Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mpwapwa
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. GEORGE N. MALIMA: Mheshimiwa Naibu Spika, niungane na wenzangu kuipongeza Wizara hii ya Afya kwa kazi nzuri ambayo inaendelea kufanyika. Naomba nichangie katika eneo la upungufu wa dawa. Kama ambavyo wenzangu wengi wameeleza, kuna shida kubwa sana ya dawa katika hospitali zetu lakini hasa katika vituo vya afya na zahanati. Mara nyingi vituo vya afya na zahanati viko vijijini na kule vijijini ndiko watu wengi walipo.
Mheshimiwa Naibu Spika, upungufu huu umesababisha kumekuwepo na mrundikano wa maduka ya dawa katika maeneo ya vijiji. Kusema kweli maduka mengi hayana sifa ya kuwepo. Hatari iliyopo ni kwamba hata wale wanaohudumia kuuza dawa zile, hawana utalaam wa kuuza dawa na kwa sababu wako vijijini hawafuatili. Kwa hiyo, watu wengi wanakunywa dawa ambazo wakati mwingine zimepitwa na wakati, zime-expire, lakini hakuna mtu anaweza kufuatilia mambo haya.
Mheshimiwa Naibu Spika, hawa wamechukua advantage kwa sababu ya upungufu wa dawa, wanajua kabisa kule kijijini hakuna dawa, kule kwenye zahanati hakuna dawa, kwa hiyo wanapeleka maduka na hawaweki hata watu professional. Anajua akimweka professional kwanza hatakaa kijijini lakini pia hawezi kumlipa mshahara, hivyo, anaweka mtu ni mtu. Kwa hiyo, yule anakuwepo pale, mtu akienda kutafuta dawa anachofanya anapiga ramli kwamba huyu anahitaji paracetamol lakini ukweli ni kwamba hajui na hiyo ni hatari tunaweza kujikuta tumeua watu wetu kwa sababu ya jambo hili.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nilikuwa nashauri Serikali maduka haya ya vijijini ya dawa yafuatiliwe. Kwanza kujua hawa watu wanaouza dawa wana utaalamu wa kuuza dawa hizo? Wanafahamu hizo dawa? Wana A, B, Cs za dawa?
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia wafuatilie waone hizo dawa hazijapitwa na wakati? Kwasababu kule mambo yanajiendea hivyo sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo ningependa kuchangia ni upungufu wa watumishi. Hili ni tatizo la nchi nzima, hospitali nyingi za wilaya, vituo vya afya, watumishi hawatoshi. Kwa mfano hospitali yangu ya Wilaya ya Mpwapwa ina upungufu mkubwa sana wa watu. Hospitali ile inatakiwa kuwa na wafanyakazi 310, lakini waliopo sasa hivi ni 152 ambayo ni sawa na asilimia 49. Ina upungufu wa wafanyakazi 158 ambayo ni sawa na asilimia 51; upungufu huu ni mkubwa sana na ndio maana unaona huduma hii pamoja na nia njema ya Serikali hakuna efficiency kwasababu, watumishi hawatoshi.
Mheshimiwa Naibu Spika, nishauri sana Wizara hii iangalie uwezekano wa kupata watumishi wa kutosha. Na hasa katika hospitali zile ambazo watu wengi wanazitegemea kama hospitali za wilaya na mikoa na zile hospitali za rufaa.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo ningependa kuchangia ni miundombinu chakavu katika hospitali zetu karibu zote. Ukienda katika hospitali za wilaya karibu nchi nzima, za mikoa, utakuta majengo mengi ni chakavu, lakini hakuna vifaa tiba. Kwa mfano ukienda katika hospitali ya Wilaya yangu ya Mpwapwa jengo lile la OPD limechakaa san ahata unasema hapa mazingira hayaruhusu kabisa kutoa huduma ya afya pale.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kuna majengo mengine, miundombinu ya maji-taka na maji-safi yote ni ya zamani na imeharibika, lakini pia umeme hakuna umeme wa uhakika, lakini hospitali ile ya Mpwapwa mpaka leo haina X-Ray, just imagine. Haina X-Ray wakati mwingine wanaazima kutoka kwenye kituo cha afya, X-Ray ya kizamani sana, lakini hospitali kama hadhi kama ya wilaya inahitaji kuwa na Digital X-Ray. Kwa hiyo, naomba sana Wizara iangalie sana Mpwapwa hakuna X-Ray tunaazima kutoka kituo cha afya ndio inakuja kutumika na X-Ray ile haina efficiency yoyote ni mbovu.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa huwezi kuhudumia watu wa wilaya nzima kwa kutumia vitu vya kubahatisha kama hivi. Kwa hiyo, Wizara nashauri sana hivi vitu vya miundombinu ni muhimu, hospitali zetu ziwe na vifaa tiba vya kisasa, ili tuweze kuendana na wakati, lakini pia huduma kwa watu wetu iweze kufanyika vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo ningetaka kuchangia ni juu ya bima ya afya kwa ajili ya wazee. Sera hii imetungwa siku nyingi, lakini sioni kama kweli Wizara inatoa hizi bima kwa wazee. Katika Wilaya yangu ya Mpwapwa nadhani ni katika wilaya chache ambazo hazina, wazee wengi hawana bima ya afya. Pamoja na bima ya afya, lakini pia wazee wetu hata wale wanaokwenda kwenye Dirisha la Wazee huduma haipo. Wazee wenye umri mkubwa unakuta wamesongamana msururu akifika kwenye dirisha anaambiwa dawa hii hamna kanunue mahali fulani. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ni jambo pia la kuliangalia sana, kama hakuna dawa ni afadhali wasipange foleni. Kwa nini wapange foleni watu wenye umri mkubwa wanarudi wanaumwa na dawa hawakupata? Si ijulikane moja kwamba, hakuna dawa wazee wasiende kupanga foleni. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la wizi Mheshimiwa mmoja amezungumzia sana habari ya wizi wa dawa. Na nimeona ukienda katika vijiji utakuta maduka ya dawa ni ya baadhi ya watumishi wasio waaminifu. Yeye ndiye anayeandika dawa kwa hiyo, anaandika dawa na anaelekeza nenda kanunue mahali fulani, lakini kijijini ni watu wangapi wanaweza kununua dawa?
Mheshimiwa Naibu Spika, wana bima ile iliyoboreshwa, lakini dawa pale hamna. Dawa zinaharibiwa na baadhi ya wahudumu ambao sio waaminifu kwa hiyo Serikali lazima iwe makini sana na wahudumu wa namna hii vinginevyo tutapigizana kelele hapa kila siku, huduma hazitakuwa nzuri, watu wetu wataendelea kuathirika na utaratibu huu ambao sio mzuri. Wizi wa dawa ni jambo kubwa sana linaloendelea sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)