Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mikumi
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. DENNIS L. LONDO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia hoja ya bajeti ya Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi. Bajeti ya Wizara hii ni muhimu sana kwa Taifa hili kwa sababu Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi ndiyo roho ya kile ambacho tunaita mapinduzi ya nne ya viwanda ama uchumi wa kati ama uchumi wa viwanda. Hatuwezi kuzungumzia uchumi wa viwanda bila kuzungumzia miundombinu hasa ya barabara ambazo zinapitika mwaka mzima. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, maeneo mengi ya nchi yetu bado barabara ni changamoto. Ni muhimu wakati tunajadili bajeti ya Wizara hii, kuangalia ni jinsi gani Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi inakuwa na mafungamano ya karibu sana na Wizara zote ambazo tunazitegemea katika ku-transform uchumi wetu hasa Viwanda na Biashara, Wizara ya Kilimo, Afya, Uvuvi na Mifugo; hizi zote zinategemea sana mipango ya Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi ili ipange mipango ya muda mfupi na muda mrefu ya maendeleo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara hii ya Ujenzi na Uchukuzi pamoja na dhana nyingine ya kuwa na mafungamano ya karibu na Idara nyingine ama Wizara nyingine, zina umuhimu sana wa kuangalia ni jinsi gani inaenda kuunganisha wananchi wa Tanzania hasa wanaoishi katika maeneo ya pembezoni.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kuna kasi ambayo inaendelea katika ujenzi wa standard gauge. Pembeni ya standard gauge kuna barabara ambayo inahudumia ujenzi wa reli hizi ambazo imeunganisha vijiji vingi sana katika nchi yetu. Barabara hizi sasa hivi ukipita zimesahaulika, ni barabara ambazo zinaokoa maisha ya watu, lakini zinakuza uchumi sana katika maeneo ya vijijini. Kwa hiyo, ni muhimu Wizara hii ikaziangalia barabara hizi kwa jicho la pekee. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hayo kule Wilaya ya Kilosa kila mwaka tunakuwa na mafuriko. Kuna mabwawa yanaitwa mabwawa ya punguza, mabwawa haya yalitengenezwa enzi ya Mjerumani na miaka yote yalikuwa chini ya Shirika la Reli, tangu yamepelekwa katika Wizara ya Kilimo yamejaa na maji ya Mto Mkondoa yanashindwa kuwa na mahali pa kufikia, matokeo yake yanasababisha maafa kwa wananchi wetu siku zote.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninapozungumzia dhana ya mafungamano kati ya Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi hapa ndipo ninapoanzia. Kuna umuhimu wa Wizara hii kukaa na Wizara ya Kilimo na Wizara ya Maji kuona ni jinsi gani maji ya mito kama haya ambayo yanachukua reli kila siku, reli ya kati kule Godegode inabebwa kila siku kutokana na mafuriko ya mto huu. Ni lini Wizara hii itakaa pamoja na Wizara ya Maji na Wizara ya Kilimo kuona kwamba maji haya badala ya kuwa dhahama na balaa kwa reli yetu ambayo ni miundombinu tunayotegemea inakuwa baraka kwa kutengeneza mabwawa ambayo yanaenda kuhifadhi maji, hivyo kuepusha vifo vya wananchi katika Wilaya ya Kilosa na maeneo ya Jimbo la Mikumi.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba wakati Waziri anahitimisha hoja atuelezee Wizara yake imejipanga vipi kuhakikisha kwamba inazungumza na Wizara nyingine kuhakikisha mabwawa haya ambayo yalikuwa chini ya Shirika la Reli yanarudi huko na yanatunzwa na kuangalia ni jinsi gani maji yake yanaenda kuzuiwa yasilete athari kwa wananchi wetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ni kuhusiana na suala zima la uwezeshaji wa wakandarasi wetu wazawa. Kuna miradi mingi mikubwa ambayo tunaigharamia kama Standard Gauge, lakini kuna bwawa la Mwalimu Nyerere na miradi mingine mikubwa ya barabara. Ni kwa jinsi gani miradi hii tunaitumia kama fursa ya kuwafundisha vijana wetu kuiba teknolojia ama kutumia teknolojia ambayo wenzetu wanaitumia katika ujenzi huu kama sehemu ya masomo ama mafunzo kwa vijana wetu wa ndani. Hii itasaidia miradi hii inapokamilika, basi vijana wetu wanatoka na ujuzi ama wanatuachia ujuzi ambao kesho hautatulazimisha kuagiza ama kuwapa tender makampuni ya nje kwa kisingizio kwamba wakandarasi wetu hawana ujuzi.
Mheshimiwa Naibu Spika, tumeona jitihada za makusudi ambazo Wizara ya Ujenzi inafanya katika kuwawezesha wakandarasi wetu wazawa. Pale Kilosa kuna Barabara ya Kilosa - Mikumi ambayo Kampuni ya Umoja ambayo ni ya wazawa wamepewa kama sehemu ya majaribio ama sehemu ya kujifunza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kule Tabora kuna Barabara ya Kaliua - Urambo ambayo wamepewa wakandarasi wazawa. Pamoja na kuwawezesha wakandarasi hawa wazawa, bado mradi huu ambao tunauona ulikuwa ni sehemu nzuri ya wao kujifunza unakwazwa na nia njema ya baadhi ya watu. Pamoja na kwamba nia ni kujenga barabara hii, lakini vijana hawa unaweza kuona kwamba wanashindwa kutekeleza mradi wao kwa wakati kwa sababu ya GN, fedha haziji kwa wakati, malipo yao hayaji kwa wakati na hivyo kupelekea faida ndogo ambayo ingeweza kutumika kwa wao kuongeza uwezo wa kudai miradi mingine unapotea…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
NAIBU SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa kengele imegonga.
MHE. DENNIS L. LONDO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)