Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto

Hon. Regina Ndege Qwaray

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto

MHE. REGINA N. QWARAY: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru kwa nafasi uliyonipatia nami niweze kuchangia bajeti ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto. Kwanza nianze kupongeza Wizara hii ikiongozwa na Mheshimiwa Waziri pamoja na Naibu Mawaziri na watumishi wote wa Wizara kwa kazi kubwa wanayoifanya kuhakikisha huduma hii ya afya inaendelea kuboreshwa. Pia, niipongeze Serikali yetu kwa kazi kubwa inayofanya kuhakikisha huduma ya afya inaendelea kuboreka ili wananchi wetu waweze kupata huduma. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nichangie kuhusu huduma ya mama na mtoto. Niombe Wizara itueleze wazi dhana halisi ya huduma bure kwa akinamama wajawazito na watoto wa chini ya umri wa miaka mitano. Huduma hii imebaki kuwa nadharia, akinamama wengi wanapokwenda kujifungua wanatakiwa waje na vifaa vyao ili waweze kupata huduma hiyo ya kujifungua, wakati tunasema kwamba huduma hii ni bure kwa akinamama wajawazito, wanapokwenda kujifungua wapewe huduma stahiki.

Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile, ukienda kwa upande wa watoto chini ya miaka mitano, huduma hii si bure kwa sababu hawapati dawa. Watoto hawa wanapata huduma ya kuwaona Madaktari lakini linapofika suala la dawa wanatakiwa wajigharamie na kwenda kununua.

Mheshimiwa Naibu Spika, basi niiombe Wizara ituweke wazi ni namna gani sasa huduma hii ya akinamama wajawazito inapatikana bure, lakini huduma kwa watoto chini ya miaka mitano inapatikana bure. Katika eneo letu mfano, hususan Mkoa wetu wa Manyara, jiografia yetu ni ngumu na ya mazingira magumu mno. Sasa inapofika hatua mama anaambiwa aje na vifaa vyake anapoenda kujifungua, inabaki akinamama wengine wala hawaendi hospitali, wanajifungulia nyumbani, kitu ambacho kinahatarisha maisha yao. Hatimaye akinamama wengi wanapoteza maisha kwa sababu fedha za kumudu gharama.

Mheshimiwa Naibu Spika, huyu mama mjamzito, kwanza kutoka kwenye eneo lake analoishi kwenda kwenye hospitali ni zaidi ya kilometa 70, 80 hadi 100. Sasa mama wa kijijini unapomwambia sasa aje na vifaa, kwanza akiangalia gharama zile za usafiri, aje agharamie vifaa vya kwenda kujifungulia, kiujumla wanashindwa kumudu hizo gharama. Kwa hiyo, naomba iwekwe katika utekelezaji, tusibaki katika nadharia, iwekwe kwa vitendo kwamba akinamama wapatiwe huduma na watoto wale chini ya miaka mitano wapatiwe huduma. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hospitali zetu za Wilaya na vituo vyetu vya afya hakuna vyumba vya kuhudumia watoto njiti. Watoto njiti wanapopatikana wanahudumiwa locally, lakini naomba sasa Serikali ihakikishe vituo vyetu vya afya, hospitali zetu za Wilaya, vyumba vile vya kuhudumia watoto njiti pamoja na wataalam wale wa kuwahudumia wale watoto. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo kuna huduma ya phototherapy unit, wale watoto ambao wanapata homa ya manjano. Maeneo yetu mengi hasa Mkoa ninaotoka mimi, watoto hawa wanapopata tatizo hilo la homa ya manjano kiukweli hawapati hiyo huduma inayostahili kwa sababu hatuna mazingira wezeshi, hatuna vifaa, hizo phototherapy unit hazipatikani. Kwa hiyo, Serikali ione namna gani basi angalau hata hospitali zetu za wilaya na rufaa ambazo ni hospitali za mikoa ziwepo hizo phototherapy unit ili watoto wetu wanapopata tatizo hilo basi wahudumiwe kitaalam zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nijikite zaidi kwenye huduma ya wazee. Kiukweli huduma hii ya wazee bado niishauri Serikali ione namna bora ya kuwahudumia hawa wazee wetu wa miaka 60 kwenda juu. Wazee hawa wanateseka mno wanapofika kupata huduma hizo katika hospitali zetu. Ukizingatia hospitali zenyewe hizi bado tuna upungufu mkubwa wa dawa, lakini yule mzee anapohitaji ile huduma akijua kwamba Serikali yetu inamhudumia bure, anapofika ile huduma haipati, kiujumla wananyanyasika na kufedheka hawa wazee. Naomba tuwatunze hawa wazee wetu kwa sababu na wenyewe walikuwa vijana kama sisi. Sasa wanapofika katika ule umri mkubwa, naomba Serikali itusaidie basi kuhakikisha ile huduma inapatikana kikamilifu ili wazee wetu nao waendelee kuishi wakiwa na afya njema. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nami niungane na wenzangu walioongolea suala la Bima ya Afya. Kiukweli hili suala la Bima ya Afya ni kilio kikubwa. Hii Bima ya Afya CHF ambayo inatakiwa kwa wananchi wote bado kuna tatizo kubwa. Bado kuna tatizo kubwa. Tunaomba Wizara sasa ione mkakati upi wa namna gani ya kuboresha hiyo huduma ya Bima ya Afya. Utaona hata mwitikio kwa wananchi unaenda kuwa mdogo kwa sababu mtu anapokata ile Bima ya Sh.30,000 akitegemea anapata huduma katika zahanati au kituo cha afya, matokeo yake hapati dawa. Anabaki na ile hali kama ni mgonjwa atabaki na ugonjwa wake.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia hata unapompa rufaa kwenda hospitali ya wilaya anapata tabu ya kwenda hospitali ya wilaya kwa sababu hata nauli ya kwenda huko hana. Kwa hiyo, yule mtu anaendelea kupata tabu huku akiwa mgonjwa, anahitaji kuhudumiwa lakini huku anahitaji kutoa fedha zake ili aweze kupata huduma hiyo. Naomba huduma hii ya Bima ya Afya iboreshwe ili walau kama kweli tunahitaji wananchi wetu wapate huduma kwa kupitia Bima ya Afya, tuwe serious na jambo hili ili huduma hii itolewe.

Mheshimiwa Naibu Spika, nikija kwenye suala la NHIF. Ukiangalia huduma ya NHIF, watu wengi wamezungumzia humu ndani. Ni kwamba huduma hiyo bado inatakiwa iangaliwe tena upya. Kuna baadhi ya dawa ambazo ni muhimu, zinatakiwa ziwepo kwenye huduma hiyo ya Bima ya Afya. Mfano kuna dawa za sukari, pressure ambazo ni muhimu wananchi wapate. Tena ikiwezekana wapate bure maana ni magonjwa ambayo yanajitokeza, sio magonjwa ya kuambukizwa. Kwa hiyo, unakuta hiyo huduma haipo kwenye Bima ya Afya na inalazimu watu wanaanza kununua zile dawa kitu ambacho sasa ni gharama. Mtu anajiuliza kwa nini anakuwa na Bima ya Afya.

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine nishauri, kama itapendeza Serikali ione namna ambavyo yule ambaye ni mchangiaji tunakuwa na wale wategemezi. Sasa wale wachangiaji unakuta mtu hana mtoto, hana baba, mama, hana mume, hana mke lakini yeye ni mchangiaji namba moja. Wakati huo huo anakuwa na mtu ambaye anamtegemea kama mlezi wake aliyemlea, bima inamkataa yule mtu. Nafikiri tuangalie mfumo upya kwa sababu yule mtu ataendelea kuwa mtegemezi kwake na ataendelea kumhudumia na wakati huo yule mtu anaendelea kuchangia bima ya afya lakini hanufaiki, atanufaika yeye peke yake wategemezi watakuwa hawajanufaika na huduma hiyo ya bima ya afya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo naomba nichangie suala la ukosefu wa vituo vya afya katika maeneo yetu. Pamoja na jitihada kubwa ya Serikali, lakini bado katika maeneo yetu tuna changamoto kubwa ya ukosefu wa vituo vya afya. Natolea tu mfano katika Mkoa wetu wa Manyara, Wilaya ya Kiteto pale tuna vituo viwili vya afya. Sasa ukizingatia vituo viwili vya afya na zahanati 23 katika kata 23 kiukweli wananchi wetu bado wanafuata huduma mbali sana. Huduma hizi zisogezwe karibu na wananchi. Mheshimiwa Naibu Spika,

Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile hata kwa zahanati zilizopo hatuna vifaatiba, wananchi bado wanateseka kwa sababu vifaa tiba havipo na dawa hazipo na wakati huo huo tuna upungufu mkubwa sana wa watumishi wa huduma ya afya. Kuna zahanati zingine hata Madaktari tu hawapatikani, wamebaki kuwa watoa huduma. hivyo inawalazimu watu kwenda hospitali zingine na wengine kukosa hiyo huduma ya afya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru sana na naomba niunge mkono hoja. (Makofi)