Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Hon. Iddi Kassim Iddi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Msalala

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

MHE. IDDI K. IDDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru kwa kunipa fursa hii ya kuchangia kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Msalala, ninaomba nichangie kwenye hotuba hii ya bajeti ya Wizara ya Mawasiliabo. Kwanza kabisa, naomba nijielekeze kwenye suala zima la usalama wa fedha za mtu anaye-transfer fedha kutoka kwenye mtandao mmoja kwenda kwenye mtandao wa pili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwa na changamoto kubwa kwa watumiaji wa mitandao wanaofanya transfer kutoka mtandao mmoja kwenda mtandao wa pili juu ya usalama wao wa fedha mahali ambapo wanakosema kutuma fedha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitatoa mfano na mwenyewe ni muathirika, mimi ni mtumiaji wa mtandao wa Airtel na inapotokea bahati mbaya ninatuma fedha kwenda kwenye mtandao mathalani wa Vodacom, inapotokea nimekosea usalama wa fedha unakuwa ni mdogo. Kwa hiyo, naomba nishauri Wizara iweze kuona namna gani basi sasa ianze kushauri kampuni hizi zijikite katika kuhakikisha kwamba wanaweka coordination ili ku-secure zile fedha za mtumiaji anayetuma mtandao mmoja kwenda mtandao wa pili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nijielekeze moja kwa moja kwenye Jimbo langu sasa la Msalala. Jimbo langu la Msalala lina kata 18 na lina vijiji 92 lakini katika Kata zaidi ya 12 hatuna mawasiliano. Kumekuwa na changamoto nyingi sana juu ya ukosefu wa mawasiliano katika Jimbo langu la Msalala na hasa katika Kata ya Jana, Mwaruguru, Mwanase, Kashishi, Lunguya, Ntobo, Shilela, Mega na kata nyingine nyingi. Matatizo haya yanasababisha sasa ndoa kuvunjika. Leo hii katika maeneo mbalimbali katika Jimbo langu la Msalala ukitaka kupiga simu mpaka utafuta mti au mbuyu mrefu ili uende ukapige simu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, matatizo haya nimeshawasilisha kwa Waziri na nimemuomba Waziri kwamba aone namna gani anaweza kutusaidia sisi wa Jimbo la Msalala ili tuondokane na adha hii. Ndoa nyingi zinavunjika kwa sababu ya kisingizio cha mtu kwenda kwenye mlima fulani kupiga simu, unakuta ameshaandaa mchepuko hukohuko. (Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukosekanaji wa mawasiliano haya unahatarisha sasa ndoa za wananchi wangu wa Jimbo la Msalala. Nikuombe Mheshimiwa Waziri, chondechonde, makao makuu ya wilaya hatuna mtandao. Wanapotaka kuchapisha document za halmashauri ni mpaka wasafiri waende Kahama Mjini, Mheshimiwa Waziri hebu tuangalie. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini sio hilo tu, tuna maeneo mengi ya machimbo katika Jimbo langu la Msalala. Kama mnavyofahamu suala zima la biashara ya madini na biashara nyingine linaenda kimtandao, lakini suala la applications mbalimbali linaenda kimtandao, ukosekanaji wa mawasiliano katika Jimbo langu la Msalala, hasa katika Kata ya Segese, Kata ya Bulyanhulu, Kijiji cha Nyangalata, Kata ya Jana na maeneo mengine, unasababisha kuwanyima haki wananchi juu ya kufanya application ya kuomba leseni za madini na kibali cha mazao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama mnavyofahamu wananchi wetu ili kupata kibali cha kusafirisha mazao unatakiwa u-apply kwa mtandao na maeneo yale hayana mtandao. Mheshimiwa Waziri ukosefu wa mawasiliano katika Jimbo la Msalala unasababisha anguko kubwa la kiuchumi. Tunakuomba chondechonde katika kata hizi ambazo nimezitaja angalia namna gani basi unaweza kutupatia mawasiliano, ili wananchi wetu waweze kuondokana na adha hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, yangu yalikuwa ni hayo. Naunga mkono hoja, naomba Mheshimiwa Waziri chondechonde akina mama na akina baba wanalalamika ndoa zao ziko hatihati, tuangalie kwa jicho la huruma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, naunga mkono hoja. (Makofi)