwa kazi nzuri ambazo wanalifanyia Taifa letu na hususani Mkoa wa Tabora ambao kwa kweli sehemu kubwa tunakwenda vizuri. Nisisite kumpongeza Mheshimiwa Waziri, Katibu Mkuu wake pamoja na Meneja wetu wa Mkoa wa Tabora. Meneja yule kwa kweli ningeomba Wizara pengine hata mmuandikie barua ya pongezi kwa kazi nzuri ambazo anaziendeleza katika Mkoa wetu wa Tabora. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi yangu maombi tu, pale Kaliua barabara ya kutoka Urambo imepita Kaliua na sasa ipo mpaka karibia na Usinge, lakini bypass ya kwetu pale ni kilometa 5.5. Kwa sababu barabara imepita kulia, imeacha Kata za Ushokola, Kaliua Mjini pamoja na Kasungu, maeneo haya yote naomba hii barabara ambayo inapita katikati ya Mji na Stendi na wafanyabiashara wakubwa wa Kaliua pale tuwasaidie tuweze kujenga ile bypass ili waone faida nzuri ya utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili ambalo naomba ni kuanzia Usinge, wanapojenga ile barabara ya Kazilambwa – Chagu, kutoka pale ni kilometa 4 kuingia Usinge Mjini. Naomba na penyewe wasije wakasahau kuhakikisha kwamba hata kama siyo mwaka huu, wakianza mwaka huu Kaliua hizo kilometa 5.5 basi kwa Usinge mwakani wanaweza wakaweka kuingia mjini kwa sababu Usinge ni sehemu kubwa na ina kata karibu tatu na karibia asilimia 23 ya wakazi wa Kaliua wanapatikana Usinge pamoja na Kata ya Usenye. Kwa hiyo, tunaomba hizo lami kilometa 5 waweze kutusaidia pale Kaliua Mjini na kule kilometa nne. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, la tatu, naendelea kuwashukuru, kuna barabara nimeona kubwa kweli ya kutokea Kahama – Ushetu – Igwisi – Kazaroho – Kaliua – Zugimlole kilometa 60 mpaka Mpanda, tumeona pale mmetuwekea daraja. Kwa awamu hii mimi naunga mkono kwa kweli tujengeeni kwanza daraja, mmetuandikia hapa mnatutafutia fedha, hizo fedha mhakikishe mnazipata ili barabara hii ya kiuchumi ya kutokea Mpanda kupita Kaliua mpaka Kahama iweze kukamilika. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini la mwisho, pale Kaliua ni junction abiria wanaotumia treni kutoka Kigoma wakifika Kaliua wakishuka wanatumia treni inayokwenda Mpanda; eneo lile naomba waongeze muda wa treni kwa sababu muda wa kusimama treni Kaliua ni mchache, ni dakika kumi na ile ni junction ina abiria wengi sana. Kwa hiyo, naomba waboreshe pale kwa kuongeza muda ili uwe wa kutosha. Jambo la pili pale pale ni tiketi, Kaliua tiketi hazitoshi, naomba watupe tiketi za kutosha sisi bado tunatumia sana usafiri wa treni. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini la tatu hapo hapo, ni usimamizi kwenye vile vituo vidogo, kituo kama kilometa 34, kilometa 48 mpaka Mpanda. Naomba maeneo hayo toeni muda wa kutosha kwa sababu treni inasimama dakika moja unaona imeondoka, mnasababisha ajali. Kwa hiyo, naomba wananchi wa maeneo hayo waweze kuongezewa tiketi na muda wa kutosha kwa ajili ya kuhakikisha wanasafiri vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nashauri pia Wizara pamoja na kazi nzuri walizofanya, ile reli ya kutoka Kaliua kwenda Mpanda ni mbovu mno, wanatumia saa kumi. Sasa saa 10 kwa kilometa chache hizo karibu kilometa 180, naomba waiboreshe wakati tunasubiri hiyo Standard Gauge ambayo inakuja, waikarabati reli hiyo vizuri tupunguze hata muda wa kusafirisha mazao yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kuyasema hayo, nirudie kuipongeza sana Wizara hii kwa kazi nzuri wanazozifanya lakini nawaomba wasisahau kurekebisha zile kilometa 5 za Kaliua mjini pamoja na taa za barabarani, maana wale wananchi wakifika tu Urambo, wanaona Urambo bypass yao ipo safi na taa za barabarani wanauliza Mbunge yupo wapi nami napenda nirudi awamu ijayo. Ndugu zangu chondechonde nawaomba kabisa kwenye bajeti hii muendelee kuwa wasikivu na kunihakikishia mmeniwekea hizo kilometa 5. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kuyasema hayo, nawashukuru sana, naunga mkono hoja. (Makofi)