Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. NEEMA K. LUGANGIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa fursa hii. Kwanza kabisa natoa shukrani za dhati kwa Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutoa mwongozo na nia yake ya kuhakikisha miundombinu ya teknolojia ya mawasiliano inafika asilimia 80 ifikapo mwaka 2025. Haya ni maono makubwa ambayo yatatupelekea kuimarisha uchumi wetu zaidi. Eneo la teknolojia ya mawasiliano ni sekta mpya ambayo ikiangaliwa kwa umakini, nchi hii inaweza kujipatia kipato kikubwa pamoja na kutengeneza ajira.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe mfano mdogo kwa ndugu zetu Wakenya, sekta ya teknolojia ya mawasiliano inachangia asilimia nane ya pato ghafi la Taifa; na tayari sekta hii kwa Kenya imeshatengeneza kakribani ajira 250,000; na hii ni kwa takwimu ya Serikali ya Kenya. Ukuaji wa sekta ICT Kenya umepita ukuaji wa sekta zote kwa zaidi ya asilimia 23 na hii ni kwa mlongo uliopita peke yake. Kwetu hapa Tanzania bado kuna changamoto ambazo tukiziangalia vizuri zitasaidia kuongeza ajira katika sekta hii ambayo hivi sasa tumeifunga. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe tu mfano mdogo, wachangiaji wengi asubuhi waliongelea kuhusu YouTube. Hivi sasa kwa Tanzania YouTube mazingira yake siyo Rafiki. Nasema hivi kwa sababu wako wanamuziki wachache ama wadau ambao wanatumia YouTube kama akina Dimond, Alikiba na Milard Ayo ambao wamenufaika; lakini baada ya kuleta sheria ambazo zimepelekea changamoto, wako pia watu wengi ambao wamejiondoa kutumia mtandao huu ambao wengi wao ni vijana. Sasa hii inaleta changamoto kubwa kwa sababu vijana hawa wanatumia teknolojia hii na sekta hii kujipatia ajira ambazo ni changamoto. Kwa hiyo, sera zetu lazima ziweke mazingira ya kuwawezesha wao kujiajiri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na changamoto hii, tofauti na nchi nyingine, hapa Tanzania vijana wengi ambao wapo kwenye sekta hii hawana elimu rasmi ya masuala ya kidijitali. Kwa hiyo, tunapowaongezea gharama za kulipa ni kufifisha jitihada zao binafsi ambazo wao wenyewe wamezichukua kama viijana kujitengenezea ajira. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo naomba niishauri Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia masuala yafuatayo: jambo la kwanza, Wizara ione namna gani itaweza kupunguza gharama zinazolipwa na Watanzania hususan hawa vijana kwa sababu hivi sasa ni changamoto kubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la pili, naiomba Wizara ifanye mapitio ya sheria ili kuona namna ya kuondoa baadhi ya makosa kutoka kuwa makosa ya jinai iwe makosa ya madai, kwa sababu na yenyewe inaleta changamoto kubwa sana kuhakikisha kwamba watu wananufaika na sekta hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la tatu, tuongeze ufikiaji wa internet kama ambavyo wengine wamechangia, hususan kule vijijini, hata tukiweza kufikia 3G. Tumeona kwenye miji mikubwa hii access ya internet inasaidia sana kufanya biashara, hususan kwa viijana na wanawake. Ukiingia mtandao wa Instagram, wengi wananufaika sana, lakini fursa hizi hazitunufaishi wale ambao tunatoka hususan Mikoa ya pembezoni. Kwa hiyo, nadhani lazima jitihada zifanyike katika eneo hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile bado gharama za kupata internet hapa nchini Tanzania ni kubwa ukilinganisha na majirani zetu. Nitatoa mfano mdogo. Nairobi gharama ya uzito kwa mwezi ni Dola za Kimarekani 5.5, tukienda Uganda ni Dola za Kimarekani 10; Uganda kwa maana ya Mji wa Kampala, lakini tukija Tanzania kwa maana ya Mji wa Dar es Salaam ni dola za Kimarekani 15.5. Kwa hiyo, unaweza kuona ulinganishi. Kwa Nairobi ni 5.5 kwa Dar es Salaam 15.5. Kwa hiyo, nadhani ni muhimu tufanye tena uangalizi wa gharama hizi, kwa sababu kwa ilivyo sasa hivi Watanzania wengi hawafaidiki na hawanufaiki na sekta hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tukiweza kufanya hivyo, tutaipunguzia Serikali mzigo wa ajira kwa vijana, kwa sababu tutaweza kufungua vijana kujiajiri kupitia Sekta hii. Katika hili naomba niishukuru Kamati kwa sababu na wenyewe pia wamelisemea suala hili kwenye wasilisho lao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu wa tano, naomba Serikali iangalie namna ya kushirikiana na wabunifu ili kuongeza faida ambayo inapatikana na sekta hii. Yaani Wizara msijifungie, kwa sababu wako vijana ambao ni wabunifu tuone ni namna gani tunaweza tukashirikiana nao. Katika eneo hili nichukue fursa hii nimpongeze sana Spika, Mheshimiwa Job Ndugai kwa sababu kwa jitihada zake awali alifungua milango akakutana na vijana ambao ni wabunifu hadi wakatengeneza App iliyokuwa inawezesha vijana pamoja na wananchi kuwa karibu na Wabunge wao. Kwa hiyo, huo ni mfano tosha kwamba hata Wizara ikishirikiana na hao wabunifu inaweza ikaleta tija. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kumalizia, nirudie tena kwamba tunaweza tukajifunza kwa wenzetu wa Kenya ambao wana Sera ya Digital Economy Blueprint ambayo hivi sasa sisi Tanzania hatuna. Yote ambayo yamechangiwa hapa, kama tutakuwa hatuna sera madhubuti ya Digital Economy Blueprint, mengi haya yatashindikana kwa sababu hii ni sekta ambayo inahitaji iwe na miongozo thabiti na iwe na njia zote ambazo zitahakikisha zinawalinda watumiaji na walaji wa hii sekta. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja kuwasilisha, angalau pia atueleze: Je, ana mpango gani wa kuja na Sera ya Digital Economy Blueprint. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nashukuru kwa fursa hii, naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)