Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Hon. Yahya Ally Mhata

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nanyumbu

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

MHE. YAHYA A. MHATA: Mheshimiwa Mwenyekiti, niko

MWENYEKITI: Uko tayari, haya karibu.

MHE. YAHYA A. MHATA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami naomba nichukue nafasi hii kumpongeza sana Waziri na Naibu wake pamoja na watendaji wote walio chini ya Wizara yake kwa kazi nzuri wanayoifanya.

Mheshimwa Mwenyekiti, tarehe 05 Mei, 2021, niliuliza swali la mawasiliano ndani ya Jimbo langu la Nanyumbu, Mheshimiwa Waziri alitoa majibu yenye uhakika kwamba tenda inatangazwa na maeneo yote yenye changamoto yatachukuliwa hatua zinazostahili. Ni matarajio yangu kabla hatujaondoka ndani ya Bunge hili nitapata taarifa sahihi tenda imetangazwa lini na nani anakuja katika jimbo langu kufanya kazi hii ya mawasiliano. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili ni changamoto ambayo tumeanza kuishuhudia ndani ya nchi yetu. Wiki mbili zilizopita TRA ilikumbana na changamoto ya mtandao wake wa malipo kutokufanya kazi, karibu siku tatu uchumi wa nchi hii uliyumba, watu hawakulipa na hakuna malipo ya aina yoyote yalifanyika TRA. Siku tatu zilizopita tumeshuhudia Kampuni yetu ya TANESCO imeshindwa kutoa huduma ya kununua LUKU. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo hili ni tahadhari, nawaomba sana Wizara, nawaomba sana wataalamu wetu wa TSA wawe waangalifu, dhahama inakuja. Kama hatutakuwa na backup system ya kukabiliana na utaratibu huu iko siku hapa tutakwama kabisa kufanya shughuli zetu. Mheshimiwa Waziri atakapokuja ku-wind-up atueleze ni mikakati gani inayofanywa na Wizara yake kukabiliana na hizi changamoto ambazo zimeanza kujitokeza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni minara. Kuna wajanja ambao wapo ndani ya nchi hii wanapata taarifa kwamba kuna Kijiji A kutawekwa mnara, Kijiji B na Kijiji C. Wanakuja kule wananunua maeneo ya wananchi wetu kwa kujua kwamba kesho unakuja kuwekwa mnara, hawa ni matapeli. Namuomba Mheshimiwa Waziri niko tayari kumsaidia wale wote waliokuja ndani ya jimbo langu wakanunua maeneo ya wakulima kumbe lengo lao ni
kuwekwa minara, minara ile walipwe wahusika. Huu ni wizi mkubwa, haiwezekani mtu atoke huko atokako aje kununua eneo ndani ya kijiji chetu kumbe kesho unawekwa mnara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, matokeo yake Serikali ya Vijiji imekosa mapato, wananchi wamekosa mapato na yule mtu kanunua lile eneo na haonekani yuko wapi. Jambo hili kwa kweli linaumiza sana.

T A A R I F A

MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti,

MWENYEKITI: Taarifa.

MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nataka nimpe Taarifa mzungumzaji, katika Wilaya yangu ya Liwale kuna Kijiji cha Kibutuka kuna tapeli mmoja ameenda kuchukua eneo la shule, mnara uko kwenye eneo la shule lakini unasoma mtu yuko Arusha.

MWENYEKITI: Taarifa hiyo Mheshimiwa.

MHE. YAHYA A. MHATA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa hiyo naipokea. Ndani ya Wilaya yangu kwenye Kata ya Sengenya, kwenye Kijiji cha Mkumbaru, kuna hao matapeli wamekuja na wamechukua hayo maeneo na wameweka minara. Kwenye Kata ya Mkonona, kwenye Vijiji vya Mangara Mbuyuni kuna watu wa aina hiyo. Kwa hiyo, naomba sana Wizara ihakikishe kwamba jambo hili kwa kweli linakoma na hawa watu warudishe minara hiyo kwa wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni kuhusu Shirika letu la TTCL. Ni jambo la kushangaza sana inakuwaje Serikali inadaiwa na Shirika hili? Ndani ya bajeti tunapitisha hapa bajeti za Wizara, inakuwaje leo wanashindwa kuwalipa? Hhili jambo halikubaliki. TTCL pia mimi naomba niwalaumu inakuwaje unambembeleza mteja? Kama hakulipi si umkatie? Mbona private sector wanafanya hivyo sisi tunashindwaje? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunakuja kulialia hapa kumbe power tunazo, tukate. Vinginevyo kama utaratibu huu wa kubembelezana utaendelea mashirika yetu ya umma yatakufa. Tunapitisha bajeti tutalipa umeme, maji, simu, kwa nini wewe Mtendaji Mkuu wa Shirika hukulipa simu TTCL? Unapata huduma bure na unaendelea kuchekewa, hili jambo halikubaliki. Mimi naishauri Serikali, TTCL nendeni mkawakatie wale wote mnaowadai vinginevyo tutakuwa tunakwama. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho, Shirika letu la Taifa (TBC) matangazo yake hayasikiki maeneo mengi ya nchi yetu. Jimbo letu la Nanyumbu TBC haisikiki kabisa. Mfuko huu wa Mawasiliano kwa nini hawawawezeshi TBC wakasikika nchini kwetu? Hili ni eneo ambalo wananchi wetu wanategemea kupata mawasiliano ya uhakika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi tuko mpakani na Msumbiji, tunatarajia mawasiliano ya uhakika yapatikane kutoka…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante, muda wako umekwisha.

MHE. YAHYA A. MHATA: Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja lakini namuomba Mheshimiwa Waziri jioni hapa hapataeleweka kama hakutakuwa na majibu sahihi. Ahsante sana. (Makofi)