Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Muheza
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. HAMIS M. MWINJUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kunipa nafasi hii niweze kuchangia kwenye hotuba hii ya Wizara na Mawasiliano na Teknolojia ya Habari. Kwanza nichukuwe nafasi hii kuwapongeza Mheshimiwa Waziri Dkt. Faustine Ndugulile, na wasaidizi wake Engineer Kundo Mathew, dada yangu Dkt. Zainab Chaula na Mwalimu wangu Jim Yonazi kwa hotuba nzuri yenye matumaini inayoonyesha kwamba nchi yetu inajielekeza kwenda sawa sawa na dunia nzima kwenye upande wa teknolojia. Tuna walakini hapa na pale lakini lengo lenu linaonekana wazi kabisa ni kwamba mmekusudia tusiachwe na kasi ya dunia hongereni sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nina mambo mawili ya kuchangia japokuwa nina mengi kwa sababu nimekuwa hapa toka asubuhi leo na michango mingi ya Waheshimiwa Wabunge imekuwa ya kitaalamu na iliyojitosheleza sana, sitaki kuijazia nzi, kuipigia miluzi mingi na kumpotosha Waziri, nafikiri ameandika mengi na anajua mahali pa kushughulikia ili kupata mwelekeo ambao tunaokusudia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo ambalo limesemwa na Waheshimiwa Wabunge wengi na mimi napenda nilitilie msisitizo ni kuhusiana na udhaifu au kukosekana kabisa kwa mawasiliano sehemu kubwa ya vijijini katika nchi yetu. Mimi natoka Jimbo la Muheza ambapo kimsingi zaidi ya nusu ya Jimbo la Muheza aidha lina mawasiliano dhaifu sana ya simu ama hakuna kabisa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mahali ukiambiwa mtu yupo halafu ukampata kwenye simu unaanza kumuuliza kwanza unatumia simu ya aina gani mpaka inapatikana hapo ambayo inaweza kushika mtandao kibabe namna hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna tarafa, kata vijiji na vitongoji vingi ambavyo havina kabisa mawasiliano. Kwa mfano tuna Kata ya Kwezitu iliyopo katika Tarafa ya Amani sehemu yake kubwa haina mawasiliano, Lanzoni kule Kwemingoji hakuna mawasiliano, Kiwanda na Mangugu kwenye Kata ya Tongwe hakuna mawasiliano, Magoroto na Ufinga, Mtindiro, Kwemhanya, Kwebada, Songa, Kwafungo; zote aidha hazina mawasiliano kabisa ama mawasilisano ni dhaifu sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi binafsi nikienda kijijini kwangu yaani simu inakuwa ni ya kuchezea game ama kama unataka kufanya shughuli yenye manufaa kwenye simu hiyo uwe umesha-download kitabu uende ukaitumie kusomea lakini suala la kuitumia kwa ajili ya mawasiliano halipo kabisa. Nimuombe Mheshimiwa Waziri, sitaki kulalamika tu na kuliacha hili suala linaelea, kwa sababu najua kimsingi operators wetu wanafanya biashara na pengine wanasema kwa sababu ya gharama ya kusimika aidha minara hii na gharama ya kuiendesha inawafanya wasifike baadhi ya sehemu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, najua Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na Naibu Katibu Mkuu ninyi ni watu wa kisasa sana, mimi katika pitapita zangu nimeshakutana baadhi ya watu ambao wanatoa teknolojia mbadala ya kufanya shughuli hizi ili tupate matokeo hayahaya tunayoyalilia na wananchi wote waweze kupata mawasiliano kwa kadri inavyotakikana. Mheshimiwa Waziri nikuombe suala la mawasiliano kwenye nchi hii tusilifanye baadhi ya sehemu likawa ni jambo la anasa. Kwa hisani yako nakuomba wewe na Wizara yako sasa muangalie namna ambavyo mnaweza kupata teknolojia mbadala na kuhakikisha hili suala linatatulika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mtu alikuwa ananiambia kuhusiana na teknolojia ya new line wireless na kwa jinsi gharama alivyokuwa anazilinganisha japokuwa mimi sio injinia nilikuwa najiuliza kwa nini tumechelewa, kwamba gharama ya kusimika minara hii ni ndogo sana, teknolojia hii haitumii umeme ama mafuta kama inavyotumia hii minara mikubwa ya makampuni kwa maana ya ma-operator wetu wa sasa na uwezekano wa kufanya project ndogondogo kwa ajili ya kutatua kero za sehemu husika ni mkubwa vilevile. Kwa hiyo, nawaomba muangalie namna ambavyo tunaweza kupata teknolojia hii na nyingine nyingi za aina hii, najua ziko nyingi na ninyi ni watu wajanja, watu wa kisasa mnaweza kuzipata kwa sababu mme-specialize kwenye Wizara mnayoishikilia, mnaweza kutupatia ufumbuzi. Narudia tena Mheshimiwa Waziri tusiache mawasiliano ya kueleweka yakaonekana ni kitu cha anasa kwenye nchi hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ni suala la YouTube. Nimekuwa kwenye Bunge lako Tukufu hili toka asubuhi na nimesikiliza michango mingi, nimefurahishwa na concerns za Wabunge wengi kuhusiana na mapato yanayopotea ya Serikali na wasanii husika kwenye makusanyo ambayo yanaweza kupatikana kwenye mtandao wa YouTube. Kwanza, niseme kwamba ni kweli YouTube ina hela lakini kuna misconception kubwa, sio hela hizo ambazo Waheshimiwa Wabunge wengi wanaziona.
Mheshimiwa Mwenyekiti, YouTube ni miongoni mwa platforms ambazo zinafanya shughuli ya kuuza muziki (streaming) lakini sio peke yake, kuna platforms nyingi ambazo zinafanya shughuli hii na kimsingi platforms ambazo zinapatikana kwenye nchi hii YouTube ni ya mwisho kwenye kuingiza mapato yaani inalipa kidogo kuliko platforms zote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitatoa mfano, YouTube kwa views milioni moja kwa nchi yetu inalipa kati ya dola 400 na 500. Kimsingi YouTube inalipa kutokana na nchi ambayo aliyei-upload yuko. Kama kuna nchi nyingine ambazo matangazo mengi yanaweza kuwekwa wanalipwa Zaidi, kuna mahali wanalipwa mpaka dola 1,000 kwa views milioni moja lakini kwetu ni kati ya dola 400 na 500 kwa views milioni moja. Wakati Spotify wanalipa kwa namba hiyohiyo ya views kati ya dola 7,000 mpaka 10,000 kwa streams hizohizo. Tofauti ya YouTube na hizi platforms zingine ni kwamba YouTube yenyewe ni visual hizi nyingine unaweza kusikiliza peke yake. Kina Spotify, Apple Music, Napster, Deezer, Tudor, zote hizi zinafanya shughuli hiyohiyo na zinalipa zaidi ya inavyolipa YouTube. Kwa hiyo, niwaombe Waheshimiwa tusitoe tu macho kwamba YouTube ndio platform peke yake inayolipa, kuna sehemu nyingi sana ambazo wasanii wanaweza kupata kipato kikubwa na zinatakiwa kutolewa macho. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kimsingi YouTube inabidi kuwa na aggregator lakini nchini kwetu hatuna aggregator hata mmoja. Nilimsikia Mheshimiwa mmoja asubuhi ameliweka kama wasanii na content creators ni kosa lao au ni ufahamu wao kuwa mdogo. Sisi wengine tumejaribu kuhakikisha nchi hii inakuwa na aggregator kwa miaka karibuni minne au mitano iliyopita, siyo suala rahisi, haliwezekani kirahisirahisi. Pengine nimuombe Mheshimiwa Waziri kama tunataka kuwa na aggregator basi Serikali iingilie kati ijaribu ku-harmonize haya majadiliano kati yetu na YouTube tuone kama tunaweza kupata aggregator kwenye nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Afrika Mashariki na Kati yote aggregator ni mmoja tu Mkenya Ngomma VAS lakini wasanii wote wengine wanatumia Believe ambayo ni ya Ufaransa agent wao ni Zeze ambao wako Kenya, Spice Digital ambayo ni ya South Africa ambaye agent wao kwa hapa ni Muziki, Metal Music ya Nigeria ambayo haina agent hapa na Ngomma ambayo ni ya rafiki yangu CLEMO ndiyo ya Kenya. Kimsingi sisi hatuna aggregator na watu wengi naowafahamu nikiwemo mimi mwenyewe tumejaribu kupata aggregator kwenye nchi hii imeshindikana. Ndugu zangu Wasafi watakuwa mashahidi, Diamond Platinum najua alienda mbele sana lakini kuna mahali alikwama mpaka leo hana hiyo huduma. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe Serikali yetu iangalie namna ambavyo inaweza kulinda content creators wake lakini pia na walaji, yaani watazamaji na wasikilizaji wa kazi hizi zinazowekwa kwenye mitandao. Kwa mfano, YouTube ukiwa na views zinaonyesha kabisa nyimbo imesikilizwa mara ngapi nchi gani. Kwa hiyo, Marekani wao wanachukua kodi asilimia 30 ya content zote zinazoangaliwa ikiwa zimeangaliwa nchini Marekani. Wao wanachukulia kwamba kama mlaji ni Mmarekani basi ametumia facilities zetu kuitumia hii YouTube kwa hiyo asilimia 30 yetu tunaitaka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri Serikali na sisi tuna wasanii wetu wengi na wasanii wa nje ambao wanaangaliwa hapa. Kwa mfano DJ Khaled akiangaliwa Tanzania si inakuwa imeonekana kwamba ameangaliwa mara ngapi na sisi tupate percent yetu kama sio 20, 30 lakini tuichukue. Kwa nini Wamarekani wachukue asilimia 30 na sisi tusipate hata percent moja wakati walaji ni wetu, fedha na facilities walizotumia ni za kwetu na sisi tunastahili kupata fedha hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuna platforms zingine nyingi ambazo ni plugs ambazo wasanii wetu wanaweza kuweka mziki wao na wasikatwe hata senti moja yaani wasipite kwa hawa aggregators. Ndio maana kwa sasa tumepunguza sana kufuatilia kuwa na aggregatoror kwa sababu tunaona kwamba kuna namna mbadala tunaweza tukaendesha shughuli zetu bila kuwa nao. Kwa mfano, Caller Tune wanakutoza kwa wimbo unao-upload ama album na ni dola kumi ama dola 100 kwa album na unapata ingizo lako lote ya nyimbo zako namna ambavyo…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Nakuongeza sekunde ishirini.
MHE. HAMIS M. MWINJUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Nihitimishe kwa kusema kwamba naiomba Serikali hasa Wizara ya Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari iweke dawati maalumu la kwa ajili ya kuwasaidia watu wetu hasa wasanii na content creator kuhusiana na ufahamu wa masuala haya. Nasema hivyo kwa sababu tunapoteza pesa nyingi na tuna vijana wengi wa Kitanzania ambao ufahamu wao kwenye masuala haya ni mkubwa wanaweza kutusaidia kutuongezea pato la Taifa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. (Makofi)