Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa mwaka wa Fedha 2016/2017

Hon. Sabreena Hamza Sungura

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. SABREENA H. SUNGURA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuweza kuchangia katika Wizara ya Viwanda na Biashara. Kwa kuwa ni mchango wangu wa kwanza napenda kutoa shukurani za dhati kwa chama changu kwa kunirudisha Bungeni kwa awamu nyingine ya pili, ahsanteni sana ninawaahidi ukombozi mpaka pale nchi yetu kitakapoeleweka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili; napenda kuchukua fursa hii kulaani vitendo vya kikatili na udhalilishaji vinavyofanywa na Serikali ya Chama cha Mapinduzi vya kupiga, kudhalilisha na kuburuza Wabunge ndani ya jengo takatifu, jengo linalotunga sheria, jengo linalofanya maamuzi katika nchi hii. Ni kitendo cha udhalili na ni laana kwa Serikali ya Chama cha Mapinduzi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nije sasa kwenye suala zima la viwanda na biashara. Kinachoendelea humu ndani ni maigizo. Ni ndoto za alinacha kusema mtafanya mapinduzi ya viwanda na biashara ilhali zaidi ya asilimia 50 ya Watanzania hawana umeme, hawana maji safi na salama.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ushahidi ni Mkoa wangu wa Kigoma, Mkoa ambao tunapata umeme kwa kutumia jenereta ambazo haziwezi ku-run heavy industry. Kwa hiyo tukisema tutaanzisha viwanda, alipita Mheshimiwa Rais Magufuli kwenye kampeni akasema kwamba atahakikisha Dangote anakuja kufungua kiwanda cha cement Mkoa wa Kigoma, swali langu ni kwamba kiwanda hicho kitafunguliwa kwa umeme upi? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Kigoma hauna barabara za maana kwa maana ya barabara za kupitika. Leo hii naongea kuna wananchi walikwama zaidi ya saa 48 njiani kwa ubovu wa barabara. Mkoa hauna reli yenye standard gauge, mvua zikinyesha inakuwa ni shida. Mkoa hauna ndege za uhakika, Mkoa hauna boti ama meli za kisasa ambazo zitatusaidia kupeleka bidhaa mbalimbali katika nchi nne ambazo zinaungana na Mkoa wetu wa Kigoma. Ni viwanda gani hivyo mtakavyoleta kujenga, nchi imejaa urasimu? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilisikia Mheshimiwa Rais anasema kwamba kuna mishahara hewa, lakini nafikiri hajapewa information za kutosha, siyo tu mishahara hewa kuna fidia hewa nchi hii. Nimeshuhudia baadhi ya wananchi maeneo mbalimbali wakilipwa fidia hewa, mtu anahonga shilingi milioni 10 anapewa milioni 60. Sasa kama kuna fidia hewa hakuna kiwanda kitakachojengwa katika mazingira hayo, mnajidanganya na Serikali inajua kama fidia hewa zipo lakini kwa kuwa ni miradi yenu hamchukui hatua zozote za kudhibiti. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo ningependa kulizungumzia ni kuhusu mitaji. Ni wajibu wa Serikali kuwawezesha wananchi wake kupata mitaji ya kuendeleza viwanda vidogo, viwanda vya kati na viwanda vikubwa. Mheshimiwa aliyemaliza kuongea hapa, amezungumzia matusi ambayo amepata mwekezaji wa ndani, mzalendo ndugu yetu Mengi. Lakini juzi juzi tumesikia Bakhresa naye akiambiwa kwamba ni mkwepa kodi, unaweza kukuta uhuni ule umefanya na management ya watu wachache tu katika kiwanda kile. Sasa nasema ni wakati muafaka wa Serikali kuweza kuwapongeza na kuwashikilia wawekezaji wa ndani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mtu kama Ndugu Mengi, mtu kama Ndugu Bakhresa na familia zao, rasilimali walizonazo wakisema waweke kwenye fixed deposit kwa mwaka fedha, watakayopata matatizo yao na familia zao wanamaliza, lakini wanawekeza kwa niaba ya Watanzania. Please Watanzania wanaojitokeza kwenye uwekezaji, Serikali iwaunge mkono. Kwanza kwa kutoa ardhi, pili kwa kutoa sheria zozote ambazo ni kandamizi kwao, lakini tatu kwa kumaliza migogoro ya fidia kwa wananchi mbalimbali na nne kuhakikisha kwamba mnawapa ruzuku. Serikali isiwe kikwazo kwa wawekezaji katika sekta ya viwanda, biashara na uwekezaji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri wa Viwanda, napenda kuzungumzia zao la mchikichi. Mkoa wa Kigoma nilizungumzia hapa miaka 40 iliyopita tuliwapa mbegu nchi ya Malaysia, Malaysia sasa hivi inafanya vizuri kwenye zao hili kutokana na kuliendeleza. Ajabu na aibu ya Tanzania, zao hili halijafanyiwa utafiti, zao hili halina bodi wala Serikali hamna mpango madhubuti wa kuendeleza zao la mchikichi. Tunaiomba Serikali ituambie ni lini mtawekeza nguvu za kutosha kwenye zao hili kwa sababu zao hili linazalisha bidhaa zaidi ya 20 ndani ya zao moja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa uchache naweza nikataja mafuta ya mawese, naweza nikataja mafuta ya mise, zao hili linazalisha sabuni, zao hili linazalisha chelewa, zao hili linazalisha majani ambayo yanafunikia mapaa katika nyumba zetu, lakini zao hili linazalisha makafi ambayo tunatumia kama nishati ya kupikia. Serikali ya Chama cha Mapinduzi miaka 54 ya Uhuru haijaona umuhimu wa zao hili na kuweza kuliendeleza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri nilizungumzia kuhusu bandari. Kulikuwa kuna kelele za sukari, imefikia mpaka shilingi 3,000, shilingi 3,500, shilingi 4,000 mpaka shilingi 5,000 baadhi ya maeneo, lakini wakati Serikali imelala hapa Dodoma, sukari mbovu inapitishwa kwenye mwambao kuanzia Pangani mpaka maeneo ya Mbweni kule Dar es Salaam. Bandari bubu zimejaa, Serikali inajua, watu wanakusanya kodi, Jeshi la Polisi liko pale, Serikali haipati mapato. Hii ni Serikali inafanya kazi kwa utashi ama ni Serikali inafanya kazi kama panya road? Lazima muamke, lazima muwe makini, fedha za nchi zinapotea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wa Tanzania sasa hivi wengi ukienda hospitalini figo zinafeli kwa sababu ya kutumia sukari za KK.
Mheshimiwa Mwenyekiti, akina mama wanaotengeneza juice na vijana na akina baba, kijiko kimoja cha sukari kinahudumia ndoo mbili za lita 20. Wananchi wanafeli figo na wakienda katika hospitali yetu ya Taifa Muhimbili hakuna matibabu wanayopata ya ziada. Napenda kusema kwa kusikitika niliwahi kukutana na mgonjwa mmoja ambaye figo zake zimefeli na sababu kubwa ikiwa ni hizi juice ambazo zinaungwa KK. Mgonjwa yule figo zimefeli kwa sababu ya sukari hizi lakini kilichotokea gharama za matibabu zimekuwa ni kubwa akawaomba wauguzi arudi nyumbani nikapumzike nisubiri kuonana na muumba wangu kwa sababu siwezi kukidhi gharama hizi za matibabu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo mnaweza mkaona kwamba sekta hii inaathiri vipi sekta nyingine. Mnaingiza sukari mbovu, Serikali mmelala, mnashindwa kuziba mipaka ya nchi, bidhaa mbovu zinaingizwa, Watanzania wanakufa, mnajiita Serikali ya hapa kazi tu. Mimi nawaita Serikali ya hapa kuchoka tu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo ningependa kuzungumzia ni suala la uvuvi. Mkoa wa Kigoma tuna Ziwa Tanganyika na takwimu tu toka mwaka 2003 mpaka 2014 zaidi ya nyavu na mashine za bilioni sita zimeibiwa katika Ziwa Tanganyika. Lakini kama Serikali ingekuwa makini kudhibiti wizi huu basi ni imani yangu tungeweza kuvua samaki wa kutosha na tungeweza kutengenezewa viwanda vya kusindika samaki hivyo tungeweza kuuza samaki ndani na nje ya nchi. Sioni mkakati wowote wa viwanda vya kusindika samaki katika Ziwa Tanganyika. Tunaomba Waziri ukija kuhitimisha utuambie ni kwa kiasi gani utawekeza kwenye viwanda hivi ili vijana wa Mkoa wa Kigoma waweze kuajiriwa katika sekta hii ambayo ni muhimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kuna viwanda kama viwanda vya chumvi. Hivi ni viwanda ambavyo havijapewa kipaumbele kabisa. Ukiangalia Bagamoyo kuna chumvi inatengenezwa, ukiangalia Uvinza kule Kigoma kuna chumvi ambayo ilikuwa inatengenezwa, lakini Mtwara na kwenyewe walikuwa wanatengeneza chumvi, Serikali hatujaona hata siku moja mkitoa hata ruzuku ya madini joto kusaidia suala zima la chumvi. Kila mtu anayekuja hapa ni sukari, sukari, sukari, How about chumvi? Kwa nini mmesahau? Ama hamuoni kama Watanzania watakosa madini yenye chumvi yanaweza na yenyewe yakaathiri afya zao. Ningependa mtuambie mkakati gani wa kusaidia watu wanaosindika chumvi ili mambo yaweze kwenda. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la mwisho ningependa kuzungumzia kuhusiana na suala zima la uwekezaji. Ukiangalia katika sekta ya uwekezaji maeneo mengi matumizi ya Taasisi na Mashirika ya Serikali, matumizi yamekuwa ni makubwa kuliko bajeti ya maendeleo. Huu ni udhaifu wa Serikali. Ukiangalia Taasisi nyingi hazina bodi, bodi zimeisha muda wake, TR ameikumbusha Serikali kwamba kunatakiwa kuundwe bodi mpya lakini Serikali bado imelala. Je, mna dhamira ya dhati ya hapa kazi tu ama mnaendelea kufanya mazingaombwe kwa Watanzania?
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunawaomba Mawaziri mnapokaa kwenye mabaraza yenu mumkumbushe Mheshimiwa Rais aunde bodi mbalimbali ziweze kusaidia kilimo katika nchi hii. Ninashukuru.