Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Mbarali
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. BAHATI K. NDINGO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kupata fursa ya kuchangia katika Wizara hii ya Afya na Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto.
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kuipongeza sana Wizara kwa kazi nzuri na nzito ambayo wameendelea kuifanya. Pia nimpongeze Mheshimiwa Rais, Mama Samia Suluhu Hassan kwa hotuba yake aliyoitoa tarehe 7 kuhusiana mambo ya masuala mazima ya wazee. Kwa kweli, hotuba ile iliwapa matumaini makubwa wazee na tunashukuru kwa kutambua thamani kubwa ya wazee wa Taifa hili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunatambua tuna Sera ya Wazee iliyotungwa mwaka 2003 lakini mpaka sasa hatujaitengenezea sheria ya kusimamia utekelezaji wake. Hata kama tuna mipango mizuri na mikubwa kwa ajili ya wazee wetu kama tunakosa sheria ya kusimamia utekelezaji wa sera hizi, itakuwa ni ngumu sana changamoto za wazee kupata muarobaini. Kwa hiyo, nimuombe sana Mheshimiwa Waziri atakapokuwa anakuja ku-windup atuambie ni lini ataleta Bungeni sheria ya kusimamia utekelezaji wa Sera hii ya Wazee. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nijielekeze sasa kwenye vituo vya kulelea wazee vinavyomilikiwa na Serikali. Nitambue kwamba Serikali inafanya kazi kubwa kwa ajili ya wazee wetu na sasa hivi tuna vituo takriban 16 nchi nzima vya kulelea wazee, lakini hali ya vituo hivi kwa kweli inasikitisha. Mimi binafsi nimeshatembelea baadhi ya vituo vya kulelea wazee, niliwahi kwenda pale Fungafunga Morogoro miundombinu ya pale si rafiki. Ilani ya Chama cha Mapinduzi imetuelekeza kwamba wataenda kukarabati vituo 5 kama ifuatavyo: Kituo cha Kolandoto (Shinyanga); Kituo cha Nunge (Dar es Salaam); Kituo cha Njoro (Kilimanjaro); Kituo cha Magugu (Manyara) na Kituo cha Fungafunga (Morogoro). (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba wanapokwenda kufanya maboresho ya vituo hivi pia waangalie sana miundombinu ambayo itakuwa rafiki kwa wazee. Kwa mfano, pale Fungafunga (Morogoro) ukiangalia kile Kituo cha Wazee vyoo vyao viko nje kabisa ya sehemu wanazolala na wale wazee wanahitaji kusaidiwa kwa sababu ni watu ambao umri wao umekwenda sana.
Mheshimiwa NaibU Spika, kwa hiyo, niombe sana wanapofanya marekebisho ya vituo hivi waangalie miundombinu rafiki ambayo haitakuwa vikwazo kwa wazee wetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na miundombinu kuwa rafiki vifaa vya kuhudumia wazee kwenye hivi vituo hakuna, hata gloves za kuwasaidia wale wazee hakuna. Kwa hiyo, niombe sana sana Serikali vifaa viwepo kwenye vituo hivi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia kwenye vituo hivi vya Serikali huduma zinazotolewa mle ndani ni huduma za kwanza yaani mzee atapewa tu Panadol, ndio zinazokuwepo pale lakini ile huduma angalau inakuwa ni ngumu.
Mheshimiwa Naibu Spika, hivi vituo vingi vyao vipo nje sana ya miji na kusababisha wazee wengi kupoteza maisha kwa sababu ya umbali. Kwa mfano, hiki cha Fungafunga (Morogoro) kwa sababu nimeshakwenda hata barabara ya kufika pale kituoni hakuna, watu wanapita chini ya lile bomba la reli, hata gari zikifika pale kuleta dawa wanaenda na pikipiki wanavuka wanachukua ndio wanakuja kuzileta kituoni. Kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Waziri muangalie sana miundombinu ya hivi vituo vya wazee. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nilifurahi kusikia kwamba mna utaratibu wa kuanzisha uniform kwenye vituo vyetu vya afya, kwamba watu wanaohudumia wazee mtatoa uniform maalum ili mzee akifika pale ajue hawa ndio wanaohudumia wazee. Naomba katika utaratibu huo mwaangalie pia walemavu na viziwi ili wajue kabisa, kama mtaweka sare hizo kwa wazee muweke na sare pia kwa watu wengine ambao wanauhitaji maalum. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la pili, naomba niongelee kuhusu mambo ya vyoo. Magonjwa mengi sana yanatokana na ukosefu wa vyoo; usambazaji wa uchafu kutoka vyooni. Kuna kampeni moja ilikuwa inaongelea “Nyumba ni Choo.” Kampeni ile ilifanyika, lakini kwa vijijini kule bado suala la vyoo ni shida. Kwa hiyo, naomba sana, kampeni hizi za nyumba ni choo iendelezwe ili iweze kuleta tija mpaka kule vijijini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kule vijijini hakuna vyoo na maradhi mengi yanatokana na kukosa vyoo. Endapo Serikali mtaichukulia uzito hii Kampeni ya Nyumba ni Choo na vyoo vikawepo kwenye kila maeneo, itatusaidia sana kupunguza magonjwa mengi na itaisaidia pia Serikali kutopoteza fedha nyingi kwa sababu ya kukosekana magonjwa ambayo ni hatarishi. Kwa hiyo, niwaombe sana Serikali mjitahidi.
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
NAIBU SPIKA: Ahsante sana, kengele imeshagonga.
MHE. BAHATI K. NDINGO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana, ahsante. (Makofi)