Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. CONCHESTA L. RWAMLAZA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia kidogo katika bajeti iliyo mbele yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kuzungumzia kuhusu fidia kwa viwanja vya wananchi wa Kata ya Mkonze lile eneo la Miganga West na Miganga East ambapo kunapita njia ya reli ya SGR. Mara ya kwanza walitathmini wakalipa watu lakini wametathmini mara pili mpaka sasa hivi tayari barabara zimeanza kupita katika viwanja vya watu lakini fidia kwa wananchi ambao wametathminiwa mara ya pili haijafanyika.
Kwa hiyo, tunaomba Wizara ituambie ni lini wananchi hawa watalipwa ili waweze kununua viwanja vingine hasa kwa kuzingatia kwamba viwanja hapa Dodoma ni ghali sana. Kwa hiyo, wanapocheleweshewa fidia watashindwa kununua viwanja vingine ili waweze kuendelea na maisha yao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo langu la pili, napenda kuongelea Bukoba Vijijini Jimbo ambalo nimegombea mimi na nimesema ni lazima nitasaidia wananchi hawa ambao kwa muda mrefu wamekosa mtu wa kuwatetea. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, Bukoba Vijijini ni Jimbo ambalo limetelekezwa kwa muda mrefu tangu uhuru. Wananchi wa Bukoba Vijijini ni wakulima wa migomba, ni wakulima wa kahawa na sasa hivi wamepanda miti sana. Kwa hiyo, kuna mazao mengi sana, kabisa kabisa ya mbao. Tangu uhuru hatujawahi kupata barabara ya lami. Bukoba Vijijini imezungukwa na Jimbo la Bukoba Manispaa, Misenyi, Muleba Kaskazini na Karagwe. Kwa hiyo, hakuna mahali popote ambapo pamefunguka ili watu waweze kupitisha mazao yao waweze kuendeleza uchumi wao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimeangalia katika kitabu cha...
MHE. DKT. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.
MHE. CONCHESTA L. RWAMLAZA: …cha Waziri ukurasa wa 167.
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Conchesta Rwamlaza kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Ritta Kabati.
T A A R I F A
MHE. DKT. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Nilikuwa nataka tu nitoe taarifa kwa mchangiaji kwamba Jimbo la Bukoba Vijijini halina mtetezi wakati kuna Mbunge wa Jimbo ambaye siku zote huwa tunamwona anauliza maswali.
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. (Makofi/Kicheko)
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Conchesta Rwamlaza, unapokea taarifa hiyo?
MHE. CONCHESTA L. RWAMLAZA: Mheshimiwa Naibu Spika, mimi sipokei kwa sababu Mbunge amekuwepo zaidi ya miaka 15 na hatuna barabara. Kwa hiyo, sasa mnataka niseme nini? Hebu niachie nitetee wananchi, ndiyo kazi ya Wabunge iliyotuleta hapa. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kitabu cha Waziri ukurasa wa 167 kuna barabara zimeandikwa hapo, naomba Waziri anisikilize, muda ni mchache. Kuna barabara ya kutoka Mutukula – Bukoba – Mtwe – Kagoma, wametenga fedha, shilingi bilioni moja kwa ajili ya upembuzi yakinifu. Sasa naomba niulize, hii barabara ipo ya lami, unafanya upembuzi gani? Mnapembua nini, barabara ambayo imeshatengenezwa? Pale katika hiyo shilingi bilioni moja, kuna barabara ambayo inatoka Bukoba Mjini – Businde – Maruku – Kanyangereko; pia, kuna barabara ya Kanazi kutoka Kyetema – Ibwera – Katoro – Kyaka; naomba niulize, hii barabara ambayo inafanyiwa upembuzi usioisha, inakamilika lini? Kwa sababu watu wa Bukoba Vijijini tunaumia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niongezee kitu kingine; kuna daraja linaitwa Karede. Daraja hilo haliwezi kupitisha mizigo tani 40 na watu wote ambao wanafanya biashara ya mbao wanapaswa kuzunguka sasa, kutoka eneo hilo la Ibwera, hawawezi kupitisha mizigo katika daraja lile, wanapaswa wazunguke mpaka Kyaka kwenda Misenyi, yaani wanakwenda kwenye Jimbo lingine halafu warudi Bukoba Manispaa halafu waje kuelekea njia ya Biharamulo. Unaweza kuona adha tunayoipata. Kwa hiyo… (Makofi)
MHE. DKT. JASSON S. RWEIKIZA: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Conchesta Rwamlaza, Mheshimiwa Rweikiza Mbunge wa Bukoba Vijijini, anataka kukupa taarifa.
T A A R I F A
MHE. DKT. JASSON S. RWEIKIZA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimpe taarifa mzungumzaji kama ifuatavyo: kwamba barabara ya Kyetema – Ibwera – Katoro hadi Kyaka imo kwenye Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka huu; na hivi ninavyozungumza, tumepata shilingi bilioni moja za upembuzi yakinifu. Barabara ya Busimbe kupita Rugambwa kwenda Maruku hadi Kanyangereko imo kwenye Ilani ya uchaguzi na hivi ninavyozungumza ina fedha ya upembuzi yakinifu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ya kuanzia Bukoba Mjini kupita Kata tano hadi Rubafu imejengwa kwa asilimia 51 kwa kiwango cha lami katika miaka hii mitano tunayoendelea nayo. Barabara ya kuanzia Kyetema - Katerero hadi Kanyinya ina lami na kazi zinaendelea kwa
kiwango kikubwa katika Jimbo la Bukoba Vijijini. (Makofi/ Kicheko)
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Conchesta Rwamlaza, unapokea taarifa hiyo kutoka kwa Mbunge wa Jimbo la Bukoba Vijijini?
MHE. CONCHESTA L. RWAMLAZA: Mheshimiwa Naibu Spika, sipokei, lakini ninachosema, mnaona ushindani wa kisiasa ulivyo mzuri! Kwa hiyo, tunashindana na wananchi watafute maendeleo; na ndiyo kazi ya kisiasa. Kwa hiyo, sasa mwenzangu, mtani wangu wa jadi na wewe sasa umetoa maneno leo ili watu wasije wakakuita bubu. Kwa hiyo,…(Makofi)
MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: Usiseme uongo.
MHE. CONCHESTA L. RWAMLAZA: Mheshimiwa Naibu Spika, tunachotaka ni Jimbo la Bukoba Vijijini liweze kupata barabara.
MBUNGE FULANI: Sawa sawa. (Makofi)
MHE. CONCHESTA L. RWAMLAZA: Mheshimiwa Naibu Spika, tunachotaka ni wananchi wa Bukoba Vijijini waweze kuendeleza maisha yao. Kwa hiyo, hapa haya mambo hili Bunge tunaweza kusema is a political policy, lakini lazima tuseme na lazima tuseme. Naye akisema, aseme yake, mimi nasema yangu. Kwa hiyo, niliyoyaona kama anaona udhaifu, ni lazima niuseme na lazima ziwepo ajenda. Kwa hiyo, lazima Bukoba Vijijini tuisemee kuhakikisha kwamba Jimbo hili linapata maendeleo yake. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, nije sasa kwa TARURA. Barabara nyingi za Kata katika Jimbo la Bukoba Vijijini ni mbovu na TARURA haina uwezo wa fedha. Sasa Halmashauri kwa Sheria ya TARURA wanapashwa na wao kuchangia katika kutengeneza barabara, lakini uwezo wa kutoa michango haupo. Mimi napenda kushauri kwamba sasa Serikali ifikirie namna ya kurejesha baadhi ya mapato, yaani vile vyanzo vya mapato vilivyowekwa na Serikali, vinaweza kurejeshwa ili na Halmashauri yenyewe iweze kupata pesa za kusaidia TARURA. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ukienda kwenye Kata za Kibirizi; na ninaomba huyu mtani mwenzangu anisikilize. Kibirizi…
MBUNGE FULANI: Ehe!
MHE. CONCHESTA L. RWAMLAZA: …Ruhunga, Chamlaile, ndugu yangu ukipita na gari unatengeneza barabara wewe mwenyewe kwa gari yako. Anajua, kwa mfano nimwambie kutoka Kibirizi kwenda Kamuli…
MBUNGE FULANI: Ehe!
MHE. CONCHESTA L. RWAMLAZA: …kwenda Akashalaba, wewe ulipitaje pitaje? Lazima utengeneze barabara wewe mwenyewe kwa gari yako. Kwa hiyo, ninachoomba kusema ni kwamba Jimbo la Bukoba Vijijini halijakaa vizuri, barabara siyo nzuri na hazipitiki kwa mwaka. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. (Makofi/ Kicheko)