Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Karatu
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. DANIEL A. TLEMAI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa nafasi. Nami niungane na wenzangu ambao kwenye wilaya yao hawajapata chochote kwani nami ni mmojawapo.
Mheshimiwa Naibu Spika, Jimbo la Karatu Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri mjue ni jimbo ambalo limekombolewa kutoka kwenye miaka 25 ya kutawaliwa na Vyama vya Upinzani. Wakati tunatafuta kura tukiwa na wenzangu wa Chama cha Mapinduzi wakiwepo viongozi wakuu akiwepo Mwenyekiti wetu wa Chama cha Mapinduzi Taifa ambapo wakati huo alikuwa mgombea wa Chama cha Mapinduzi kule tuliahidi mengi. Tuliahidi barabara ya kutoka Karatu - Njia Panda - Junction Matala barabara ambayo inaunganisha Mkoa wa Arusha na Mkoa wa Simiyu, hiyo ni kilometa 328 ambazo ziko kwenye Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi lakini hakijatengwa kitu chochote.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kutoka hii barabara ambayo Mheshimiwa Flatei anataka kupiga sarakasi imeanzia Karatu, katika Ilani ya Uchaguzi wa Chama cha Mapinduzi lakini wameenda kuweka kilomita 25 pale Mbulu kwenda Haydom. Barabara hii kwenye Ilani ya Uchaguzi wa Chama cha Mapinduzi imeanzia Karatu – Mbulu – Haydom – Singida. Mimi silalamiki kwamba kwa nini wale wa Mbulu wamepata kilometa 25, niseme tu kwamba sasa Mheshimiwa Waziri sisi Karatu atutengee kiwango kidogo ili na sisi tuwepo katika kula matunda ya nchi hii ambayo tumeyakosa kwa miaka 25 tukiwa chini ya Upinzani. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kweli pale Karatu Rais wa Awamu ya Nne aliahidi kilometa 2 katika Mji wa Karatu lakini mpaka leo hakuna hata kilomita moja. Rais wa Awamu ya Tano aliahidi kilometa 10 kwa mwaka wa 2015 leo ni mwaka 2021 hakuna hata kilometa moja. Mwaka jana tarehe 24 wakati Rais wa Jamhuri wa Tanzania Hayati Dkt. Magufuli akininadi alisema kama anajenga fly overs Dar es Salaam hashindwi kujenga kilometa 10 katika Mji wa Karatu. Sasa nashangaa tena kwenye bajeti hii hamna hata kilometa moja sasa wananchi wale 2025 nitawaaambia nini? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, asubuhi Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI aliongea kwamba mwaka 2025 kwenye Jimbo lake la Tanga hawezi kurudi kama hajafanikisha maendeleo ambayo ameahidi kwa wananchi wa Tanga Mjini. Nami kwa wale wa Karatu tulivyoahidi Chama cha Mapinduzi na tukiwa na viongozi wa Chama cha Mapinduzi kwamba tunaweza kuleta maendeleo kwa speed mkikichagua Chama cha Mapinduzi.
Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi wa Jimbo la Karatu walijitahidi kuchagua Mbunge wa Chama cha Mapinduzi, nami kilio hiki nimefikisha kwenu ninyi Serikali ya Chama cha Mapinduzi. Ni ombi langu kwamba maombi haya yatazingatiwa na kilometa hizi kumi ndani ya Jimbo la Karatu tuweze kupata na kilometa hizi kutoka Karatu – Mbulu
– Singida tunaweza kupata, vilevile barabara hii ya kutoka Oldeani – Mangola – Matala – Lalago kule Simiyu; na barabara hii ni muhimu sana kwa sababu inaunganisha Mkoa wa Arusha na Mkoa wa Simiyu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naiomba Serikali yangu ya Chama cha Mapinduzi, tuliinadi Ilani ya Chama cha Mapinduzi na wananchi walio wengi waliamini ahadi kubwa sana ya Chama cha Mapinduzi na Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi. Ni imani yangu kwamba Ilani ile ya Chama cha Mapinduzi ili wananchi waendelee kuiamini, kwamba sasa inaweza kwenda kutekelezwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. (Makofi)