Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Buyungu
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
2
Ministries
nil
MHE. ALOYCE J. KAMAMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi kuweza kuchangia kwenye Wizara hii ya Uchukuzi. Moja, nikushukuru tena kwa kunipa nafasi, lakini kwa nafasi hii kwanza nikutaarifu kwamba Mkoa wetu wa Kigoma ndiyo pekee katika Mikoa yote 26 ambao haujaunganishwa kwa kiwango cha lami. Nitaarifu kwamba barabara ni uchumi na barabara ni maendeleo. Kutokuwa na barabara maana yake mazao yanayozalishwa katika Mkoa wa Kigoma hayana uwezekano wa kupelekwa kwenye soko. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hatujaunganishwa Tabora kwenda Kigoma, hatujaunganishwa Mpanda kwenda Kigoma, lakini hatujaunganishwa Kagera kwenda Kigoma. Kwa nafasi hii tu nishukuru kwamba kuna makataba umesainiwa wa ujenzi wa barabara ya Kakonko – Kibondo – Kasulu hadi Buhigwe, lakini ujenzi wake unakwenda taratibu sana. Naomba sana Mheshimiwa Waziri hebu fika uangalie ujenzi unavyoendelea sasa. Nimetoka kule kwa shughuli ya kampeni, naona kama vifaa vipo, lakini ujenzi sasa ni mwaka mmoja na nusu, kama unaweza kuhesabu ni kama kilometa 10 tu basi. Sasa naomba atakapokuwa anawasilisha taarifa yake ya mwisho lini barabara hii itakamilika? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ipo barabara katika Jimbo langu inaanzia Kakonko kwenda Kinonko kwenda Bwarama - Kabale hadi Muhange. Inapofika kwenye mpaka wa Muhange, pale kuna soko kubwa limejengwa zaidi ya shilingi milioni 583 ziko pale, lakini soko lile halifanyi kazi kwa sababu hatuna barabara. Naomba sana na bahati nzuri Mheshimiwa Rais Hayati Dkt. Magufuli aliahidi ujenzi wa barabara hiyo ambayo ni kilometa 40, ili kuhakikisha kwamba shughuli zinafanyika, naomba atakapokuwa anawasilisha taarifa yake, lini barabara hiyo sasa itajengwa ili iunganishe nguvu ya huku kwenye Makao Makuu ya Wilaya hadi pale kwenye mpaka wa Muhange?
Mheshimiwa Naibu Spika, wapo wananchi ambao barabara hii inapojengwa katika Vijiji vya Kasanda - Kaziramihunda hadi Kabingo, hawa hawajapewa fidia kwa majengo yao. Naomba nayo atakapokuwa analeta taarifa yake ya mwisho tujue wananchi hawa watalipwa fedha zao lini? Zipo fedha ambazo zimetengwa kwa ajili ya matengenezo ya kawaida kwa kutumia fedha za Mfuko wa Barabara. Ukurasa 321, Mkoa wa Kigoma katika mikoa yote, haijapangiwa kwenye eneo hili.
Mheshimiwa Naibu Spika, hii inakwenda sambamba na ukurasa 335 mpaka 336, fedha za matengenezo ya muda maalum kwa ajili ya barabara, Mkoa wa Kigoma nao kwenye eneo hilo haikupangiwa. Sijajua, kwa nini Mkoa wa Kigoma kama Mikoa mingine ilivyopangiwa haujaweza kupangiwa fedha? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ipo bandari; pale Bandari ya Kigoma ya Kigoma kuna Meli ya Liemba, ina zaidi ya miaka 100. Wakati Mikoa mingine au kwenye bandari nyingine wananunua meli mpya. Kigoma wanasema kwamba wanakarabati ile ya zaidi ya miaka 100, kwa nini tusinunuliwe na sisi meli mpya, kama wanavyofanya kwenye bandari nyingine? Kwa hiyo, naiomba sana Serikali iliangalie hili na sisi katika bandari ya Kigoma tuweze kupata meli mpya kama inavyofanyika kwenye Ziwa Victora kama inavyofanyika kwenye ziwa Nyasa na maeneo mengine. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, upo uwanja wa ndege. Kigoma ipo jirani na Kongo, Kigoma ipo jirani na Rwanda, Kigoma ipo jirani na Burundi, lakini kupitia Ziwa Tanganyika kuna muunganisho kwenda Zambia. Naomba uwanja uweze kujengwa, uimarishwe kwa ajili ya kuhakikisha kwamba wananchi wetu wa Mkoa wa Kigoma wanapata usafiri wa ndege.
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja. (Makofi)