Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Hon. Nashon William Bidyanguze

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kigoma Kusini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

MHE. NASHON W. BIDYANGUZE: Mheshimiwa Mwenyekiti, uliniita mchangiaji wa tatu, nipo hapa William Nashon.

MWENYEKITI: Ulipoitwa hukuwepo.

MHE. NASHON W. BIDYANGUZE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwepo.

MWENYEKITI: Haukusimama lakini.

MHE. NASHON W. BIDYANGUZE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nilisimama, nilikuwepo.

MWENYEKITI: Haya endelea.

MHE. NASHON W. BIDYANGUZE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nami nikushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia Wizara hii muhimu sana ambayo ni Wizara ya Mawasiliano. Kwanza naomba nimpongeze ndugu yangu Waziri pamoja na Naibu Waziri kwa kazi nzuri wanayoifanya. Wizara hii ni Wizara nyeti sana, kwa sababu sasa hivi kwa kweli wananchi wameshaelimishwa na wanazo simu zao na njia nyingi ni kutumia simu. Ukitaka kulipia maji, ni lazima utumie simu, lakini pia ukitaka kulipia umeme lazima utumie simu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi kuna shida kwenye mtandao huu wa kulipia umeme. Nadhani mnaweza mkaona kabisa, yaani hakuna namna ya kulipia umeme, kuna shida sana. Kwa hiyo, bado Wizara ina kazi kweli ya kufanya hii shughuli ili iweze kuwa na ufanisi mkubwa kuliko ilivyo sasa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi natokea Wilaya ya Uvinza ambayo kwa kweli ni Wilaya ambayo watu waliitikia sana katika utaratibu huu wa wananchi kuwa na simu, kwa sababu hakuna namna nyingine, maisha ni simu. Kwa hiyo, Wizara hii ni Wizara ambayo inawagusa watu. Kwangu ninazo kata 16, lakini zipo kata nne, zote zina matatizo ya mawasiliano. Yaani ukienda kule Mbunge unafanya ziara, hata kama ningekwenda na Waziri, yaani siku hiyo tunashinda hakuna mawasiliano kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, moja, ni Kata ya Mtegowanoti, yaani haina mawasiliano kabisa na hakuna mnara hata mmoja; ya pili ni Kata ya Kandaga hasa katika Kijiji cha Kandaga chenyewe. Kwa kweli na Kijiji kile ndipo ninapotokea; mimi nikishaingia kijijini pale, hakuna mawasiliano mpaka kesho nitoke kule, niende eneo lingine ambalo lina mawasiliano. Ni aibu sana. Kwa hiyo, nilikuwa naomba kwakweli jambo hili Mheshimiwa Waziri aweze kuliangalia hasa katika eneo langu hilo la Kandaga na vijiji hivi ambavyo nimevitaja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kata ya Herembe ina vijiji vitatu, lakini vyote havina mawasiliano; Kata ya Igalula ina vijiji saba lakini vijiji ambavyo vina mawasiliano ni viwili; ambavyo ni Lukoma pamoja na Igalula yenyewe, vilivyobaki vyote, havina mawasiliano. Sasa kwa kweli ukiangalia hili ni tatizo. Ukienda kule wananchi wanamlalamikia Mbunge kwamba ni vipi sisi tumetengwa? Mbona wengine wana mawasiliano, sisi inakuwaje? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nilikuwa nadhani, kwa kuwa na sisi Serikali inao mtandao wa TTCL, kwa nini basi tusiweze kupata minara ya TTCL ili tuweze kuondokana na hilo tatizo? Kwa sababu makampuni mengine haya yanafanya kazi kibiashara zaidi, lakini mtandao wetu huu wa kampuni ya TTCL, pamoja na kwamba na yenyewe inafanya kazi kibiashara, lakini pia mtandao ni wa Serikali. Kwa maana hiyo, ina huduma pia. Wenzetu hawa hawana huduma; wakiweka eneo mtandao au huo mnara, wakiona hali siyo nzuri ya mapato, wanahamisha. Sasa wakihamisha wale wachache maana yake wanaobaki, hawana huduma. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Waziri, katika Jimbo langu eneo la mawasiliano, tukimaliza bajeti yake yeye mwenyewe Waziri twende Pamoja. Haiwezekani tuwe marafiki, halafu mimi nyumba inaungua. Mheshimiwa Waziri nitafurahi sana tukienda wote huko ili uone. Simu zako utazima, kwa sababu hutakuwa na uwezo wa kuzitumia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niunge mkono hoja. Kama Mheshimiwa atanifanyia hivyo, basi hata shilingi yake sitashika. (Makofi)