Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

Hon. Nashon William Bidyanguze

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kigoma Kusini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

MHE. NASHON W. BIDYANGUZE: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nikushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia kwenye Wizara hii muhimu, Wizara ya Miundombinu. Naomba nilete masikitiko yangu kwa barabara kubwa hii ambayo inatoka Tabora kwenda Kigoma. Kwanza, naomba nichukue nafasi hii nimpongeze na kumshukuru Rais wa Awamu ya Nne, ndiye aliyetuunganisha na mikoa mingine sisi Kigoma pale alipotutengenezea Daraja la Mto Malagarasi na likaitwa Kikwete. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kipo kipande kilibaki cha kilometa 51 ambacho kinatokea Mpeta baada ya kuvuka Daraja la Mheshimiwa Kikwete mpaka Uvinza ni kilometa 51, hili eneo limekuwa ni tatizo kwa muda mrefu sana. Unatoka Dar-es-Salaam, Dodoma, Tabora, unakwenda mpaka Kigoma lakini eneo hilo ndilo limebaki na vumbi, ni jambo la ajabu sana. Wananchi wanajiuliza hivi kuna nini? Kwa hiyo, naomba Waziri pamoja na kwamba nimeona kwenye bajeti yake ameitaja, lakini naomba nisisitize na wananchi wasikie kwamba barabara hiyo nimeitaja, ni kero kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia ipo barabara nyingine ya Uvinza kwenda Kasulu nayo ni kero sana na ni barabara fupi sana. Kwa kweli, naomba katika bajeti hii hii barabara nayo iweze kuangaliwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia ipo nyingine inatoka Uvinza kwenda Mpanda kupita Mishamo. Hii nayo ni barabara ambayo kwa kweli ni ya kimkakati, ikiwekwa lami na sisi Kigoma tutakuwa tumeondokana na lawama na malalamiko kama ya wale wenzetu waliokuwa wanasema wametengwa. Sisi tumetengwa kwa sababu tumetengenezewa barabara za lami lakini vipande vimebaki. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Jimbo langu la Kigoma Kusini, wewe ni shahidi, ulipokuwa ukitokea kwenye msiba wa marehemu Mbunge wetu ambaye alitangulia mbele ya haki, Mheshimiwa Nditiye, wakati unarudi kutoka Kigoma kwenda Mbeya ulipotea. Ulichukua barabara ambayo sio yenyewe, ile barabara ni ya Simbo – Kalya, ulikwenda kurudia kwenye kivuko cha pale kwenye Mto Malagarasi, pale ndiyo uliposhtuka kwamba barabara ile sio yenyewe, nakupa pole sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuja kuambiwa kwamba Naibu Spika alipotea alidhani hii barabara inakwenda Mbeya. Ukweli barabara ile kama itajengwa vizuri inayo access ya kwenda Mbeya, ulikuwa hujakosea, sema kule mbele ungepata shida sana. Barabara ambayo ungepita badaye ni kutoka Rukoma kwenda Ikuburu na Rubalisi baadaye inapita Mwese halafu ndio ungeingia sasa Mpanda kwenda sasa Kalya. Hii barabara ni muhimu sana kwa sababu ni barabara ya mkoa lakini inakwenda kuishia Kalya peke yake. Ni barabara nzuri bado tunatumia changarawe na kwa kweli kupitia nafasi hii nimpongeze Meneja wa TANROADS wa Mkoa wa Kigoma Bwana Eng. Choma, hii barabara anaingalia sana lakini bado kuna vipande ambavyo vina shida.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa kengele imeshagonga.

MHE. NASHON W. BIDYANGUZE: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimalizie kwa kusema tu kwamba Daraja la Mto Malagarasi pale ulipokwamia ni tatizo, lakini nashukuru Wizara imetenga shilingi milioni 250 kwa ajili ya upembuzi yakinifu. Nina imani daraja hilo litaenda kujengwa. Naomba niunge mkono hoja. (Makofi/Kicheko)